Kundi la I-ZI: Urahisi na ugumu wake

Kama katika makala iliyotangulia, ninasisitiza tena unasibu katika lugha, sifa ambayo ni ya jumla kwa kila lugha na sio Kiswahili pekee. Mpwa wangu, Khelef Nassor, ameifafanua vyema zaidi dhana hii katika mchango wake kwenye mada iliyopita. Leo tuzungumzie kundi la majina la I-ZI, msisitizo ukiwa urahisi na kile kinachoweza kuitwa ‘ugumu’ wake. Hii nukta ya ugumu ninaiwekea alama makusudi, maana inahojika zaidi.

Imesadifu tu kwamba neno la Kiingereza ‘easy’ ambalo kimatamshi linakaribiana sana na I-ZI, lina maana ya rahisi au -epesi. Basi, kwa masihara, huwaambia wanafunzi wangu kuwa kundi hili pia ni rahisi na jepesi sana. Kwa nini na kwa vipi?

Kwanza, majina yote kwenye kundi hili hayana viambishi vinavyoashiria umoja na wingi, bali umoja na wingi wake hujuilikana katika muktadha ambao neno linatumika. Kwa mfano, tunajuwa ikiwa inakusudiwa nyumba moja au nyingi, ikiwa tu sentensi iliyosemwa imeonesha hivyo na sio jina tu – nyumba.

Inaposemwa “nyumba hii imejengwa mwaka jana”, tunajuwa kuwa imekusudiwa umoja. Inaposemwa “nyumba hizi zimejengwa mwaka jana”, tunajuwa imekusudiwa wingi. Lakini linaposimama peke yake, umoja wa nyumba ni nyumba na wingi wa nyumba ni nyumba. Ndivyo yalivyo maneno yote yaliyomo kwenye kundi la I-ZI. Huo ni urahisi kwa wanaojifunza Kiswahili.

Pili – isipokuwa katika mifano michache – kundi hili linasimama kama kapu linalokusanya majina yote yaliyotoholewa kutoka lugha za Ulaya, Asia na Arabuni. Hoteli, ofisi, skuli, kompyuta na picha ni mfano kutoka Kiingereza. Shule, zahanati kutoka Kijerumani. Meza na pesa kutoka Kireno na Kihispania. Talaka, hisia, fikira, sura, aya, serikali kutoka Kiarabu. Huo nao ni urahisi wake.

Lakini pia ndio ugumu wake. Kwa sababu ile ile ya sifa ya lugha kuwa sauti za nasibu, basi si kila jina kutoka lugha Kiarabu au Kiingereza huingia kwenye kundi la I-ZI. Vile vile, kundi hili halikufunga milango yake kwa majina mengine yenye asili ya lugha za Kibantu.

Japo katika mifano michache, utakuta majina mengine yaliyotoholewa kutoka lugha za Ulaya, Asia na Arabuni hayamo kwenye kundi hili, lakini unaweza kukuta majina mengine yenye asili ya Kibantu ndani yake.

Majina kama friji, feni, begi, koti, kabati, kwa mfano, asili yao ni Kiingereza lakini yanaingia kwenye kundi la LI-YA. Majina kama nyumba na nyota yana asili ya lugha za Kibantu lakini yamo kwenye I-ZI.

Na huu ndio utamu wa lugha. Nasibu. Sadfa.

About Zanzibar Daima 1614 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

3 Trackbacks / Pingbacks

  1. Majina yenye wingi na au kundi zaidi ya moja | Kiswahili Kina Wenyewe
  2. Yaliyomo kwenye kundi la YU-A-WA | Kiswahili Kina Wenyewe
  3. Eti ”Hauwezi kumaliza shuuli zote izo kwa lisaa limoja” | Kiswahili Kina Wenyewe

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.