Kiza cha Nyoyo

Bwanatosha shukrani, mwanao kunijuliya
Tupoe sote wendani, Watani yakwangamia
Mbele ya zetu uyuni, mambo yatuharibikia
Ndilo niloshuhudia, nilipokwenda nyumbani

Majuzi nili nyumbani, wana kuwadamkia
Nalokuta Kijiweni, hiyakumbuka nalia
Si totoro mitaani, pekee ilikongia
Kiza hiki ki pabaya, kwamba ’mengia nyoyoni

Kiza ki tele nyoyoni, Wazenji kimewajaa
Hawahisi hawaoni, ’mekufa zao hisia
Natamani natamani, taa ningewawashia
Mambo yakazieleya, nafusi zi duniani 

Wakajuwa duniani, hayatendwi mambo haya
Kwamba wanayo thamani, ipaswayo kutetewa
Wala hilo si hisani, ni wajibu kutendewa
Lau wangejua haya, miji haiwi kizani

Isingekuwa kizani, Malindi wala Sogea
Makunduchi, Mkwajuni, na Donge kungeling’aa
Lau si kiza nyoyoni, umma kilichowavaa
Tungeweza kiondoa, kiza hiki mitaani

 Naona cha mitaani, si kiza cha kushitua
Lau kuwa nafusini, nuru ingelizagaa
’Singethubutu Amani, kuwakebehi raia
Kwamba wao waumia, yeye nje ziarani

Mohammed K. Ghassani
Dar es Salaam
13 Juni 2008

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.