Sina la Kujuta

Sikujuta, sijuti, sitajuta
Si jana, si leo, si kesho
Kwa nnalolitafuta
Lingakumbwa na vitisho
‘Tasema
‘Tatenda
‘Tapigana
‘Tachukia

‘Tachukia chuki kubwa
Kubwa, kuu na kali
Jibwa ‘taliita jibwa
Sitaliita tumbili
Ukweli
Dhamiri
Kauli
‘Tasimamia

Tasimamia kwa dhati
Nikiaminicho ndicho
Kwa vyovyote sikiwati
‘Tasimama nacho hicho
Kwa moyo wangu
Roho yangu
Akili yangu
Na hata damu
Na hata uhai
Na maisha yangu

Mohammed K. Ghassani
7 Disemba 2015

Nairobi

About Zanzibar Daima 1696 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply