Habibi Zenj!

Ungalinipa dhahabu, almasi na yakuti
Na makasiki ya fedha, na mabakuli ya wati
Kwa kutaka niiwache, Zenji yangu siiwachi
Ni radhi utwae yote, lakini si kitu hichi
Kwamba ndiyo roho yangu!

Zenji ndiyo roho yangu, pumzi na wangu moyo
Hiyino jigambo langu, na utukufu na cheyo
Bila Zenji sina changu, litabaki jongomeo
Ndipo haapa kwa Mungu, popote Zenji ninayo
Kwamba niwe maishani!

Najiona maishani, Zenji yangu ‘kinawiri
‘Kiniuza watakani, panapo mambo mazuri
Penye sufi, melmeli, na libasi za hariri
‘Takwambia sijatoshwa, nikosapo Zinjibari
Hiyino yangu imani!

Zenji ni yangu imani, na hilo sifanyi siri
‘Kiniuliza ni nani, ‘tamba ni Mzanzibari
Nikifa nizikwe wapi, hapa hapa Ziinjibari
Ukoshwe muili wangu,
Iswaliwe maiti yangu,
Libebwe jeneza langu,
Na ndugu zangu, watu wangu, Wazanzibari
Ardhi ya Zenji inisitiri!

Nikifa Zenji i hai, ‘tajiona sijakufa
Bali Zenji ‘kipotea, pumzi ingalimofa
Sitajiona naishi, kwangu hayo ni maafa
Bora nende miye mwanzo, lau Zenji itakufa
Sitaweza kuhimili, kuingojea kashifa
Lau yatafika hayo, Mola nitwae kabisa!

Mohammmed K. Ghassani

About Zanzibar Daima 1609 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.