Wanadhulumu na wanataka washangiliwe

Uchaguzi Zanzibar 2015
HUWAJE jamii inayolazimishwa iukubali uongo au ihalalishe haramu? Imenibidi nijiulize swali hilo na nilitafakari kutokana na ule uitwao “uchaguzi wa marudio” uliofanywa Zanzibar Jumapili iliyopita, uchaguzi ambao umelaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa.
Serikali za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Uhispania, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani zimetoa tamko la pamoja zikisikitika na kuonyesha wasiwasi wao kwamba uchaguzi huo ulifanywa.
Serikali hizo zilimsihi Rais John Magufuli aonyeshe uongozi katika mkwamo huo wa kisiasa wa Zanzibar. Kwa kusema hayo wanaonyesha kwamba hawakuridhika na jibu la Magufuli kwamba hana mamlaka ya kuingilia kati Zanzibar.
Msimamo wa mataifa hayo, pamoja na ule wa Muungano wa Ulaya (EU) unathibitisha yale ambayo sisi tunayoyajuwa na dunia nzima inayoyajuwa kwamba uchaguzi uliofanywa Zanzibar Oktoba 25, 2015 ulikuwa wa haki na usio na dosari za kusababisha ufutwe.
Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Kadhalika, inajulikana kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliufuta uchaguzi huo Oktoba 28 baada ya matokeo yaliyotangazwa hadi hapo kuonyesha kwamba mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye aliyekuwa akielekea kupata ushindi katika mchuano wa urais.

