Ulipoanza Maisha

Mulipoanza maisha, si siku mulozaliwa
Ni siku mulofungasha, bibi na bwana mukawa
Mungu ‘kamshuhudisha, kuwa sasa mumekuwa

 • Mohammed Ghassani

Kama hayo ndo maisha, basi mie sitoowa
Kiwa sasa yanachosha, na bado bwana sijawa?
Mzigo huo wa ndowa, kattu sitojibebesha

 • Simon Bin Itegi

Hayano ndiyo maisha, wa Itegi Saimoni
Nawe ungayakanusha, kwa khofu ziso yakini
Ndugu ‘tajihangaisha, uhai uwe ni deni

 • Mohammed Ghassani

Usambe nayakanusha, kwa hofu ziso yakini
Yalivyo hayo maisha, ndu’yangu ni kama zani
Na’ndaa ya uzimani, ndoa sitojibebesha

 • Simon Bin Itegi

Ndoa ina ladha yake, ni vyema ukatambua
Haswa ukipata mke, maisha anoyajua
Uoe uheshimike, ule raha za dunia

 • Ismail Islam

Usinifanye niteke, kwa unavyo zisifia
Naomba nieleweke, s’o kwamba napinga ndoa
Na’mba heri uwe pweke, za kisasa zina doa

 • Simon Bin Itegi

Ndoa ‘sipojibebesha, nduu yangu Saimoni
Hutayajua maisha, asilani abadani
Yako itawa geresha, fensi ya mitaani

Sambi ndoa ni tamasha, furaha tupu ya shani
Ina mangi mahangasha, na dharuba na tufani
Lakini ndiyo maisha, ya mja wa duniani

 • Mohammed Ghassani

Sasa hayo mahangasha, na dhoruba na tufani
Ndio imi yanitisha, yafanya nisitamani
Hayo ya ndoa maisha, yahitaji mwenye moyo

 • Simon Bin Itegi

Yano yakikukhofisha, yapi yasonayo kwani?
Hakika yake maisha, mkufu wa mitihani
Mmoja unapokwisha, mwengine uko njiani

Wapaswa jikurupusha, wa Itegi Saimoni
Nawe uanze maisha, wetwe u mtu watuni
Wakati usijekwisha, nawe kwa moyo unao

 • Mohammed Ghassani

Kasumba mun’zijaza, vichwani zin’wakaa
Jambo linonishangaza, mukataao kuoa
Yakini ukichunguza, mwaendekeza hawaa

Wanawake mun’jaza, kutwa mwawagharamia
Nafusi ‘kiyendekeza, hakika utaumia

 • Ismail Islam

Bure utajidhulumu, ukioa hatokaa
Siku hizi waadhamu, hizi ndoa ni balaa
Ndoa tulozihishimu, hazipo sasa ni baa

Haupo uaminifu, waja leo wa hadaa
Hutopata mtiifu, walo sasa ni vichaa
Heri umche Latifu, us’ongozwe na tamaa

 • Simon Bin Itegi

 

 

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.