Tamko la Mzanzibari: “Zanzibar Daima…Jana, Leo na Kesho”

CUF Zanzibar

1
Ilahi kwa jina lako
Nianze hili tamko
Lifike nikutakako
Nako liweze pokewa

2
Lipokewe kwa hishima
Adabu na taadhima
Sababu anolisema
Hadhi yake alijuwa

3
Ni tamko la kusudi
La nia kuiradidi
La kuilinda ahadi
Na hishima ya uzawa

4
Ni tamko la kiapo
Nacho hakitangukipo
Wala hakitaangukapo
Na wala kugeukiwa

5
Ni tamko la shahada
Ni sehemu ya ibada
Na kwalo sina labda
Ni la hakika najuwa

6
Ni tamko la fakhari
Ya kuwa Mzanzibari
Tamko la ujuburi
Na kwalo sioni haya

7
Basi Mola natamka
Na hali nina hakika
Ni Wewe uliyetaka
Mimi hapa kuzaliwa

8
Vyengine ungeamuwa
Ndivyo hivyo vingekuwa
Kwengine ningezaliwa
Kukawa ni biladiya

9
Bali wewe Mola wetu
Ulitaka pawe petu
Zinjibari iwe yetu
Ndipo ukatugaiya

10
Tangu zamani za kale
Zama hizo za wavyele
Ulitaka iwe vile
Zinjibari biladiya

11
Waliotutangulia
Nchi wakatuachia
Na wanaofuatia
Wajibu kuikutia

12
Ndipo kwa huo wajibu
Tungo hii nakutubu
Iwe nayo ni sababu
Ya Watani kulindia

13
Nailinda nchi yangu
Kwamba ndipo hapa pangu
Ikiuka sina change
Niwezacho kiringia

14
Mtu kupenda Watani
Si tendo la kihaini
Bali li kwenye imani
Ni wajibu kisheria

15
Ni sheria na wajibu
Mtu nchi kuihubu
Watu hungia harubu
Watani kupigania

16
Nami kwalo naradidi
Kuna wale mahasidi
Lengo lao na kusudi
Nchi hii kuitwaa

17
La kwao kwangu ni vita
Ndilo watakalopata
Ndoto zao wanoota
Kwelini hazitangia

18
Na kushinda vita hivyo
Ni lazima nisemavyo
Navyo ndivyo niapavyo
Kwa jina lake Moliwa

19
Ni vita nisivyoweza
Kuthubutu vipoteza
Labda nife wa kwanza
Mapambanoni hingia

20
Labda nife nizikwe
Kaburini nifunikwe
Ndipo Watani nipokwe
Na mikononi kutwawa

21
Bali niwapo ni hai
Mzima sijarufai
‘Tapigana kwa inai
Kulinda Zinjibaria

22
‘Tapigana ardhini
‘Tapigana baharini
‘Tapigana na angani
Na popote patokuwa

23
Popote pale pawapo
Qitali kitangazwapo
‘Tanikuta nami nipo
Muhanga kujitolea

24
‘Tapigana ikomboke
Hishima ihishimike
Utukufu itukuke
Nchi yangu biladiya

25
Tapigana kwa silaha
Mungu alonijalia
Si ya kuua raia
Bali akili kunoa

26
Na kushinda ni lazima
Mithali nilivyosema
Nitapambana daima
Watani kujilindia

27
Nitaulinda Watani
Kwa nguvu na kwa imani
Kwa kudura ya Manani
Zenji yangu ‘tabakia

28
Na hivi si vita vyangu
Vyangu miye peke yangu
Ni vyangu na vya wenzangu
Wazanzibari jamia

29
Wazenji hivi ni vita
Siye vishavyotupata
Basi hatupaswi sita
Mstarini kungia

30
Ni vita tusivyoweza
Ushindi kuupoteza
Iwe nuru iwe giza
Kuwe mvua kuwe jua

31
Kushinda hivi lazima
Nchi ibaki salama
Tuwarithishe na wana
Kitu cha kujivunia

32
Wana wairithi kheri
Ya kuwa Wazanzibari
Kamwe wasirithi shari
Adha ya kutawaliwa

33
Waurithi utukufu
Kheri ya umaarufu
Wasirithi udhaifu
Uyatima na ukiwa

34
Uyatima si kukosa
Baba na mama kwa sasa
Uyatima ni kufisa
Nchi yako ya uzawa

35
Mayatima ndio hao
Watu wasio na kwao
Waso chao waso lao
Waso mava kuzikiwa

36
Na miye hilo sitaki
Wenetu wapate dhiki
Kisha wakose rafiki
Na bega la kulilia

37
Mtu hasa rafikiye
Si yule alaye naye
Walakini ni nchiye
Kitovu ilozikiwa

38
Watwani ndiye swahibu
Watwani ndiye muhibu
Watwani ndiye tabibu
Ndiye ponyo ndiye dawa

39
Ndipo hataka wenetu
Wairithi nchi yetu
Na warithi neno letu
La nchi kupigania

40
Wasipiganie mali
Wala vyeo na magari
Wapiganie kauli
Nchi yao ya uzawa

41
Zaidi tupiganavyo
Nao wapigane vivyo
Na hata tukifa kwavyo
Radhi roho zetu zawa

42
Akhera na duniani
Ni radhi mwangu moyoni
Tukiufia Watwani
Na kwao tukazikiwa

43
Rabbi kwa rehema zako
Lilinde hili tamko
Lende mbele nyuma mwiko
Lipe nguvu na satuwa

44
Lisimamishie kweli
Madhubuti mihimili
Na liwe sauti kali
Isiyodharauliwa

45
Lipe nguvu ya ajabu
Ulizompa Habibu
Kwenye Badri harubu
Ushindi akachukua

46
Lipe kila mantiki
Naliwe halipingiki
Naliwe halianguki
Hata linapotishiwa

47
Lifanye liwe ni hoja
Wapemba na Waunguja
Wote wajile pamoja
Nchi yao kukomboa

48
Liwe ni neno la wote
Wazenji wawe popote
Wakiuzwa wasisite
Tamko hili kutoa

49
Na miye nilitowaye
Ulinzinimo nitiye
Adui ‘sikaribiye
Njia kunizuilia

50
Salama usalimini
Nisikwame safarini
Uwashinde mafatani
Rabbi Wewe wawajua

51
Basi nilinde mjao
Kwa kheri ya ulinzio
Na hao niwambiao
Nao walinde sawia

52
Utulinde Mola wetu
Tuilinde nchi yetu
Tushinde adui zetu
Hasidi waone haya

53
Tuepushe Mungu wetu
Yalopatwa nchi yetu
Mwaka sitini na tatu
Na uliofuatia

54
Mwaka iliyochuuzwa
Nchi yetu ikauzwa
Na shimoni ‘kaingizwa
Kwenye mdomo wa chewa

55
Mwaka sitini na nne
Etuchuuza Karume
Akatutenda kinyume
Nchi yetu kuigea

56
Yeye na Mchongameno
Walifanya mapatano
Wakayeta Muungano
Jamhuri Tanzania

57
Hilo lekuwa ni pigo
Kubwa mno sio dogo
La kuitia upogo
Zinjibari baladiya

58
Karume etenda kosa
Nchi yetu kuitosa
Akidhani akinasa
Angeweza ‘jinasua

59
Karume alikosea
Muunganoni kungia
Sababu ni nia mbaya
Nyerere alonuia

60
Kule kwenye nia yake
Nyerere yuli na lake
Alimtega mwenzake
Na mwenzake akangia

61
Nyerere mbaya mno
Hakutaka Muungano
Alichotaka ndoano
Zinjibari kuitia

62
Alitaka aishike
Mikononi isitoke
Nchi hii iwe yake
Na wanawe alozaa

63
Etaka aidhibiti
Zenji isijizatiti
Choyoche na dhulumati
Zipate kutimilia

64
Aliwahi kutamka
Angeweza angetaka
Zinjibari kuifyeka
Baharini kuitia

65
Lakini uwezo huo
Nyerere hakuwa nao
Ndipo akafanya mbio
Makuchani kuitia

66
Akamtisha Karume
Kuungana aungame
Sivyo angoje aone
Atakavyopinduliwa

67
Naye Karume kwa woga
Kasumba ikamzuga
Akaitoa muhanga
Nchi alopigania

68
Msiba ukatufika
Nchi kufanywa sadaka
Ikapewa Tanganyika
Na bure-ghali ikawa

69
Hivyo ndivyo ‘livyokuwa
Madaraka kutwaliwa
Zenji ikapokwa pawa
Na nguvu za kuamua

70
Sivyo wanavyotamka
Udugu wa Afrika
