Yana Mwisho

Haya! Kuwa ongezeka, jipe nyadhifa na vyeo
Jifanye umetukuka, kwa deko, ringo na shoo
Bali utavyotanuka, juwa una hatimayo
Yangakuwa maguuyo, mawingu hutayafika

Vyovyote ‘tavyonyuuka, anguko ndio mwishowo
Anguko utaanguka, mithali waangukao
Wangapi ‘shaporomoka, walokuwa mfanowo?
Basi nawe kwa mwendowo, sikuzo zahesabika

Huna utavyokubwika, ‘sivyojiumba mwenyewo
Madhali umeumbika, wetu ndiye Muumbawo
Juwa siku itafika, tukufunike ubao
Zaidi ya amaliyo, huna utalojitwika!

Zidisha kupumbazika, tuione khatimayo
Kila lipeapo joka, Mungu hulipaza mbiyo
Nawe unavyolanika, yakujiayo ni yayo
Kila ngoma ivumayo, ni punde itapasuka!

Ubaya si kuondoka, wangapi waondokao?
Ubaya ni kuondoka, kwa aibu na jojeo
Watu wakakukumbuka, kwa baazo na shariyo
Ikawa kwa mautiyo, watu wanashereheka.

Haya! Lewa, pumbazika, jivune kwa manenoyo
Haya! Vuma, kashifika, utishe kwa matendoyo
Walakini juwa fika, yote yana mwisho hayo
Wababe wa kablayo, wawapi? Washatoweka!

Mohammed K. Ghassani
1996
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.