Ulipopata Bunduki

Ulipopata BUNDUKI:
Hukukaa msituni
Bali wekaa mjini
Kwenye raha kila fani
Soda, kuku na Pajero!

Ulipopata MIKUKI:
Hukuchoma wazandiki
Bali ulipinga haki
Ukawa u mamluki
Wa madhalimu kulinda!

Ulipopata MASHOKA:
Majambazi hukufyeka
Wanyonge ‘lodhalilika
Haki yao wakitaka
Wekwenda wachangachanga!

Ulipopata na SIME:
Ukajiona u dume
Ukasubiri waseme
Wananchi uwachome
Hadi ukarowa damu!

Ulipopata SAUTI:
Ukaanza usaliti
Ukauwacha umati
Kwa bwanao ukaketi
Butile kurambaramba!

‘Lipopata na UWEZO:
Ndipo ukaanza bezo
La sizo kuzeta ndizo
Kwamba u kwenye mchezo
Na sasa upewe nini?

JIBU KWA SHAIRI LA MOHAMMED SEIF KHATIB ‘NIKIZIPATA BUNDUKI’

Mohammed K. Ghassani
Februari 2001
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.