Ndiyo sababu hakika
Nchi yetu kunyakuwa

71
Sivyo wanavyotamka
Kwamba ati Tanganyika
Na Unguja zilitaka
Udugu wao kukua

72
Na sivyo wanavyosema
Sababu ni usalama
Zinjibari ingekwama
Bila ya kuegemea

73
Vilivyo ndivyo ni kuwa
Walikwisha kuamua
Zinjibari kunyakuwa
Vyovyote vitavyokuwa

74
Wemfadhili Karume
Wakamtisha kiume
Kusudi mwisho akwame
Wapate mtumilia

75
Kwenye hili kwa hakika
Karume alitumika
Kupata wanalotaka
Muradi wao ukawa

76
Walijipanga zamani
Nyerere na wakoloni
Kuitia mikononi
Zinjibari baladiya

77
Mkoloni Mwingereza
Kusudi alifanyiza
Nchi kuiteketeza
Kwamba aliikhofia

78
Siku hizo Malkia
Na wenziwe ‘liamua
Hatari Zinjibaria
Huru itapobakia

79
Waliona Zenji huru
Itakuwa ni udhuru
Afrika kuwa nuru
Ya dini yake Nabiya

80
Fitinaye Mwingereza
Kwetu aliyoleteza
Ubaguzi ni wa kwanza
Akawagawa raia

81
Wagawe uwatawale
Ndiyo siasaye yule
Akajifanya mpole
Mnafiki alopea

82
Siasa za kinafiki
Mwingereza hazichoki
Kwazo bingwa wa fasiki
Wa majanga na balaa

83
Basi hasa dhamiraye
Si kutawala pekeye
Alotaka litimiye
Ni dini kuangamiya

84
Mwingereza hasidi
Wa diniye Muhamadi
Alilotaka kusudi
Dini ije kupotea

85
Aliumia moyoni
Kuona wa Visiwani
Wa kando kando na pwani
Wamfuata Nabiya

86
Bado engali na chuki
Na dola ya Kituruki
‘Livyoweza tamalaki
Kwa jina Islamiya

87
Kanisa Angilikana
Kiapo kaapishana
Lisingekaa ‘kaona
Nguvu hiyo inamea

88
Basi kila palipo dalili
Kufatwa dini ya kweli
‘Kasema hawakubali
Kuona paendelea

89
Na Zinjibari ‘likuwa
Na chembe za Thumaniya
Ghamidha zikawangiya
Lazima kuangamia

90
Basi kwayo wakapanga
Ya kichawi na kiwanga
Huku lengo walolenga
Nchi yangu kumegua

91
Walisema ikatike
Kila kipande na kwake
Kusudi itawalike
Na iweze nyambuliwa

92
Walianza na kumega
Kilwa, Mombasa na Tanga
Na kisha wakazitenga
Sehemu zenye da’awa

93
Ghibu karne nzima
Kabla ya kuja zama
Wazalendo kusimama
Kuudai uraia

94
Na zama zilipofika
Wananchi kuinuka
Uhuru wao kutaka
Mwingereza kang’amua

95
Mapema akafahamu
Ule wake udhalimu
Kwa Zanzibari adhimu
Huenda usije kuwa

96
Ili lisishindikane
Akaamua vyengine
Apate mtu atume
Wa lengo kulifikia

97
Kwa lake kukamilika
Ehitaji kibaraka
Atayeweza tumika
Tumo lolote la kuwa

98
Na mtu huyo sifaze
Ni lazima apendeze
Machoni awapumbaze
Awaghilibu raia

99
Wakasema wampange
Mtu huyo wamchonge
Kisha wamuengeenge
Hadi juu kufikia

100
Mzaliwa Butiama
Kwenye nchi ya Musoma
Ndiye waliyemtuma
Naye ‘kawatumikia

101
Fitina ya Mwingereza
Na Nyerere ikaweza
Mambo mengi kugeuza
Kwenye yangu biladiya

102
Wakabadilisha mambo
Ya mijini na viambo
Wakatunga na uongo
Na njia za kulindia

103
Kazi ikawa kulinda
Uongo waliounda
Kusudi tuwe mapanda
Wana wa Zinjibaria

104
Mkubwa ubaya wao
Walofanya watu hao
Ni kugeuza kibao
Cha tarikhi ya Visiwa

105
Tarehe ikageuzwa
Ubaguzi ‘katukuzwa
Na chuki kapandikizwa
Kwenye vichwa na vifua

106
Wakafanya taawili
Ionekane ni kweli
Muarabu ni katili
Waafrika ‘kaua

107
Mwenye damu ya Mwarabu
‘Kafanywa ajinasibu
Ni yeye mstaarabu
Mfanowe hatokuwa

108
Washirazi ‘kaambiwa
Peke yao ni wazawa
Na mwengine hatokuwa
Mwenyeji jina kupewa

109
Tukalazwa usingizi
Wazenji tusimaizi
Kamsahau Mwenyezi
Na dini yake Nabiya

110
Tukalazwa usingizi
Kwayo kali hino dozi
Mwishowe ni Mapinduzi
Nchi ikapinduliwa

111
Na hapa tusifichane
Ukweli tuambiane
Mwaka sitini na nne
Ni nchi ‘lopinduliwa

112
Ni nchi ilopinduka
Mchangani ‘kaanguka
Ikawa yapapatika
Pasiwe wa kuombea

113
Heangushwa Jamshidi
Wala Shamte Hamadi
Ni Zenji kifudifudi
Ndiyo ‘liyopinduliwa

114
Na wala walopinduwa
Wazanzibari hewawa
Wao bali wetumiwa
Lengongwa kulifikia

115
Hakupinduwa Abedi
Si Babu wala Rashidi
Bali Abal Hasadi
Ndiye hasa kapinduwa

116
Kufanywakwe Mapinduzi
Kulikusudiwa wazi
Kutia kwenye kitanzi
Zinjibari baladiya

117
Ilitakiwa hakika
Nchi hii kutoweka
Na lengo hili kufika
Mapinduzi ‘kawa njia

118
Mapinduzi ‘metumiwa
Si lengo bali ni njia
Lengo hasa lilikuwa
Muunganoni kungia

119
Mapinduzi, Muungano
Ni vitu vya mfanano
Lilo lilo moja neno
Biru lilobiruliwa

120
Sababu ya Mapinduzi
Ni Muungano kwapuzi
Na hilo ‘mewekwa wazi
Na watu wanaojua

121
Nyerere alitumiwa
Kwa mwenyewe kuamua
Kwamba liwe litokuwa
Zenji angeichukua

122
Alilia kiapo
Malkia ampapo
Limshindalo halipo
Liwezalo mzuia

123
Kutimiza jambo hilo
Akapewa atakalo
Lolote aamuwalo
Akawa asapotiwa

124
Dola ya Muingereza
Daima ‘limtukuza
Nyerere ilimkweza
Kama mwana wa kuzaa

125
Ndiyo iliyomlea
Ndiyo ilomnyanyua
Na siku ‘lipowadia
Ndiko alikokufia

126
Vile ati kuradidi
Kwamba ni Vita Baridi
Marekani uhasidi
Ndio ulotulemea

127
Ati pale ‘lipoona
Mapinduzi yanafana
Na watu wenye dhamana
China wameegemea

128
Hima wakakurupuka
Marekani wakataka
Inyanyuke Tanganyika
Zinjibari kuitwaa

129
Ikatafutwa sababu
Kuwashinda kina Babu
Carlucci akaratibu
Na Muungano ukawa

130
Au na vile kusema
Karume yake azima
Ni Nyerere kumchuma
Pawaye kumlindia

131
Kwamba hakukusudia
Kwenye ndoa kubakia
Bali alidhamiria
Punde angelijitoa

132
Ni kweli yalisadifu
Matokeo yakakifu
Bali ni hoja dhaifu
Kusema ndivyo vikawa

133
La kweli na la mizani
Huu uli ukoloni
Uliopangwa zamani
Na bado umebakia

134
Muungano ni alama
Waziwazi inosema
Kwamba Zenji si salama
Wala huru haijawa

135
Muungano ni kichonge
Cha ukoloni mkongwe
Uhusiano mazonge
Na wenye dhamira mbaya

136
Muungano ni ishara
‘Livyotupata hasara
Kupoteza yetu dira
Na heshima ya uzawa

137
Hili ni kumi la nne
Tangu nchi ziungane
Ila hisabu uone
Mangapi yametokea?

138
Ni lipi tulilotoa?
Lipi tulilopokea?
Na lipi lilobakia
La sisi kujigambia?

139
Tumepotezewa dira
Nchi yetu ‘medorora
Kila kitu sasa Bara
Ndiyo inayoamua

140
Tumepoteza hishima
Ya pamoja kusimama
