Ishangia Ramadhani

Ishangia Ramadhani, nianze fanya hashuo
Nijiweke kiblani, hijifanya mwanachuo
Ilhali ni shetani, nawavua watu nguo

Ikingia Ramadhani, mimi hujifanya mwema
Nikalisha majirani, wanyonge na mayatima
Japokuwa maluuni, hukaa hashika tama

Hujifanya Muungwana, wachafu nikawabeza
Haacha mambo ya lana, hakaa nikijiliza
Himuomba Maulana, anitoe kwenye giza

Hujileta redioni, nikitoa mawaidha
Hisema huko peponi, kuna mengi yenye ladha
Wakati kwangu moyoni, Ramadhani kubwa adha

Kuna siku hujitowa, nende kuwaona watu
Na vitende nikagawa, wanione nami mtu
Japo nishawapotowa, utu wao sasa butu

Nikiipata nafasi, ya kusema mitaani
Hukumbatia upesi, japo sina jambo geni
Hazungumza kifusi, na mambo yaso thamani

Mimi huwa ninafunga, kwa kuwa nionekane
Kwa kuwa nisipofunga, wataniona  mwengine
Kisha wanipige panga, wanizike Meli Nne

Mussa Shehe
27 Mei 2017
Zanzibar

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.