Punda

Kwatakwata na mdundo, punda jasho lakutoka
Punda wenda kwa kishindo, mwendo mchaka mchaka
Mgongoniko ni rundo, bahasha la taka taka
Na bwana fimbo kashika, punda uongeze mwendo

Punda zigo ulobeba, limejaa takataka
Zigo halina haiba, lanuka vundo lanuka
Ya bwanao matilaba, hata yakitimizika
Wewe hutofaidika, hutosinza, hutoshiba!

Punda jifanye hujali, ujikaze kakakaka!
Juu kijua kikali, chini nchanga wafuka
Na bakora mbili mbili, bwanao akutandika
Nawe umo wachapuka, umo wazikata meli!

Punda kwa wako ujinga, ‘kitumwa unatumika
‘Mejitolea muhanga, japo unatilifika
Wakanyaga vifaranga, zigo liweze kufika
Bwana kupata ridhika, ndilo punda unozinga

Punda! Nyama kubwa punda, lakini umepotoka
Nyama wenzio waponda, bwana apate ridhika
Na jazayo ni kibanda, na bakora na kuchoka
Na bado watutumka, pa kwenda zigo wenenda

Mitaani ukipita, watutia patashika
Watoto huwauwata, kwa mateke kuwanyaka
Wenda mbio kwatakwata, zigo lipate kufika
Na hata likishafika, huna unalolipata

Ponda, tafuna, kanyaga, dai umelazimika
Piga, sondoga sondoga, ili upate sifika
Jifuwe, nguruma, uga, zigo liweze kufika
Hadi ukishakongoka, manyanga utayabwaga

Mohammed K. Ghassani
1996
Pemba

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.