Wino, Neno na Mfano

Uandikao si wino, bali hili chozi langu
Ninenayo si maneno, bali ni hadithi yangu
Nitoayo si mifano, bali ni ukweli wangu
‘Sisikize minong’ono, sikiza kauli yangu

  • Mohammed Ghassani

Shukurani ‘e Ghassany, twaenzi uwepo wako
Kuandika kwako fani, ‘kutunuku mola wako
Usemalo lina shani, ukweli khulka yako
Akuhifadhi manani, vitimbi adui zako
Tunatoa shukrani, kwayo njema kazi yako

Nami niombe nafasi, nitoe yangu maoni
Wino bila karatasi, sijaona mshindani
Usiwe na wasiwasi, machozi futa usoni!

Kake bora vumilia, jikaze tena kiume
Twajua unaumia , la ukweli tuseme
Makubwa walipitia, maswahaba na mitume
Chozilo n’chozi gani, la furaha la huzuni?

Kake sifanye mzaha, ya kwangu nami sikia
Kichwani mwangu nahaha, chozi nataka lijua
Chozi lako la furaha, utakalo simulia
Chozilo n’chozi gani, la furaha la huzuni?

Kake upo taabani, unatamani kulia
Muungwana le rohoni, kidume chagugumia
Chozi lako la huzuni, wataka tusimulia
Chozilo n’chozi gani, la furaha la huzuni?

Kaka wengekuja tena, kutuleza undani
Vipi unalia sana, huna furaha moyoni
Halafu unajibinya, unakaa kipembeni
Usikae kujibana!hebu rudi ukumbini

Tulisikia sauti, jiranizo tukafika
Ilitupate bahati, tujue yalokufika
Japo tutoe sauti, lakini umetoweka
Sasa jawabu hutupi, kipi unakiogopa?

Mamlaka tupumuwe, unamjua Ghassani?
Yeye ni nguvu ya jiwe, hajibanzi pembezoni
Asema bila kiwewe, hulkae nafsini
Ajiamini mwenyewe, kulia si yake hani
Ghasanni ana wenyewe, twampenda kwa undani

Aliposema ni chozi, hakumaanisha majonzi
Nadhani atupa kozi, kuwa ye si mchokozi
Anenayo kama lozi, hayakupi kikohozi
Amaanisha machozi, Yeye kwetu muokozi
Yeye kwetu mkombozi, kwa raha hata majonzi

Niwapo bado niwapo, Mamlaka Tupumue
Niwapo na bado yapo, ya kunifanya nilie
Na hadithi nitowapo, ni kweli yangu mwenyewe
Na mifano nipigapo, sikiolo itegeye

Wanenapo wamalenga, mie huwa langu jicho
Sijitii ujuaji, kwa kitu n’sichonacho
Kake Mohammed hongera, ela halahala na kijicho

Kaka Ghassani, hakika somo nimelielewa
Najua hukujificha, bali ulipuuzia
Weona kusikitika, haitokusaidia
Sikio ninaliweka, nalitega kusikia

Kama ningee kimyaa, Barafaji nakwambia
Niliiona zahama, swahiba ilomwingia
Ndipo hasimama wima, nawe upate elewa
Najua sote twasoma, kwa gwiji lenye kujua

Si wino uandikao, ila ni yangu machozi
Mistari uonayo, ndiyo hiyo michirizi
Na kila penye kituo, huwa navuta pumzi
Mawio hadi machweo, mambo mashazi mashazi

 

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.