Zama Mauti Yakija

Zama za kufa zikija:
Zije ningali ni mtu, sijageuka nguruwe
Sijakuwa nyama mwitu, azaaye na wanawe
Zije bado nina utu, hiondoka nililiwe
Hishima tuwe pamoja

Mauti yakinif’ata:
Yanif’ate pirikani, njiani roho itwawe
‘Sinikute barazani, nacheka hipiga yowe
Nife kikondoo kwani, nami ni simba mwenyewe?
Simba hufa kwenye kwata

Siku yangu ikifika:
Ifike ningali ni chumvi, mithali umuhimuwe
Wanihitaji wajuvi, wahisi waondokewe
Nisife kifo uchimvi, hata tanga ‘siekewe
Kufa huko ‘singetaka.

Safari yangu ‘kijiri:
Ijiri siko fakiri, kwamba sanda nikopewe
Bali nisife tajiri, utajiri kwangu kiwe
Nisife na matajuri, bali na deni nisiwe
Deni si mwenza mzuri

Pumzi ikinihama:
Inihame sijidani, mauti yanichukuwe
‘Sinihame matungini, ama hicheza msewe
Nanife ni muumini, msala chozi utowe
Uliliye ulitima

Buku langu likifungwa:
Lifungwe bado ghulamu, dunia ipungukiwe
Lifungwe ‘ngali na hamu, hitaka lifunuliwe
Nife na wangu utamu, ufavyo muwa ufuwe
Nisife nikisimangwa

Mohammed K Ghassani
1997
Pemba

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.