Kama si baba na mama
Mmoja alotuzaa

141
Tumepoteza kauli
Ya mambo kuyaamili
Tukaipeleka mbali
Dodoma ‘kaichukua

142
Tumepokwa kila kitu
Kale kilokua chetu
Kwa maguvu ya wenzetu
Hasidi wamekitwaa

143
Tumevuna udhalili
Na dharau na kejeli
Za nahari na laili
Za kupwa na za kujaa

144
Tumepokea mashaka
Mabalaa na wahaka
Nchi kuchwa yaripuka
Na neema yapotea

145
Tumepokea mzozo
Wa sizo kuzeta ndizo
Na sasa kwenye uozo
Zenji inaogelea

146
Kipi kilichobakisha
Kuweza kuijulisha
Ingalipo haijesha
Nchi yetu ya uzawa?

147
Kipi kama si imani
Tulonayo kwa Watwani
Iliyoganda nyoyoni
Waloshindwa kuitoa

148
Walichoshindwa pekee
Ni kufanya ipotee
Zanzibar iambae
Kwenye nyoyo za raia

149
Hilo jambo hawawezi
Japo wamefanya kazi
Kubwa ya kutubazazi
Na fitina mbaya mbaya

150
Tumepokwa kila kitu
Bali si imani yetu
Wala uzalendo wetu
Kwa Mama alotuzaa

151
Bado Mama twampenda
Bado kwake tumeganda
Twataraji kushinda
Mbele anotukalia

152
Mbele anotukalia
Akaziba yetu njia
Na nchi yetu kutwaa
Hatukubali raia

153
Na kheri tungelikuwa
Kwa khiyari twaitoa
Si kwa maguvu na riya
Na ya nchi kukaliwa

154
Ingelikuwa khiyari
Tungepata ujuburi
Wa kusema tu tayari
Machungu kuvumilia

155
Lakini ni ukwapuzi
Na wa nchi uvamizi
Kuwa chini ya ulinzi
Huku tumetawaliwa

156
Hadi lini hadi lini
‘Tadumu huu uduni?
Na ushenzi na uhuni
Sisi tunaofanyiwa

157
Hadi lini tutakuwa
Watu wa kuamuliwa
Na wale wasotujuwa
Wala wasotutambua?

158
Hadi lini ukoloni
Wa Tanganyika nyumbani
Tuwe tunauamini
Kwamba watusaidia?

159
Basi sasa iwe basi
Kugeuzwa matopasi
Basi kunyimwa nafasi
Na nguvu za kuamua

160
Na hino ndilo tamko
Na ni kwetu litokako
Tunasema sasa mwiko
Nchi hii kuonewa

161
Sasa twasema hakika
Mambo tunayoyataka
Ni mawili kufanyika
Hima yasijechelewa

162
Mawili yafuatayo
Twayataka leo leo
Wala si mtondogoo
Ndivyo tushavyoamua

163
Hima mno yafanyike
Yatendwe yakamilike
Ama sivyo tuinuke
Tufanye tunolijua

164
La kwanza tunalotaka
Ni Mkataba kushika
Humo yaliyoandikwa
Ndiyo tunoyatambua

165
Mkataba unataja
Mambo ni kumi na moja
Ndiyo Pemba na Unguja
Ziliyoyakubalia

166
Ni hayo ndiyo ambayo
Siye tuyatambuayo
Na wala si mengineyo
Juu ‘liyoongezewa

167
Zanzibari itwaye
Hayano madarakaye
Kisha ndiyo iamue
Lipi la kuendelea

168
Pili hayo hidashara
Twataka yaje shahara
Tujadili njia bora
Ya yano kuyaendea

169
Tujadili turidhike
Lipi humo tulishike
Na lipi tuliepuke
Lipi silo lipi sawa

170
Kisha kura ya maoni
Iamue jambo gani
Ama Muunganoni
Ama nje kubakia

171
Kura ipigwe haraka
Wananchi kuwataka
Kuamua kuuweka
Na ama kuuondoa

172
Hilo ndilo tusemalo
Wazenji tulitakalo
Kinyume na jambo hilo
Hatukhofu kuamua

173
Laiti hayatokua
Basi koti twalivua
Hakuna tunochelea
Wala tunachokhofia

174
Lau kama hawataki
Muungano kuhakiki
Kauli yetu ya haki
Ni kuvunja hii ndoa

175
Hatuchelei kutoka
