Basi ni Hapo…

zanzibar

Basi ni hapo ambapo, wenyewe tutaamua
Maamuzi ya iwapo, nani ambaye afaa
Na azuke mtu hapo, kuitanza yetu njia
Wa mamaye ‘tamjua, mkunga ikiwa yupo
Basi ni hapo ambapo….

Basi ni hapo ambapo, kichwani jua na mvua
Majumbani tutokapo, foleni kwenda kukaa
Ni hapo si penginepo, kusuka ama kunyoa
Dhamira yetu na nia, sikuye zisimamapo
Basi ni hapo ambapo….

Basi ni hapo ambapo, la kuwa litapokuwa
Lisijalotokeapo, ndipo litapotokea
Lisiloonekanapo, ndipo litashuhudiwa
Kilele shina ‘kitawa, kisha juu kisijepo
Basi ni hapo ambapo…

Basi ni hapo ambapo, giza tutapoondowa
Ni hapo iangazapo, nuru njema ‘kasambaa
Wengine wasikiapo, wabaki kutushangaa
Yatakuwa! Yatakuwa! Naapa leo kiapo
Naam, basi ni hapo…

Mohammed K Ghassani
1 Juni 2015
Bayreuth – Ujerumani

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.