Lau…!

Zimefika leo
Mia moja siku
Tangu nihame
Huko kuja huku
Na tangu nalipohama
Nekuwa hisema nanyi
Wenzangu wapenzi
Wenzi wa yetu biladi
Na leo
Hili liwe neno la mwisho
Kusema nanyi waungwana
Basi nisikizeni
‘Tasema nanyi kwa ghuna
Muijuwayo
Nawambieni lau…

Lau mwaweza tumai
Mwisho wa matunaini
Watu wanaporufai
Nyinyi mukawa makini
Muonwapo hamufai
Nyinyi mukajiamini
Katika dunia hiyo
Daima hatuwi duni

Lau mwaweza subiri
Kusubiri musichoke
Hata ‘kitenzwa jeuri
Hamuruhusu mutenzeke
Mukazuwia viburi
Na ujinga ‘siropoke
Wallahi mwawa jabari
Neno langu mulishike

Lau mwaweza jilaza
Mukaota ndoto tele
Ndoto zikafululiza
Bali zisiwatawale
Na lau mwaweza waza
Na mawazo yasiwale
Pepo ndiyo yenu jaza
Na uzima wa milele

Lau munastahamili
Pindi mambo ‘kichafuka
Muloyajenga dahari
‘Kaona yaporomoka
Nanyi mukawa tayari
Kujenga upya ‘kataka
Hapa panapo sufuri
Mwaweza kupaondoka

Lau mwatafuta tena
Baada ya kupoteza
Kila mulokosa jana
Leo mwanzo mukaanza
Pasina neno kunena
La nyoyo zenu kuviza
Basi kitapatikana
Na chengine ‘taongeza

Lau munajiinuwa
Baada ya kuanguka
Kisha mukajichunguwa
Kisa cha kuporomoka
Vumbi mukajikupuwa
Kisha njia mukashika
Safari yenu ‘ takuwa
Na mwendako mutafika

Lau mbele ya wadogo
Hamujipi utukufu
Wala mbele ya vigogo
Hamujifanyi dhaifu
Lau kubwa au dogo
Nyinyi haliwapi khofu
Nyoyo ‘tapunguwa zogo
Na roho ‘tawa nyoofu

Lau mema ya’ ndikwayo
Mwakaa mukayasoma
Na mazuri yasemwayo
Mwakaa mukayapima
Halafu mawili hayo
Matendoni ‘kasimama
Pepo mutakuwa nayo
Hamujafa mu wazima

Kwaherini!

Mohammed Ghassani
27 Mei 2007

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.