Mitumwa Itumikayo

Mitumwa itumikayo, utumwa ikaubeba
Na hao waitumayo, kwa kuilipa vibaba
Hima nairudi nao, kwetu kujaa si haba
Kuni inayozibeba, ‘tawachoma wenyiwao

Mitumwa is’ojijuwa, kuwa iyo ni mizoba
Mijitu ‘lotawaliwa, hadi bongo zimeziba
Haiwezi tuondowa, kwenye yetu matilaba
Si mama zao si baba, nchi hii walopawa

Mitumwa ya kifikira, mimama na mijibaba
Haijuwi kilo bora, haina cha tajiriba
Ona yaficha misura, nyuma ya shungi na juba
Ingawa kweli mijuba, ingalikuja shahara

Mitumwa ya kiakili, minjaa isiyoshiba
Haijuwi ta’awili, mila na vyetu vitiba
Siye tuko kwenye kweli, hatuchelei ujuba
Na kwalo hatuna toba, twasimamia kauli

Mohammed K. Ghassani
12 Disemba 2015
Bonn

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.