Zanzibar Njema

Juwa lenda machweoni
Linazama baharini
Dhahabu yake launi
Na mvuvi kidauni
Arudi toka mavuvi

Mwisho huu wa jioni
Kutoka mbali ya pwani
I wazi sura yakini
Mandhari ya watani
Zinjibari mji mwema

Aona upendezavyo
Mataa yaangazavyo
Aupenda unga’ravyo
Lakini afikirivyo
Umeme ni wa kukopa!

Inamjia kichwani
Taswira ya bustani
Darajani, Forodhani
Bali mara haioni
Aona shida ya maji

Mvuvi anawazia
Mauwa yakichanua
Rihi njema yanukia
Kisha mara wamjia
Uvundo wa karo chafu

Mule mwake fikirani
Aona yu Mazizini
Kwenye jumba la roshani
Ila mara yu Pandani
Na kivuruche kibovu

Fikira haijakoma
Hali aloacha nyuma
Mtotowe yuna homa
Naye mzazi mzima
Pesa tano hatimizi

Aitazama bandari
Vile ilivyonawiri
Mameli na matishari
Kichwanimwe afikiri
Kwani afe masikini?

Ajiuliza sababu
Maishaye kuwa tabu
Kutwa pwani na sulubu
Bali hapati jawabu
Hata apate iweje?

Naye yumo kuwazia
Mara king’ora chalia
Magharibi ishangia
Mvuvi ajinamia
Huku amwaga machozi!

Mohammed K. Ghassani
1998
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.