Chetu Chao, Chao Chao

Naandika kwa kilio, machozi hadi viatu
Wino ndilo kimbilio, na shahidi Mola wetu
Nayawahi haya leo, bado ningalithubutu
Naliwahi hili bao, bado lingali ni letu
Sababu hatuna chetu, vyote vishakuwa vyao

Nisaidiani kilio, tulieni wanakwetu
Tuliliye tufanywayo, tuporwapo haki yetu
Iyoneni hiyo hiyo, yatolewa ndani mwetu
Wanayo wenenda nayo, wasema yao si yetu
Ya Ilahi Mola wetu, hebu lete hukumuyo!

Utesi si kusudiyo, naicha gowe si kitu
Bali hichi ni kiliyo, chozi letu na wenetu
Twalia tupokonywao, tupokwapo kilo chetu
Twalia watupokao, na kale wali wenzetu
Cha kwao wao si chetu, lakini chetu ni chao

Tazamani muonao, onani hiyo papatu
Haya wayachukuwayo, yetu siye mali yetu
Wazitwaa hata nyoyo, hata hizi roho zetu
Na miili ndiyo hiyo, sasa waujia utu
Punde ‘takuwa vibutu, yote washakwenda nayo!

Ni uchungu unipao, na nguvu na jasho letu
Kwani chao kiwe chao, chetu kisiwe ni chetu?
Kwetu kuwapo ni kwao, kwao hakuwini kwetu?
Mungu hakuwapo vyao, shuruti watwae vyetu?
Kwa nini hatuna chetu, tulichonacho ni chao!?

Mohammed K. Ghassani
1997
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.