Leila wa Majinuni

Lau kupenda ni kosa, nimo kwenye wakosao
Kwenye kosa nimenasa, sitanasuka kwa leo
Wala sijali kabisa, hiki kikiwa kituo
Leila wa majinuni, ‘tatua yangu maisha!

Na lau kuna adhabu, wapewayo wapendao
Mimi naistahabu, niadhibiwe kwa hayo
Ni radhi kupata tabu, kutetea wangu moyo
Leila wa majinuni, mahabani nitafia

Lau hupigwa viboko, wale watu wapendao
Nitakwenda huko huko, kwenye hao wapigao
Nambe nipigeni mboko, kwa uzito mutakao
Leila wa majinuni, wala kabisa sijali

Hata iwe ni risasi, polisi wafyatuwayo
Wallahi sina kisisi, nipigwe nanife leo
‘Takufa nikijihisi, ni hai chini ya bao
Leila wa majinuni, hafi huishi daima

Basi naviwe viwavyo, nayasemwe yasemwayo
Vyovyote vitukiavyo, sivunji ninuwiyayo
Kwamba ndivyo wafanyavyo, wale watu wapendao
Miye Leila Majinuni, lawama zenu zikome!!

Mohammed K Ghassani
2000
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1655 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply