Wataamka!

Wataamka, nasema wataamka, nalo nelisema kale
Wataamka, punde muda ukifika, kwanza wawache walale
Wataamka, kwa majogoo kuwika, na jua kuvya mishale
Wataamka, kwa kwisha kupambazuka, na kwa kwisha tongo zile!

Wataamka, lazima wataamka, uwatoke mzukule
Wataamka, damu ‘navyowazunguka, wa hai si wafu wale
Wataamka, ndoto ikimalizika, wajione pale pale
Wataamka, ‘kijua ‘medanganyika, na walaani: ‘Kyefule!”

Wataamka, shuruti wataamka, apingaye shaurile
Wataamka, tena haraka haraka, na wala si pole pole
Wataamka, na langoni watatoka, bawabu atupwe kule!
Watamka, ‘madhali washageuka, ‘melala ubavu ule

Wataamka, naapa watamka, kwa macho na tongo zile
Wataamka, walitupe mbali shuka, kitandani wakimbile
Wataamka, wende nje kwa kusaka, wazinge riziki wale
Wataamka, matumbo yakiwawaka, njaa kwa mwari ni ndwele!

Wataamka, wenyewe wataamka, nasema lile kwa lile
Wataamka, kama walivyoamka, wale walolala kale
Wataamka, kisha watachangamka, kisha kamwe wasilale
Wataamka, dozi ikimalizika, na wote wenende mbele

Wataamka, vyovyote wataamka, wanyanyuwe na vidole
Wataamka, waitwe na kuitika, wauzwapo watongole
Wataamka, mzugo ukiwatoka, pumbao la mkobele
Wataamka, ndere ikishawashika, Bi Kirembwe ambwe: “Pole!”

Wataamka, tamati wataamka, ikishalia kengele
Wataamka, na mbiyo ‘takurupuka, iwe sumile sumile
Wataamka, si kwa mimi kuwataka, wala si zangu kelele
Wataamka, kwa kwishatimu dakika, na sababu wasilale!

Mohammed K. Ghassani
1999
Zanzibar

 

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.