Ukweli huu utabaki katika historia na hautoweza kufutika. Utaendelea kuzungumzwa ndani, na hata nje, ya mipaka ya Tanzania kwa miaka na mikaka.
Kwa hakika, serikali haikuwa na lazima ya kuuendesha uchaguzi wa Machi 20. Viongozi kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) — wa Zanzibar na wa Bara — walikwishasema, si mara moja, si mara mbili, kwamba hawatoitoa serikali ya Zanzibar kwa karatasi. Kwa kusema hayo wakimaanisha kwamba hawatokubali kuitoa serikali hata ikiwa chama chao kitashindwa katika uchaguzi.
Inavyoonyesha ni kwamba wenye msimamo huo ndio wenye nguvu ndani ya CCM. Kwa hivyo, hapakuwa na haja ya kupoteza fedha za umma kuuendesha uchaguzi huo, uchaguzi ambao badala ya kutuliza mambo hatimaye utakuja kuthibitika kuwa ndio chachu ya chachawizo na balaa linalosubiri kuikumba Zanzibar na hata Tanzania, kwa jumla.
Hatua ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, ya kuufuta uchaguzi wa mwaka jana ni kichekesho kilichoiaibisha Tanzania. Hali kadhalika, uchaguzi wa Machi 20 nao ulikuwa uchaguzi wa kichekesho uliofanywa katika mazingira ya kuaibisha.
Hamna namna ya kuuelezea uchaguzi huo isipokuwa kwamba ulikuwa “uchaguzi wa uhange”. Nilipokuwa nikiyafuatilizia yaliyojiri kuhusu uchaguzi huo mara nyingine nikijihisi kama nikishuhudia tamthiliya ya vikaragosi au mchezo wa kile kipanya “Micky Mouse” na wenzake.
Yaliyojiri hayasemeki. Vilikuwa vichekesho juu ya vichekesho. Bahati mbaya kwa taifa kwamba vilikuwa vichekesho vya kuaibisha ambavyo huenda baada vikaligharimu taifa kwa kiwango tusichokifiria. Bahati mbaya kwa wapinzani wa Kizanzibari kwamba vichekesho hivyo vikiandamana na vitisho na utumizi wa mabavu.
Watu watakumbuka vifaru vya kijeshi vilivyokuwa na silaha nzito pamoja na wanajeshi waliokuwa mitaani wakibeba silaha. Kukaribia Machi 20 viongozi kadhaa wa CUF waliwekwa ndani.
Machi 18 tulipata taarifa kwamba Salma Said, mwandishi wa muda mrefu mwenye kuheshimika kwa ukakamavu wake wa kusaka undani wa habari, alitekwa nyara na watu wasiojulikana nje ya uwanja wa ndege wa Dar es Salaam katika mazingira yenye kutatanisha.
Alipoachiwa Machi 20 Salma, ambaye ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi na ripota wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani Deutsche Welle (DW), alidai kwamba waliomteka nyara walimpiga mateke na vibao. Ninapoyaandika haya hatujayapata bado maelezo kamili ya kadhia hii.
Siku ya uchaguzi wenyewe ilikuwa ya aina yake. Watu wengi hawakwenda kupiga kura wakifuata agizo la CUF na vyama vingine vilivyoususia uchaguzi huo. Hata hivyo, juu ya ususiaji huo majina ya waliogombea uchaguzi mwaka jana kwa niaba ya CUF na wa vyama vingine vilivyosusia uchaguzi wa Machi 20 hayakuondoshwa kwenye karatasi za kupiga kura.
Vyombo vya habari vya nje na ndani ya nchi vilionesha vituo vya kupiga kura vikiwa na watu wachache na hata vingine vikiwa vitupu huku wasimamizi wa vituo wakiwa wanasinzia. Lakini mashirika ya utangazaji ya Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) na Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC) yaliripoti kwamba “watu wengi” walikwenda kupiga kura. Hayo si ya ajabu kwa vile mashirika hayo mawili ya TBC na ZBC yako chini ya udhibiti wa serikali.
Haikuwa ajabu pia kwamba wakati kituo cha ITV kilipokuwa kikionesha jinsi vituo vya kupiga kura Zanzibar vilivyokuwa vitupu ghafla umeme ulikatika katika sehemu kubwa ya nchi.
Yote hayo ni katika majaribio ya kuufuta ukweli na kuusaliza uongo. Huo uongo uliosalia ndio utaokuja kuwa ukweli. Baada ya muda huo “ukweli” mpya, ukweli-mamboleo utapambwapambwa na kutiwa nakshi ili uzidi kuaminika kuwa ndio ukweli halisi.
Huo ndio utamaduni wa uongo ambao watawala wetu wameuzoea. Tuwaamini vipi watawala kama hao wasioweza kusema kweli au chama chao kinachoupinda ukweli? Ni taabu kuwa na imani nao, taabu kuamini kwamba wanaweza kuongoza kwa uadilifu. Na Magufuli alipokuwa akiomba kura akisisitiza kuwa yeye ni muadilifu.
Kwa kiwango kikubwa, hadi sasa hali ya mambo visiwani Zanzibar ni tulivu licha ya kuwepo wasiwasi na wahaka. Wa kupongezwa kwa utulivu huu ni Maalim Seif na viongozi wenzake wa CUF, hususan naibu katibu mkuu Nassor Ahmed Mazrui na Ismail Jussa. Wote hao, katika nyakati tofauti, wamekuwa wakiwahimiza wafuasi wao wawe watulivu na wasikubali kuchokozeka. Hawa ni viongozi ambao kwa matamshi yao, na vitendo vyao, wanaonyesha kwamba ni watu wasiopenda na wasiotaka damu imwaike.
Watawala wetu, kwa upande wao, wanasema wamebadilika na wanafuata demokrasia lakini vitendo vya kijahili vinavyofanywa na vyombo vya dolavinathibitisha ile methali au usemi wa kwamba kuzunguka mbuyu si dawa ya shetani. Wayafanyayo ni yayo kwa jayo — ujahili, ukaidi, ubaguzina ugandamizi. Tunawashuhudia wakiwapokonya raia haki zao, vyombo vya dola vikiwapiga watu na halafu watawala wakiwataka watu haohao wawapigie makofi.
Ugandamizi huu umefanyika wakati Dk. Magufuli akionyesha shauku ya kutawala kiaskari, hata uteuzi wake wa hivi karibuni umejaa wanajeshi wastaafu.
Wapenda haki na wenye kuitaka nchi yetu istawi hawawezi kuziachia siasa zetu zizidi kuchacha na kuoza wakati dunia ikiwa inasonga mbele.
Juu ya hayo, haimkiniki kwamba hali ya mambo ya Zanzibar itaendelea kuselelea vivi hivi. Hakuna popote duniani tuliposhuhudia udhalimu ukidumu au madhalimu wakitawala kwa raha au wakawa na mwisho mwema.
Juzi tu tumesikia yaliyomkuta makamu wa Rais wa Congo Jean-Pierre Bemba aliyepatikana na hatia ya makosa ya uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) huko Hague. Bemba alishtakiwa kwa kosa la kushindwa kulidhibiti kundi la wapiganaji lisiwaue watu, lisiwabake wanawake na wasichana huko kwao Congo.
Siku chache kabla ya hapo ilitangazwa mjini Abidjan kwamba Simone Gbagbo, mke wa aliyekuwa Rais wa Cote d’Ivoire Laurent Gbagbo, atapandishwa kizimbani Aprili 25 akishtakiwa kwa makosa ya jinai dhidi ya wanadamu. Kwa hivi sasa bibi huyo mwenye umaarufu wa “Bibi wa Chuma” yuko gerezani baada ya kuhukumiwa mwaka jana kifungo cha miaka 20 kwa kushiriki katika ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2010 ambapo mumewe alishindwa.
Wa huku kwetu wenye kuyadhibiti makundi kama ya “mazombi”, “janjawid” au “ubaya ubaya” wasidhanie kwamba wanyonge waliowadhulumu watayasahau mateso yao na kwamba wataishi maisha bila ya kuwajibika. Inafaa wakumbuke kwamba fimbo ya mnyonge mlifi Mungu na fimbo ya Mungu haina mlio.
Kwa yanayotokea ni wazi kwamba ingawa watawala wetu hawaziogopi sheria wala Katiba lakini bado wanayaogopa mawazo huru ya wananchi. Woga huo ndio wenye kuwafanya waiendeshe nchi kwa mabavu na kuifanya Zanzibar ionekana kuwa na ishara kwamba inaanza kugeuka na kuwa dola ya kipolisi. Kama kweli dhamiri ni dira basi dhamiri ya watu hawa itatufikisha pabaya.
Miongoni mwa dalili za nchi kuwa dola ya kipolisi ni kunyimwa wananchi haki ya kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya woga, kutumiwa vyombo vya dola kuwatisha au kuwatia hofu wananchi na kuwakamata kiholela wakosoaji wa serikali au wa chama kinachotawala.
Mambo kama hayo ndiyo yanayowafanya wanaopigania haki, hasa vijana, wawe na misimamo mikali na halafu wasingiziwe kuwa ni magaidi.

 

Chanzo: Raia Mwema, 23 Machi 2016

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.