Ningekuwa Magufuli…

Najuwa kuwa kuna wakati Rais John Magufuli alitamani lau angelikuwa mkuu wa polisi ili “alale nao mbele kwa mbele” wale anaowaona kuwa wanaleta mchezo na dola. Inaonekana pia amiri jeshi mkuu wetu huyu hutamani lau angelikuwa mkuu wa bandari, mkuu wa mamlaka ya kodi, mkuu wa ujenzi wa barabara na ukuu wa mwengine mwingi!

Alimradi kila anapoamini kuwa pameoza – na lazima tukiri kuwa mwahala humo ni mwingi sana, basi Rais Magufuli hutamani lau yeye angelikuwa ndiye mwenye dhamana ya hilo eneo, husemi ila kuwa mkuu wa eneo husika kunakufanya peke yako kupaletea ufanisi mahala penyewe, hata kama mifumo ya kisheria na kimazowea inasema kinyume chake. Naogopa bwana huyu asije siku moja akaamka na kutamani kuwa mkuu wa nyumba zetu tu, maana nazo pia zina uozo mwingi!

Kwa vile mwenyewe anakiri kuwa hakuwa amejipanga kuwa mkuu wa dola iitwayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na, hivyo, hata hakuwazia kuwa mkuu wa chama chake mwenyewe kilichoitawala Jamhuri hiyo tangu uhuru (kikianzia kwa TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar), basi ndio maana hadi leo hajajuwa kuwa kwake mkuu wa ‘taasisi’ hizo mbili, tayari kulishampa ukuu wa mwengine mote humo amutamanimo.

Kama alivyowahi kusema Mwalimu Julius Nyerere “katiba kama ilivyo inampa rais sifa za mungu-mtu” na, kwa hivyo, tayari Rais Magufuli ni mkuu wa wakuu wote wanaohudumu chini yake, wengi wao – kama si wote – wakiwa wateule wake mwenyewe; na wala hakuna mwenye mamlaka ya kumuhoji juu ya utekelezaji wa ukuu wake huo!

Na kama hilo halitoshi, yeye mwenyewe pia ameshawahi kuwa mkuu wa mwahala mwengine ambamo mulivurunda na uvurundaji wake huo ukaitia hasara nchi mithali ya vile ambavyo uvurundaji wa wakuu wengine walio chini ya ukuu wake yeye, unavyotia hasara sasa.

Kwa namna yoyote ile, Rais Magufuli ni sehemu ya mduara wa papo kwa papo ulioitawala Tanzania kwa zaidi ya nusu karne sasa, hata kama anataka kujipambanuwa kama vile yeye si mmoja wao.

Sisemi kuwa vita vyake dhidi ya ukosefu wa uwajibikaji, ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi ya anasa ya viongozi wa umma, na uozo mwengine mwingi ambao umekuwa visawe vya Utanzania havina maana kwa kuwa tu yeye ametokana na mfumo uliouumba uoza huo.

Hapana! Hata Mtume Musa (A.S) alilelewa kwenye nyumba ya Firauni, lakini akachaguliwa na Mungu kuwakomboa Wana wa Israeli. Mtume Muhammad (S.A.W) alizaliwa na kukulia kwenye ukoo unaobudu masanamu, lakini akawa shujaa aliyetangaza imani mpya iliyokuja kuyavunja masanamu hayo hayo.

Ninachosema ni kuwa hii tabia ya yeye na wafuasi wake kujifanya kama kwamba walioinakamisha nchi hii walikuwa ni ‘wengine’ kabisa na wao ni tafauti mno, wakitaka kutuaminisha kuwa kwa utafauti wao huo, basi wataleta matokeo tafauti na yaliyofanywa na wao wenyiwao hadi hivi majuzi tu, ni kutututakana. Na matusi yatazidi kuwa makubwa kama sisi tutawaamini hivi hivi kichwa-mchungwa bila kuwahoji, kuwapima na kuwatia majaribuni.

Hivi sasa suala linalovuma ni la ripoti ya tume aliyoiunda mwenyewe Rais Magufuli na kuipa dhamana ya kuchunguza kiwango cha madini kwenye mchanga usafirishwao na makampuni ya madini kwenda nje ya nchi. Ugunduzi wa tume hiyo iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma umewatikisa wengi. Kilio kikubwa kimekuwa nchi kuibiwa na makampuni hayo kwa kiwango cha ajabu. Rais Magufuli na wafuasi wake wanatutaka sote tuitikie wimbo mmoja – wa mwizi wetu kugundulika na haja ya kumuadhibu vikali kadiri inavyoyumkinika.

Binafsi siujui ukweli wala uongo wa ripoti ya Mruma na kwa kuwa sijaona matokeo ya utafiti mwengine huru, naichukulia ripoti hiyo kama taarifa pekee iliyopo kwa sasa. Hadi hapo, utafiti mwengine na ulio huru utakapofanyika na kuja na matokeo tafauti, ripoti hii itakuwa ndiyo rejea pekee iliyopo. Lakini suala kubwa si ikiwa nchi inaibiwa au haiibiwi kwenye sekta ya madini. Suali kubwa lipo nyuma ya hapo. Wizi huu – kama kweli upo – uliwezekanaje?

Nimetangulia kusema kuwa Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitawaliwa na CCM tangu ilipopata uhuru wake. Kwanza zikiwa kama Tanganyika na Zanzibar chini ya TANU na ASP na kisha kama Tanzania chini ya CCM. Wao kwa wao, tena wao peke yao, walijitengenezea mifumo ya kisheria na kiutawala ambayo imewapa umiliki wote wa kila kilichomo kwenye ardhi na bahari. Wao ndio waamuzi wa mwisho na waamuzi wa pekee.

