Ingekuwa si unafiki wenu, mungeweza kumkemea Nkurunziza

Wanawezaje kumkemea Pierre Nkurunziza wakati wao wenyewe nchi zao wanayafanya hayo hayo? Jiulize hivi kweli aliyekuwa Mwenyeki wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe angepata wapi ujasiri wa kumkemea Nkurunziza wakati yeye mwenyewe ‘amejimilikisha’ Zimbabwe kuwa ni Rais wa kufa na kupona? Mugabe huyu huyu mwenye ‘darzen’ ya vikwazo vya nchi za Ulaya na Amerika akihusishwa kuikanyaga demokrasia wazi wazi inawezekanaje apate uthubutu wa kumsema Nkurunziza?

Usimshange Nkurunziza wa Burundi pekee jiulize vipi kuhusu Rais Kabila Joseph wa Congo DRC, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda hawa ‘wamejimilikisha’ kutawala na kudhani wengine hawana haki ya kufanya hivyo hata kama idadi kubwa ya wapiga kura inawaunga mkono, Nkurunziza wa Burundi amejiongezea muda wa utawala kinyume na matakwa ya katiba ya watu wa Burundi, hakujali na wala hajali ni madhara kiasi gani yanatokea kutokana na tamaa yake ya kutawala akishirikiana na kikundi kinachomuunga mkono, kumbuka Burundi hata jeshi limemeguka kutokana na maamuzi yake.

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Paul Kagame wa Rwanda akitumia ‘kiini macho’ na ghilba za kiuongozi amefanikiwa katika jaribio la kujiionesha kuwa yeye anakubalika, sasa atakuwa Rais wa Rwanda mpaka 2034 kama si kujimilikisha huku tukuiteje? Rwanda ni moja ya mataifa ya Afrika Mashariki ambayo inatajwa kuwa ni nchi yenye kuzingatia mfumo wa mgawanyo wa jinsi na kufika hamsini kwa hamsini, nchi inayopiga hatua kiuchumi na waliofanikiwa katika utunzaji wa mazingira lakini ni nchi inayotajwa kuwa na ukandamizaji wa kutosha wa uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari vya Rwanda vinapata mbinyo mkali sana huku wanaharakati wakikumbana na mkono wa Serikali pale wanapojaribu kuikosoa Serikali hata kama imekosea, kiufupi kuikosoa Serikali ya Kagame ni dhambi inayostahiki adhabu ya kifo!

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe yeye ndiyo ameshajitangaza kuwa Rais wa kufa na kupona, kwamba ataiongoza Zimbabwe mpaka atakapokufa kwa kile alichokiita eti ‘amechaguliwa’ na Mungu kuiongoza Zimbabwe mpaka atakapokufa, hivi kuna nchi ya kiafrika yenye uthubutu wa kufungua kinywa na kuanza kuwakemea hawa? Ubabe wa Mugabe umepelekea nchi ya Zimbabwe kuwa Taifa masikini kabisa duniani, uchumi wake unaporomoka kila dakika na hali ya maisha ya wazimbabwe inazidi kufifia siku hadi siku.

Rais Joseph Kabila wa Kongo DRC, tayari anajiandaa kugombea muhula wa tatu licha ya katiba ya nchi ambayo ameapa kuilinda ikimkataza kuhudumu kwa awamu zaidi ya mbili, kuna dalili za wazi kwa yaliyotokea na yanayotokea Burundi yanainyemelea Congo DRC, viongozi wa Afrika kimya kama vile hakuna kinachoendelea, wanasubiri damu imwagike ya kutosha waanze unafiki wa kile walichokizoea eti “usuluhishi wa mgogoro”! Ebo! Suluhu ya mgogoro wakati chanzo milshakiona tangu asubuhi na muhusika mnamjua hakuna hatua yeyote mliyochukua kabla mnasuluhisha nini kama si unafiki uliowajaa katika mioyo yenu, tukumbuke Congo DRC ndiyo Taifa lenye rasilimali zenye thamani zaidi duniani lakini je, zimewanufaishaje?

Wapo wengine wenye chembe chembe za ‘ukurunziza’ kama Sudan ya Khartum na kwengineko lakini hawakemewi wala kuchukuliwa hatua yeyote inayostahiki, mataifa ya Ulaya na Marekani yanapaza sauti zao kama kwamba haitoshi wanakwenda mbali zaidi kuweka mbinyo kwa kutuwekea vikwazo vya misaada na ikibidi kuzuia viongozi wa nchi husika kuingia nchi yeyote ya Ulaya na Marekani, rejea Zimbabwe, Tanzania (mradi wa MCC), Kenya, Burundi, Uganda, Sudan na Rwanda, wazungu wanachukuwa hatua pale wanapopaweza, sisi wenyewe tunaona muhali kutoleana uvivu na kuwacha damu ikimwagika utadhani wanaokufa ni mifugo!

Wanazalisha wakimbizi halafu wanataka Umoja wa Mataifa wawahudumie, wanasabisha machafuko halafu wanataka Umoja wa Mataifa uwapelekee majeshi ya kulinda amani, maafa yote haya wanaishia kuitwa katika meza ya mazungumzo eti wanajadili kuhusu suluhu! Suluhu gani wakati wahusika mnawalinda, hamuwakemei, ni rafiki zenu na wakishinda ‘kibabe’ pia mnawapongeza na kuzidi kushirikiana nao, mauaji yanayotokea na wimbi la wakimbizi linalozalishwa huwa mumelala ‘fofofo’!

Unafiki huu ndiyo unaoligharimu Bara hili, hakuna anayeweza kumfunga ‘paka kengele’, ndiyo! Unawezeja kumkemea Nkurunziza uwaache Kabila, Mugabe, Kagame, Omar Al-bashir? Kazi kusubiri mauaji yatokee halafu tujitie unafiki wa kutafuta suluhu kana kwamba mauaji hayo yameshuka yenyewe kutoka Mbinguni kumbe ni mikono ya wang’ang’ania madaraka na vikundi vyao vichache wakiungwa mkono na vyombo vya dola halafu wanakuja na lugha ya suluhu tena wao ndiyo hujifanya mabingwa wa kugawa vyeo, yaani mtu aliyestahiki kwenda jela yeye ndiyo anabembelezwa akubali kugawana madaraka na wenzake, tunayakumbuka yaliyotokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Unafiki wa viongozi wengi wa Afrika (sio wote) ndiyo chanzo cha migogoro tunayoishuhudia katika nchi zetu, ni nchi chache sana Barani Afrika ndiyo zenye mfano wa kuheshimu demokrasia ya vyama vingi, lakini wengi wao ni wasanii, wamekubali ‘shingo upande’ kuingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na naamini wanatamani kuufuta ila nguvu hiyo hawana maana DUNIA ITAWASHANGAA ukizingatia ni nchi tegemezi hazina uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kidiplomasia.

Siku tutakapoacha unafiki na kuusimamia ukweli tutaepusha mengi mabaya katika Bara hili, mauaji, wakimbizi, maradhi, mapigano ya kikabila, kidini na mengine ambayo yanazalishwa na unafiki wa viongozi wa Afrika!

Naomba kuwasilisha!

Ally Mohammed,
Zanzibar,
Tanzania,
Barua-pepe, allymohammed01@gmail.com

About Zanzibar Daima 1696 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply