HABARI

Barua ya Marehemu Malima yafichuwa aliyotendewa na JK

Visa na vitimbi vilivyozuka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 vinashabihiana sana na kile kilichotokea miaka 20 nyuma wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi wa kwanza tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafichuwa barua iliyoandikwa na Marehemu Profesa Kighoma Ali Malima wakati huo.

Miongoni mwa mambo yanayoshabihiana mno ni ushiriki wa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye mwaka 1995 alikuwa mmoja wa waliowania tiketi ya CCM kugombea urais wa nchi, na ambaye pia alikuwa mrithi wa Profesa Malima kwenye nafasi ya uwaziri wa fedha.

Profesa Malima alijivua nyadhifa zake zote kwenye baraza la mawaziri la Rais Ali Hassan Mwinyi, kwa kile anachokieleza kwenye barua yake ya kuomba kujiuzulu kuwa ni kukiukwa kwa maadili ya utawala na misingi ya uwajibikaji wa pamoja kulikofanywa na Kikwete.

Inafahamika kuwa Profesa Malima, aliyekuja kufariki dunia jijini London, Uingereza, miezi michache baada ya kujiondoa serikalini na kutangaza kuwania urais kupitia chama kipya cha kisiasa, aliwahi kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM na nje yake, kutokana na kujipambanua kwake kama msomi na msemaji wa ngome kuu ya CCM – jamii ya Kiislamu.

Mbele ya Profesa Malima, kwa hivyo, wagombea akina Kikwete wasingelikuwa na pa kupenyea, lakini kile kinachoonekana kama hujuma dhidi yake iliyoongozwa na wenziwe, ilimporomoa na mapema na hivyo kuiporomosha ndoto yake ya kuwa rais wa Tanzania kupitia CCM.

Ingawa wengine wanasema kuwa lawama za kuporomoka kwa Profesa Malima zinamuangukia pia Rais Mwinyi, mzawa mwenziwe wa Mkuranga, kutokana na udhaifu mkubwa aliouonesha kiuongozi, lakini njama za kundi la vijana wa wakati huo zina nafasi kubwa sana.

Historia ilijirejea tena kwa Kikwete, miaka 20 baadaye, sasa akiwa rais wa nchi, amiri jeshi mkuu na mwenyekiti wa chama tawala, pale aliposimamia mkutano uliowang’oa wagombea kadhaa mashuhuri ndani ya CCM, akiwemo aliyewahi kuwa swahibu wake wa chanda na pete, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.