Mbona Hulii Wacheka?

Ni kweli au kejeli, shingo upande ‘meweka
Watwambia u dhalili, huku kicheko wacheka
Hivi wewe u mkali, au urongo wasuka?
Ushindi wako wekua, ila wao waufuta

Eti wekuwa tayari, nguo umeshazikata
Ushazifua vizuri, zang’ara zikitakata
Waliutia dosari, mchezo wakaufuta
Wadai wasikitika, mbona hulii wacheka?

Wacheka kwa majigambo, mchezo ‘livyofutika
Wapita wakaza tumbo, na maneno yakutoka
Wasema wenu urimbo, ndege mimi nimeng’oka
Wadai wasikitika, mbona hulii wacheka?

Manenoyo kama Jongo, mwenyewe yanakusuta
Upande ‘ngaweka shingo, ushindi ungaupata
Vipi uitunge singo, haitoki kwakarata
Wadai wasikitika, mbona hulii wacheka?

Amour Hadji
Zanzibar
6 Februari 2016

About Zanzibar Daima 1700 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply