Baada ya kushinda kesi ya uchochezi dhidi yake, sasa kijana wa Kitanzania aitaka serikali imuombe radhi

Kijana wa Kitanzania, Mpaluka Said Nyagali maarufu kwenye mitandao ya kijamii kama Mdude Nyagali, ameshinda kesi ya uchochezi dhidi yake na sasa anaitaka serikali kupitia vyombo vyake vilivyoshiriki kwenye mateso makubwa aliyopitia ndani ya kipindi cha kukamatwa na kushikiliwa na vyombo hivyo, wamuombe radhi. Soma barua yake kwa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora ya Tanzania hapa.

MDUDE M.S.NYAGALI
P.O.BOX ……………
MBOZI-SONGWE
EMAIL (mdudenyagali@gmail.com)
SIMU;;+255766073888

3 MAY 2017

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
P.O.Box 2643
DAR ES SALAAM-TANZANIA
SIMU;; +255 22 2135747/8
FAX;;   +255 22 2111533 | 2111281
IMEIL;; chragg@chragg.go.tz |  mary.massay@chragg.go.tz

SALAMU

YAH: MALALAMIKO YANGU KUHUSU UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU WAKATI NAKAMATWA NA KUSHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA UCHOCHEZI
Natanguliza salamu zangu za dhati kwa watumishi wote wa Commission for Human Rights and Good Governance (CHRAGG), Tume iliyojikita kutetea haki za binadamu na Utawala bora. Kazi hii ni ngumu Sana na ni kazi ya wito inahitaji uzalendo wa hali ya juu na ndio maana siku zote nawaombea kwa MUNGU awaongoze maana mnapata changamoto nyingi katika kazi hii

 1. UTAMBULISHO

Naitwa MPALUKA SAID NYAGALI ambaye pia nimekuwa nikijulikana kwa jina la  MDUDE NYAGALI umri wangu ni miaka 29 ni Mtanzania ninayeishi mji wa Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe.

 1. LENGO LA BARUA HII

Lengo la barua hii ni kuleta malalamiko yangu kwenu  TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA chini ya ibara ya 130  ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Mimi ni muhanga nimedhalilishwa, nimepigwa, nimeteswa na Jeshi le Polisi kinyume na sheria, jeshi la Polisi Tanzania lilinihukumu kwa kunipiga ,kunidhihaki, kunidhalilisha na kunitesa kabla ya mahakama kutoa hukumu hukumu kinyume kabisa na katiba ya jamuhuri ya muungano wa tanzania ibara ya 12(2),ibara ya 13(1),ibara ya 13(6)(b),ibara ya 13(6)(c) na ibara ya 13(6)(e). mwisho mahakama na ikaniachia kwa kuto nikuta na Hatia.

 1. NILIVYOKAMATWA NA JESHI LA POLISI
 2. Mnamo tarehe 26 Agosti 2016 asubuhi ya saa 2 hivi siku ya ijumaa nikiwa nyumbani kwangu nimelala, Niligongewa mlango niliamka haraka huku nikiwa nimejifunika shuka na kwenda kufungua mlango. Nilipofungua tu mlango waliingia askari bila hodi bila utaratibu wowote,Askari mwenye cheo cha koplo kwa jina NISILE MWAITENDA alinishika kisha ku nivua shuka nikabaki mtupu yaani uchi wa mnyama kisha akanifunga pingu nilipohoji nimekosa nini alinipiga mateke tumboni huku akiagiza askari wenzake waseach ndani kwangu kila eneo.

 

 1. Hawakuniambia kosa langu kama sheria inavyowataka. Askari hao waliseach ndani kwangu bila kuwa na kibali chochote kama sheria inavyotaka, Wakanifungua pingu kisha wakaniambia nivae nguo .Nilipovaa nguo walinifunga tena pingu kisha wakanichukua mimi,walichukua simu zangu mbili pamoja na compyuta mpakato bila kufuata utaratibu wala kulikuwa hakuna  cha hati ya Ukaguzi  wala shahidi yoyote aliyeshuhudia kuchukuliwa vitu vyangu kama sheria inavyotaka.Waliondoka na mimi pamoja na vitu vyangu mpaka kituo kikuu cha polisi cha Polisi vwawa.

 

 

 1. BAADA YA KUFIKISHWA KITUONI
 2. Baada ya askari hao kunifikisha kituoni hapo walinipeleka moja kwa moja ofisini kwa RPC wa mkoa wa Songwe ambaye kwa bahati mbaya simkumbuki jina, RPC huyo alinipokea kwa lugha za matusi na kejeli moja ya maneno ninayokumbuka RPC huyo alisema nanukuu (wewe ndio mbwa unayeitwa mdude?umerudi Lini kutoka Malawi?Nina taarifa kuwa serikali iliyopita umeishika sana matako.

 

 1. Hii serikali ni nyingine na haishikwi matako.Mimi ndio mwanaume mkoa huu halafu wewe,Mbowe na Lowasa ni wanawake naweza kuwashika matako tu. Una bahati tumekukamata asubuhi watu wanaona, ila ungekamatwa usiku watu wasione tungekupoteza usingekuja kuonekana milele mbwa we mtoe ofisi kwangu huyu najisikia kichefuchefu) mwisho wa kunukuu. Na nikatolewa ofisi kwake.

 

 

 1. KUPIGWA ,KUTESWA NA JESHI LA POLISI TANZANIA
 2. Baada ya kutolewa ofisini kwa RPC nyuma ya kituo hicho cha polisi nilianza kupigwa hovyo na kila askari anayeniona nikiwa nimefungwa pingu mikononi ,Na baada Koplo nisile Mwaitenda wakituo cha Polisi Vwawa aliwaagiza askari wenzake pale nje kuwa niingizwe kwenye chumba cha mateso kiitwacho GUANTANAMO, chumba hicho kipo kituo kikuu cha vwawa ni moja ya Nyumba ya Polisi zilizopo hapo VWAWA .

 

 1. Nilifungwa miguu na mikono na kuning’inizwa juu kama mfuko wa kiroba unaopimwa mizani kisha kuniweka jiwe kubwa kifuani na wakaanza kunipiga kwa kuwekeana zamu,nilipokuwa nalia naambiwa ninyamaze nikiuliza nimekosa nini walinijibu kuwa makosa yako utaenda kuyajua Dar es Salaam, nilipigwa sehemu za matakoni, nyayo na magoti kwa rungu kubwa lililochongwa kienyeji almaarufu kama fatuma.

 

 1. Askari hao ambao ninawafahamu kwa sura waliendelea kunipiga huku wengine wakinipiga picha kwa simu na  nikiwa nimefungwa na kuning’inizwa juu miguu na mikono na Koplo NISILE MWAITENDA ndiye aliyekuwa akinipiga picha za mnato na video huku akiwaambia askari kibao wanataka niwarushie kwenye mgroup ya watsapp waone ninavyoteswa maana huwa najiona sana.Nilipigwa mpaka nikazirahi na nilipozinduka nilivutwa kama mzoga mpaka ofisini kwa RCO ambaye ninamjua kwa jina moja tu la Mtatiro  ambaye kwa sasa RCO huyo kahamishiwa Mpanda, RCO huyo aliniambia ili niendelee kuwa salama basi napaswa kuachana na siasa za upinzani,Lakini nikiendelea na siasa za upinzani basi nahatalisha maisha yangu,Baada ya kuambiwa maneno hayo nilitolewa ofisini kwa RCO na kwasababu nilikuwa siwezi kutembea kutokana na Kipigo  nikabuluzwa na Askari Polisi  mpaka mahabusu.

 

 

 

 

 

 1. KUWAZUIA NDUGU NA JAMAA WALIOKUJA KUNIONA KITUONI HAPO

Baada ya kuwekwa mahabusu Askari Polisi wa Kituo cha Vwawa  walizuia na kuwafukuza ndugu na jamaa waliokuja kuniona kituoni hapo au kuniletea chakula,Askari waliwatishia ndugu na jamaa kuwa wakiendelea kuja kuniona basi nao watakamtwa na kuwekwa mahabusu na kupewa kesi kama yangu.

 1. KUKATAA KUNIPA HAKI ZA MATIBABU
 2. Pamoja na kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa nimenifanyia unyama na ukatili wa hali ya juu kipigo na mateso lakini walikataa kunipa haki ya kutibiwa kwa kuwa nilikuwa na Maumivu makali na siwezi kutembea, Niliomba msaada wa kutibiwa bila mafanikio mpaka alipokuja wakili ISACK CHINGILILE (0754927822) ambaye aliumbwa na Wakili aliyeombwa anisaidie na Rafiki yangu Fanuel Mkisi Ndugu Boniface Mwabukusi Kwani kwa wakati huo yeye alikuwa Kigoma Kikazi.

 

 1. Wakili Huyu alishuhudia hali ya dhiki na Maumivu niliyokuwa nayo na akatishia kuchukua hatua za kisheria nisipopatiwa Matibabu kutokana na Maumivu niliyokuwa nayo yaliyosababishwa na Askari Polisi wa Kituo cha Vwawa kunipiga, kunitesa na kunisababishia Maumivu mkali, Wakili alisema kitendo mlichomfanyia mteja wangu MDUDE NYAGALI ni kinyume na sheria na ni kinyume na haki za binadamu, Wakili alitaka kabla ya mimi kutoa maelezo nipewe haki ya kutibiwa ndio nitoe maelezo. Walimuahidi wakili huyo kuwa watafanya hivyo lakini matokeo yake alipotoka walinibeba kimyakimya Usiku bila mtu yoyote kujua na kunisafirisha hadi Mbeya usiku wa saa 3 tarehe 27 Agost 2016.
 2. KUSAFIRISHWA KIKATILI MIMI PAMOJA NA WATUHUMIWA WENZANGU AMBAO NI ARISTOTLE MGASI NA HOSEA MBUBA KUTOKA VWAWA KWENDA DAR ES SALAAM.
 3. Moja ya kitu ambacho nikikumbuka huwa machozi hunitoka basi ni namna ya tulivyosafirishwa na Jeshi la Polisi kutoka VWAWA mpaka Dar es salaam usiku wa tarehe 27 agost 2016.Tulifungiwa mikono yetu yote kwenye bomba za gari ya Polisi iliyokuwa inatusafirisha. Mpaka sasa mikono yangu ina makovu ambayo pingu zilikuwa zinanikata pale gari lilipokuwa linaruka matuta ya barabarani au mashimo ya barabarani.

 

 1. Lakini pia hatukufungwa mikono tu bali tulifungwa miguu na tulipoomba kujisaidia au kuchimba dawa walikataa na walituambia kuwa tujikojolee au tujinyee muda wa kusimama hakuna. Tulisafirishwa kikatili na mateso makubwa mpaka tulipofikishwa kituo cha Polisi OSTERBAY kilichopo Mkoa wa Dar es Salaam kesho yake 28 Agost 2016 na kuwekwa mahabusu.

 

 

 1. KUCHUKULIWA NA KWENDA KUTESWA TENA NA WATESAJI AMBAO HAWAKUJULIKANA.
 2. Mnamo tarehe 29 agost 2016 siku moja baada ya kufikishwa kituo cha osterbay jumatatu mida ya mchana nilitolewa mahabusu nikakabidhiwa vitu vyangu vyote nilivyokuwa navyo nikakabidhiwa kwa watu ambao sikuwajua na nilipouliza nyie ni akina nani na wapi napelekwa hawakunijibu, ILa walikuwa watu wenye vifua vikubwa mabaunsa walinibeba na kuniingiza kwenye gari ambayo siyo ya serikali kwani gari hiyo ilikuwa na namba za usajiri za kiraia binafsi ila gari ilikuwa Land cruiser hardtop. Na nilipoingizwa ndani ya gari hiyo nilifungwa kitambaa usoni na gari iliondoka ila baada ya muda hivi tukafika sehemu kwenye nyumba moja hivi. Ninachokikumbuka kwenye nyumba hiyo ni kwamba nje palikuwa na bendera ya taifa na baadhi ya watu wenye bunduki waliokuwa wakilandalanda ndani ya ugha  wa nyumba hiyo.

 

