Ishachipuka

Tungo weye nakutuma, nawe tumika haraka
Kamwambie mkulima, mbegu mwenye kuz’atika
Mbona kuja kanakwama, na zizo zishachipuka?
Basi naje hima hima, kondeye yaharibika

Ndimi ninayekutuma, shahidi alipofyeka
Mgongo ‘lipoinama, huku kijua chawaka
Neepo himtazama, ayandamavyo mashaka
Basi mwambe muadhama, mbeguze zishachipuka

Jitihadaye ya nyuma, ya kuchukuwa nafaka
Mwambe Ilahi Karima, kamtilia baraka
Mbeguze ‘mekuwa vyema, na miche ishachipuka
Naye ni mosi nzima, shambanikwe hajafika

Basi lau yu mzima, sihaye haina shaka
Mwambe nduguye asema, aje haraka haraka
Miche yataka huduma, ipate kunawirika
Kwamba akizidi kwama, magugu ‘taifunika

Mwambie afanye hima, magugu kuja yafyeka
Lau sivyo hatachuma, mazao aliyotaka
Ajuwe yu mkulima, hapaswi kutamauka
Nguvu ashazojituma, ‘siziwache dedereka!

Mohammed K. Ghassani
21 Novemba 2002
Bonn

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.