Naitwa Mwana Ghassani

Ndimi mwanao hakika, Muhamadi wa Ghassani
Ndimi naliyeandika, uloona risalani
Na Harithi wangu kaka, mmoja wetu ubini
Na Baba yetu Ghassani, ni kweli ametutoka

 
Ghassani alotutoka, kwangu mimi kama ami
Zama walizoondoka, wavyele wetu Yamani
‘Kasogea Afirika, pande hizino za pwani

Waligawana watwani, na gele wakageleka

Wengine Pemba ‘kafika, Katanga na Upateni
Wa Pate ndio Muyaka, Al Haji wa Ghassani
Wa Pemba ndiswi hakika, wavyele wangu kirami

Wa Katanga huyu ami, wavyelewe ‘likofika

Vizazi vilozalika, navyo ‘kawa hamkani
Wa Katanga wakatweka, Unguja hapa nyumbani
Wangine kadamirika, hadi Lindi Mrimani
Ila sote tu Ghassani, hilo twajua hakika

Miji yote utofika, hukuno Sawahilini
Ghassani ‘meimarika, vitale vyote vya pwani
Na wengine wazalika, Ulaya na Arabuni
Ndimi mwana wa Ghassani, kijanao ‘noandika

Na salamu nyenginezo, ‘lizotuma karibuni
Kwa tungo niandikazo, na makala za Dirani
Nilizipata ninazo, Mahbubu shukrani
Kwamba wanipa imani, andiko nenende nazo

Ninazo zote ninazo, kila nakala nyumbani
Ingawa sina uwezo, kuzitia kitabuni
Ila lile pendekezo,  ‘meliweka mtimani
Asaa Mola Manani, kunipa lenye mafanzo

*Barua ya tarehe 13 Januari 2008 kwa Sheikh Salim Himidi wa Paris, Ufaransa, baada ya kuniandikia kutaka kujuwa ubini wangu na uhusiano nilionao na Dk. Harith Ghassany na jamaa wengine wa Ghassani.

About Zanzibar Daima 1611 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

2 Comments

 1. Ni fakhari iliyoje, kwanyi mawana Ghassani
  Mulivyo sambaa kote, humuno ulimwenguni
  Madume na matu make, Pemba hata Arabuni
  Lilobaki musimikwe, ufalme wa karini

  Ninaowajuwa miye, hawa Maghassanaini
  Khelefu naye mwenziwe, Ghassani wa Marekani
  Ni viumbe vya pekewe, vilivyoumbwa kwa shani
  Ngojani niwandikie, kwa alau sifataini

  Ghassani wa Marekani, ni Mwandishi mmahiru
  Wa Kwaheri Ukoloni, na bai bai Uhuru
  Kuyaandika ya ndani, kwa kweli ejikusuru
  Kutoa watu vizani, akawawashia nuru

  Na Ghassani wa Pandani, Mfasihi Mshairi
  Saivi yu Jerumani, yuatangaza habari
  Huna vya kumzaini, kwa wake Uzanzibari
  Huyu namwiji kwa ndani, ni wangu wa maduguni..

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.