 1. Niliingizwa kwenye nyumba hiyo ndani ambapo niliwakuta watu wasiopungua 10 wakiwemo wanawake watatu nilivuliwa nguo zote na watu hao moja ya wale wanawake akawa anazishika sehemu zangu za siri na kuzivuta kwa nguvu huku wengine wakicheka na kufurahi. Baunsa mmoja aliamuliwa na mkubwa wao mmoja anze kunipiga, Baunsa huyo alinipiga bila kujali kuwa miguu yangu imevimba kutokana na kupigwa na askari polisi walionikamata,Pamoja na kuomba wanihurumie kutokana na maumivu niliyonayo walikataa na kuniendelea kunipiga na kunifinya na vyuma baadhi ya sehemu zangu za mwili na kunilazimisha kulamba uchafu na damu uliokuwa ukichuruzika  kwenye tiles kutoka kwenye vidonda na michubuko iliyosababishwa na Vipigo na Mateso .Baada ya kipigo na mateso hayo walianza kunihoji yafuatayo
 2. Kwa nini naikosoa serikali ya mheshimiwa rais kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Walinihoji makala kadhaa nilizowahi kuandika kwenye mitandao wa facebook.
 3. Niwaambie Maandalizi na mipango ya maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika September mosi 2016 na chama cha siasa cha CHADEMA yaliyopewa jina la UKUTA.
 • Watesaji hao huku wakinitesa na kunidhalilisha nikiwa uchi kama nilivyozaliwa na Waliniambia kwamba wao ndiyo Serikali na wanaweza kumfanya mtu yeyote kitu chochote na Hakuna mtu wa Kuwazuia kufanya kile watakacho.
 1. Baada ya mahojiano hayo nilirudishwa osterbay na kunikabidhi tena kwa askari hapo osterbay nikawekwa mahabusu.
 2. KUPELEKWA HOSPITALINI:
 3. Baada ya baadhi ya ndugu,rafiki na jamaa kujua kuwa nashikiliwa kituo cha osterbay walifika kuniona na walipoona hali yangu ya afya walipiga kelele kwenye vyombo vya habari na social media nashukuru kelele zao zilisaidia kwani kati ya tarehe 30 na 31 agost nilipelekwa hospital ya mwananyamala,niliandikishwa kutokana na hali niliyokuwa nayo doctor akashauri nifanyiwe X-RAY na nilipofanyiwa X-RAY doctor alivyoniita nichukue majibu polisi walikataa mimi nilibaki nje nikiwa chini ya ulinzi halafu akaenda askari mmoja aliyechukua majibu ya X-RAY yangu pamoja na kivuri cha x-ray hiyo kisha akaenda dirishani kunichukulia dawa na nikarudishwa osterbay mahabusu pamoja na kwamba doctor alishauri nilazwe,Askari hao walimuambia doctor kuwa mimi nitakuwa natibiwa na madaktari ambao ni maaskari palepale ostarbay ambao walikuwa wanakuja kila siku asubuhi na jioni kunifanyia matibabu.Mpaka siku narudishwa mkoani Songwe polisi osterbay walikataa kabisa kunipa vielelezo vyangu vya hospitalini ikiwemo kivuri cha X-RAY na daftari lililokuwa na orodha za dawa mbalimbali HIVYO NAOMBA Tume yako Iamuru kwamba nipewe Taarifa Hizo
 4. KUKAA MUDA MREFU MAHABUSU BILA KUPELEKWA MAHAKAMANI

Pamoja na hali niliyokuwa nayo jeshi la polisi Tanzania halikujali waliendelea kunishikilia kinyume na sheria kwa muda wa siku 17 mpaka alipokuja wakili msomi TUNDU LISSU akanichukua maelezo na kulitishia jeshi la polisi kuliburuza mahakama kuu ndani ya siku 4 kwa hati ya dharula kwa kosa la kunishikilia kinyume na sheria ndio mimi na wenzangu tukasafilishwa tena kurudishwa vwawa mkoani songwe kisha kufikishwa mahakamani.

 1. MASHTAKA NILIYOSOMEWA MAHAKAMANI
 2. Kwakuwa walijua wamenikamata Kwa chuki na hawana shtaka lolote dhidi yangu Nilipofikishwa Mahakamani nilisomewa mashtaka kuwa mnamo tarehe 24 agost 2016 niliandika maneno ya kichochezi katika acaunt yangu ya facebook yenye jina la MDUDE CHADEMA NYAGALI kuwa (NIPO KALONGA MALAWI HUKO NIMEAMUA KUJA ILI NIMWONYESHE MAGUFULI KUWA KAMA NIMEVUKA HAYA MAJI HAKUNA ASKARI WA KUZUIA UKUTA SEPTEMBER MOSI JIANDAENI LA POLISI UCHWARA)
 3. Kesi yangu ilikuwa inasimamiwa na wakili wangu msomi BONIFACE.A.MWABUKUSI (0765742595) na hukumu ya kesi hiyo ya uchochezi ilikuwa 18 april 2017 katika mahakama ya wilaya ya mbozi ambapo mahakama iliniachia huru mimi na wenzangu baada ya mahakama kutotukuta na hatia.
 4. OMBI LANGU KWA TUME HII NI KWAMBA:
 5. Tume yako Ipokee Malalamiko yangu,Ifanyie uchunguzi ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vikundi visivyoeleweka vilivyo nje ya Mfumo wa Jeshi hili Kwa siri.
 6. Tume yako iingilie Kati na kuiamuru Serikali kufunga kabisa au kukomesha vikosi vya mateso kwa Raia ambavyo vinafanya kazi kwa Usiri na ushirikiano Mkubwa na Kituo cha Polisi cha Osterbay .

