Katika Nyakati Zile

Katika wasaa ule
Wa mwisho wa siku
Bado
Nabwa alitaka kuandika
Moyowe uli na simanzi:
“Punde itakuwa usiku…
Giza litazuka”
Mara vumph….
‘Kampiga bumbuwazi
Naye bado ana shauku
Ya kutaka kukumbuka
Bali nguvu ‘kamuhizi
Akafungwa vikuku
Akaporomoka
Masikini
Kumbe
Kurasa zilishafungika!

Ni nyakati kama hizi
Kimya kinenapo kuliko maneno
Likawa lamtoka chozi
Huku akiaga
Akipunga mikono
Isiyonyayuka
Akisema maneno
Yasiyosikika
“Adeyu wapenzi
Niliwahi kuwapo
Bali sasa…
Haya nd’o maagano!”
Masikini
Kumbe
Wino Ulishakauka!

Zilikuwa dakika zile
Mwisho wa furaha, mwanzo wa ukiwa
Zikaja kumbukizi, zamani za Dira
Kwake
Zama za kuneemewa
Akatamani apate
Upumzi mwengine
Na rohoye irudi ujana
Na kila kitu kiweze rejewa
Aendelee kuandika:
Siku Moja Itakuwa Kweli
Masikini
Kumbe
Kalamu yake ilishaondolewa
Na siku ya kuwa kweli…
Ilishatimia!

Basi ulishafika wakati
Japo tulitaka abakie
Ila yeye kuondoka…
Kulikuwa lazima
Ilishakwisha miezi
Ilishakwisha miaka
Saa yake
Ilishasimama
Mlango wa “Kutoka”
Ukafunguliwa
Wa “Kuingia” ukafungwa
Na akawa aambiwa:
“Nabwa fanya hima!”
Michirizi michirizi
Machozi yakatutoka
Sisi
Wanawe
Tukasimama wima
Hali twamwita:
“Baba, baba!”
Masikini
Kumbe
Taa yake ilishazima!

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.