Hiyari isiyoradulika!

Sijapewa kwa jojeyo, wala kusukumiziwa
Wala siko kwenye mbiyo, niko tuli nimetuwa
Si majununi wa hayo, akili yangu i sawa
Naambiwa hiyariyo, mwana la kulichaguwa
Ila pamoja na hayo
Unashidwa wangu moyo
Kwa sababu yote ndiyo, ninashidwa kuraduwa

Unashindwa wangu moyo, unashindwa kuraduwa
Hauyajui yasiyo, yenye kasoro na dowa
Wala kuyatwaa ndiyo, yapaswayo kutwaliwa
Kwako ni yayo kwa yayo, hauwezi yabaguwa
Na bali yaniumayo
Si ruhusa kwenda nayo
Shuruti liwe chaguo, yote siwezi yapewa

Siachiwi kwenda nayo, yote nikasabiliwa
Langu ni moja ya hayo, lolote ningaraduwa
“Jengine ni la mweziyo” ndivyo ninavyoambiwa
Ninababaika nayo, mara shika mara tuwa
Mara hili ndilo ndiyo
Kisha ninaona siyo
Na ndipo kwa hali hiyo, kuyawacha naamuwa

Mohammed K. Ghassani
1998
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.