Mikataba ambayo imehalalisha ‘wizi’ wote wa rasilimali za nchi imeandikwa, kusainiwa na kuhifadhiwa na wao. Wao peke yao. Hata palipozuka vilio vya wananchi, wabunge, wanaharakati na wadau wengine wa maendeleo kwenye maeneo husika dhidi ya mikataba hiyo ya wizi, CCM ilisimama imara kuhakikisha kuwa inatekelezwa na kutimizwa kikamilifu. Kuna mifano kadhaa ya wapinzani wa mikataba hiyo kupigwa, kufungwa, kuteswa na hata kuuawa na vyombo vya dola vya serikali ya CCM.

Ni mithali ya baba mwenye nyumba anayewaalika wizi kuingia nyumbani mwake saa nane za usiku. Wakija akawafungulia milango waingie. Watoto na mama yao wanapotaka kuwazuwia, ni yeye mwenyewe ndiye anayewapiga, akawafunga kamba za miguu na mikono na akawaziba vitambaa vya mdomo na macho. Wizi wakakomba na kukokozoa watakacho. Kisha wakatoka. Wakiwa mtaa wa pili kuondoka na mali, anaanza kuingia barabarani kuwanadia: “Wezi hao, wezi… kamata.. piga… choma moto…!”

Ikiwa watoto na mama yao watamuamini kuwa kweli baba huyu anawachukia wezi wale, basi hapana shaka wanahitaji kupimwa akili zao. Ikiwa baba mwenyewe anaamini hasa kuwa anapambana na wezi hawa, yeye si wa kupimwa akili, bali ni wa kufungwa kabisa minyororo kwenye gogo, maana wazimu wake ushafika kiwango cha juu kabisa, kiasi cha kuanza kuamini yuko angani anapaa na ilhali yu ardhini anatambaa!

Ninachokusudia hasa kukisema kwenye jazanda hii, ni kuwa CCM inahusika asilimia 100 na kila uozo ambao umetokea ndani ya utawala wake, hasa hasa ule unaohusu mikataba mikubwa ya rasilimali za nchi. Mikataba hii yote ilihusiana moja kwa moja na uongozi wa juu wa nchi, ambao ndio pia uongozi wa juu wa chama hicho kinachotawala. CCM imejenga mfumo wa ufisadi mkubwa unaotendeka ndani ya nchi – himaya ya ujambazi wa kiuchumi, waa kisiasa na wa kidola.

CCM hii haina uhalali wa kisiasa wala uthubutu wa kimaadili kujipambanuwa na ujambazi huu unaoikamua nchi damu mbichi, maana haya ni matokeo ya utawala uliojilimbikizia kila kitu mikononi mwake kwa kauli na kwa vitendo.

Kwa hivyo, wakati wengi wetu tunakubaliana na hoja na haja ya kupambana vita vya kutetea rasilimali za nchi na tuko radhi kuingia na ama kushinda au kufa kwenye mapambano ya kurejesha umiliki wa nchi kwa wamiliki wenyewe, wengine hatuiamini CCM kuwa jemedari mkuu kwenye vita hivi.

Kutokumuamini kwetu kunatokana na rikodi yenyewe kwenye matukio ya wizi wote uliofanyika hadi dakika hii naandika makala hii. Jemedari huyu anaweza kutuulisha mara moja tukiwa mstari wa mbele wa mapambano, maana huyu ni baba aliyewafunga watoto wake kamba na vitambaa vya macho na kisha akawapiga sana, wakati akiwaruhusu wezi waingie kwenye nyumba yao kuiba. Huyu hafai!

Sasa, laiti mimi ningelikuwa ni Rais Magufuli ningelifanya nini? Ningelifanya mambo matatu yafuatayo: kwanza, mara tu baada ya kupokea ripoti ya Profesa Mruma na nikawa kweli nimeiamini kila kilichomo, basi ningelitoa hotuba kwa taifa kuwaomba radhi Watanzania wote kwa niaba ya chama changu na viongozi wote walioko madarakani na washaoondoka, kwa namna tulivyoshiriki kwenye kuifanyia ujambazi nchi yao.

Pili, ningelivunja bunge, nikaitisha uchaguzi wa mapema, ambao ningelipiga marufuku kiongozi wowote wa chama changu – kuanzia ngazi ya kijiji hadi ya taifa – kuwania wadhifa wowote ule kwa angalau miaka 20 kutoka sasa. Uchaguzi huo ningeliusimamia ili uwe huru, wa wazi na wa haki.

Na, tatu, ningelikabidhi madaraka kwa serikali itakayokuwa imechaguliwa na wananchi wenyewe, ambayo nayo ingeliyashughulikia haraka yale ambayo nimeyagundua kwenye ripoti za akina Profesa Mruma. Ningeyafanya hayo, sio kwa sababu mimi sina dhamira ya kupambana na ufisadi na uoza uliotamalaki kwenye taifa kwa nusu karne sasa, bali kwa kuwa najuwa ni mimi na chama changu ndiyo pumzi tulioupa uhai uoza huo.

Akili iliyoyaumba matatizo haiwezi kuwa akili ya kuyatatuwa matatizo hayo. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahitaji akili mpya ya kuizongowa mazonge iliyozongwa, na akili hiyo haipatikani ndani ya mfumo uliopo.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.