Muunganoni hakika
Lakini tunalotaka
Pawe haki na usawa

176
Fitina naisitishwe
Na vitisho tusitishwe
Na wao nawakumbushwe
Kwamba sisi ‘meamua

177
Kama waja wa kusoma
Basi waone alama
Mbele zilizosimama
Za wakati kufikia

178
Wasome nawaelewe
Kisha nao waamuwe
Kwamba ni sisi wenyewe
Sasa tuliopania

179
Ni sisi Wazanzibari
Ambao sasa twakiri
Kwa kheri ama kwa shari
Hatutaki ‘tawaliwa

180
Hatukatai umoja
Nasi kwao tuna haja
Bali linalotufuja
Ni huku kutawaliwa

181
Twakataa ukoloni
Wa Dodoma us’o soni
Unaoua imani
Na hishima ya raia

182
Mwisho wa hili tamko
Rabbi naja tena kwako
Nilinde kiumbe chako
Kama nilivyozowea

183
Nimezoea ulinzi
Wako Ilahi Mwenyezi
Basi nipe ‘sinihizi
Niepushie balaa

184
Nilinde na mahasidi
Nilinde na mafisadi
Nilinde na makuwadi
Nchi waloikamia

185
Kile kilichobakia
Kwenye yangu biladiya
Kilinde kisijetwawa
Nacho kikeshapotea

186
Ilinde na dini yako
Walinde na waja wako
Iwe kwa hili tamko
Mwanzo wa kutuongoa

187
Ilahi tupe umoja
Wapemba na Waunguja
Tuweze kujenga hoja
Ya nchi kujilindia

187
Ya Rabbi tupe mapenzi
Tuchukie ubaguzi
Tushikane kama wenzi
Mapacha tuvyozaliwa

188
Ya Karima Mola wetu
Hupungukiwi na kitu
Ukitupa nchi yetu
Kama vile ‘livyokuwa

189
Kwako Bwana tuombacho
Sio zaidi ya hicho
Tufumbue yetu macho
Na nuru kututilia

190
Tuwezeshe kung’amua
Kosa tulilokosea
Kisha tuongoze njia
Ya hapa kujinasua

191
Lau hii ni adhabu
Kwa mambo tuloharibu
Kwako Ghafaru twatubu
Na toba zetu pokea

192
Zipokee toba zetu
Ufanye ujira wetu
Ni kutupa nchi yetu
Kama vile ‘livyokuwa

193
Wewe Bwana hufundishwi
Na wala hurekebishwi
Na wala hulazimishwi
Watenda unoamua

194
Ukitaka jambo kuwa
Husema “Kuwa” likawa
Sababu u mwenye quwa
Na ilimu is’o doa

195
Lakini hatuna budi
Kukuomba Ya Wadudi
Sisi ni wako ibadi
Tunayekutegemea

196
Kwa rehemazo Wadudi
Na dua za Muhammadi
Tumiminie suudi
Bariki hivi Visiwa

197
Swala nyingi na salamu
Zende kwa Abu Qassimu
Na sahabaze kiramu
Na wakeze wote pia

198
Na wote maiti wetu
Wazazi nao wenetu
Warehemu Mola wetu
Kwa Fatiha tun’otia

199
Mwisho mtunzi yakini
Ndimi mwana wa Ghassani
Kwetu utunzi si shani
Ni jambo tulozowea

200
Yangu pekee kalima
Ni Zanzibar Daima
Kwa leo hata Kiama
Iwapo na itamea

Mohammed K. Ghassani
2 Oktoba 2008
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

  1. Heko kwa kazi nzuri. Huu ni utenzi mwanana na safi kabisa! Natamani ungechapishwa katika kitabu ukasambazwa pembe zote za Unguja na Pemba. Ukaibwa na watoto wa skuli na katika kila kila mikusanyiko ya watu kwa shughuli mbali mbali.

    Wazanzibari walio wengi bado wamelala usingizi mzito na walioamka bado macho yao yamejaa matongo. Utenzi huu unaweza kusaidia kuwaamsha waliolala na kufuta matongo ya wale ambao bado hawawezi kuona.

    Endelea na kazi nzuri.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.