 

 1. Kitendo cha kunipiga picha za mnato na video wakati nateswa kwenye chumba cha mateso cha GUANTANAMOkilichopo kituo cha polisi vwawa kilichofanywa na askari mwenye cheo cha COPLO aitwaye NISILE MWAITENDA kisha kupost kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia namba yake ya watsapp ya 0755849140 ni kinyume na sheria ya mtandao (cyber crime) ya 2015) na baadhi ya picha alizotupiga tuliziwasilisha mahakamani kama kielelezo upande wa utetezi,Hivyo naiomba tume hii kulipokea lalamiko hili,kujiridhisha kisha kuchukua hatua kama katiba inavyowaongoza ibara ya 30(c)

 

 

 1. Naiomba tume hii imuhoji mkuu wa kituo cha osterbay kwa vyovyote anawajua wale watesaji walionichukua na kwenda kunitesa zaidi ya masaa 6 kisha kunirudisha kituoni hapo,Lakini pia najaribu kuunganisha matukio mwanamuziki aitwaye ROMA MKATOLIKI alipotekwa na kupotea alionekana kwa mara ya kwanza kituo cha osterbay.Kitu hiki kinanisukuma kuwa lazima mkuu huyo wa kituo anawajua watesaji hivyo ni muhimu kumuhoji kwa kuwa mna mamlaka hayo kikatiba.

 

 1. Naiomba tume hii ambayo imepewa mamlaka ya kumuhoji mtu yoyote ndani ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania kasoro rais ,Tume hii imuhoji RPC wa songwe aliyesema kuwa ningekamatwa usiku watu wasione wangenipoteza nisionekane tena,Kauli hii inanitia shaka ususani kipindi hiki ambacho watanzania wenzetu wamekuwa wakipotea,kutekwa na kukutwa wameuwawa ,Huenda RPC huyu ni miongoni mwa watekaji kutokana na kauli yake hivyo anaweza kujua vizuri watanzania wenzetu waliopotea au kutekwa walipo, akihojiwa vizuri anaweza pia kutuonyesha au akatusaidia watanzania kuwapata watanzania wenzetu waliopotea akiwamo ben saa nane.

 

 1. Naiomba Tume hii Ilikemee Jeshi la Polisi na Kulitaka kuacha maramoja kutumika kisiasa kuvunja haki za binadamu kwa kuwaweka watu kizuizini bila kuwapeleka mahakamani, kuwatesa, kuwapiga na kuwadhalilisha. Vyombo vya dola vifanye kazi kitaaluma na sio kisiasa.

 

 1. Naiomba tume iwaonye wanasiasa wenye mamlaka na vyombo vya dola kutumia vyombo vya dola, kutesa, kuteka na kuwadhalilisha wapinzani wao kisiasa, vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria.Na sisi watanzania tumekuwa wamoja tangu uhuru hivyo wanasiasa wenye mamlaka na vyombo vya dola wasitugawe kwa maslahi yao binafsi kwa kutumia vyombo vya dola.

 

 1. Tume yako iliagize Jeshi la Polisi Kuniomba Radhi kwa Maandishi na Likiri Bayana kwamba Hiki walichonitendea siyo haki na zaidi kwamba hawata ninyanyasa tena kwasababu ya Misimamo yangu ya Kisiasa na wawajibike kwa Maumivu ya Kimwili,Kisaikolojia niliyoyapata.

Mwisho kabisa natoa shukrani kwa kupokea malalamiko yangu naamini mtayafanyia kazi na kuchukua hatua inapobidi

ASANTE

MDUDE NYAGALI

………………………………

NAKALA   ; KITUO CHA SHERIA ZA HAKI ZA BINADAMU (LHRC)

DAR ES SALAAM.
;TANGANYIKA LAW SOCIETY (TLS)

DAR ES SALAAM

About Zanzibar Daima 1610 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.