Amina asiyeaminika 

Katika majadiliano yake na mwandishi wa gazeti la Nipashe yaliyochapishwa jana, unaweza kuuona kirahisi mughma alionao Balozi Amina Salum Ali, baada ya kuhusika moja kwa moja katika uchafuzi wa suluhu iliyowekwa na waliomtangulia tokea mwaka 2009.

Wakati mwanasiasa huyu aliyegeuka kuwa mwanadiplomasia kwa kipindi kifupi, alipoondoka kuenda kushika nafasi ya kibalozi nchini Marekani, aliiwacha Zanzibar ikiwa taabani kiuchumi na kijamii. La ajabu ni kuwa siku tu alipotuwa mguu wake nchini kwa dhamira ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania (SMT) na kuukosa, alilolifanya ni kuirejesha Zanzibar kule kule alikoiacha katika miaka ya ’90.

Alichokifanya yeye ni kujituma na kutumika sio kwenye mradi wa kuyahujumu maelewano makubwa ya wananchi, bali pia hata mfumo mzima wa kidemokrasia uliowekwa ambao haukutoa mshindi hasa baina ya chama chake cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) bali ya kujumuisha maslahi mapana ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Unaweza kujiuliza kulikoni hasa leo hii awe na kauli laini kufika hadi kuukubali ukweli wa walio wengi ndio waliogoma kushiriki katika uchafuzi wao wa Machi 2016?

Na Foum Kimara

Balozi Amina anakiri kabisa kuwa kuna uhasama mkubwa baina ya wananchi, na hali iliyopo katika ardhi hii, hasa baada ya kurudi kwake, ni bughdha na uonevu tu kwa wananchi. Lakini labda leo tumtazame hasa kwa yakini kabisa ni nani Bi Amina na kuhusika kwake moja kwa moja katika kudidimia kwa maendeleo tokea aliposhika nafasi kuu ya Hazina ya Nchi katika miaka ya ’90,  halafu tujiulize hivi huyu mama anaweza kusimama akinadia haki, uadilifu na kuwa mwenye huzuni na haya yaliyopo?

Katika historia ya uongozi wake akiwa Mkuu wa Hazina, ndie waziri wa kwanza aliyeondoka akiiwacha nchi ikiwa imefilisika kabisa. Ndie waziri wa kwanza wa fedha katika historia ya nchi hii akiondoka huku akiiwacha serikali ikiwa haina hata mapato ya kulipa mishahara ya wafanyakazi wake kwa miezi sita. Anaondoka madarakani wizara ikiwa imejaa madeni, imejaa rushwa na inanuka ufisadi. Yeye ni mmoja wa sehemu hasa ya mikataba mibovu iliyoingamiza Zanzibar hadi kupoteza sifa zote za kuwa kituo cha kibiashara katika Afrika Mashariki. Kaondoka akihakikisha Serikali ya Zanzibar (SMZ) ni fukara. Leo eti ndiye anayeitwa Waziri wa Biashara, utegemee mabadiliko kweli?

Moja ya madeni ambayo hadi hii leo tunadaiwa ni lile lililoasisiwa naye moja kwa moja pale alipojisukuma katika mkataba na Nimrod Mkono kuidai Serikali ya Jamhuri ya Muungano fedha ambazo SMZ ikiidai kwa makubaliano ya kamisheni ya asilimia 15 kulipwa Mkono kama fidia ya madai hayo.

Hakukuwa na mkataba bali ni ile “retainer note” aliyoisaini mwenyewe inayotufunga sisi kimagirini kumlipa Mkono mamilioni ya pesa bila ya hata ushirikishwaji wa wanasheria wa serikali wakati ule. Deni hili hadi hii leo linadaiwa na Mkono na kalipandisha mpaka hadi sasa ni takribani shilingi bilioni 7.

Wakati ukishangaa ya mikataba ya mchanga wa dhahabu huko Tanganyika, huku kwetu tulikuwa na kikaratasi kimoja tu cha Waziri Amina kilichotuwekea deni lililofika sasa takribani bilioni 7.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliridhia kulipa sehemu ya deni baada ya Mkono kuzungumza nao akijuwa kabisa malipo yake si chini ya milioni sabini katika milioni 400 zilizotolewa na SMT.

Haya ndiyo matunda ya Balozi Amina, mgombea wa urais na aliyepewa sasa uwaziri mpya wa biashara, baada ya genge lao kutumika kuvunja maelewano yaliyokuwapo awali, kuvunja katiba ya wananchi na mabadiliko yake ya mwaka 2010 na zaidi kuiangusha ile dhamana ya makubaliano yaliyoasisi Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoleta na afuweni kwa jamii nzima ya wananchi hapa visiwani.

Umasikini wetu huu umechangiwa pakubwa na mfano wa viongozi wa namna hii. Unafikiri kama si maslahi binafsi, wangekuwa na ushawishi wa kuufuta uchaguzi huru? Unawahesabu washiriki wakuu na kuhesabu pia madhambi yao na maslahi yao.

Nakumbuka pale mwaka 2000, wakati wa siku za awali za uongozi wa Dk. Amani Karume, mwanasheria Mkono alikuja tena na madai kutokana na ile ile “retainer note” ya Waziri Amina. Mara hii akidai shilingi bilioni 2 kama sehemu ya kamisheni yake anayoidai SMZ. Hakufanikiwa maana alipuuzwa, lakini hakuishia hapo, bali akarudi tena baada ya kutangazwa Dk. Ali Mohamed Shein kuwa rais mwaka 2010 na mara hii deni lake likapanda kufikia takriban bilioni 7. Wakati Bara wakilalamika wanaoitwa wanyonyaji wa nje, Zanzibar inaliwa na wanyonyaji wa ndani na hawa kina Mkono na bughdha ya deni la kidhalimu.

Hili lilipingwa na waliobeba dhamana ya kusimamia sheria za nchi na serikali na halikufanikiwa katika kipindi kwa muda wa 2010 mpaka 2015, kwa sababu kulikuwa na waliobeba dhamana hasa ya kuhakikisha hatuwi tena kichwa cha mwendawazimu kinachonyolewa na kila mtu.

Wakati akijipanga kwa urais wa 2015, hakuna aliyemkumbusha namna gani hazina alivyoiacha Zanzibar na kuifisidi na kudaiwa kila pembe ya nchi. Hakuna aliyemkumbusha “Retainer Note” yake ilioibebesha Serikali na umma huu mabilioni ya pesa kwa deni hewa, ambalo ni yeye aliyeingia mkataba nalo na kutuachia hadi hii leo likitusumbua. Hakuna anayemkumbusha hivi sasa matokeo ya kukurupuka katika uongozi wake uliotutia hasara kirahisi rahisi.

Ukitaka kuzijua nia za hawa watu, basi usishangae kwa sasa anayeshikilia deni hili lilipwe ni huyu huyu “Bwana Sifanyi Chochote”, ambaye naye pia ni balozi kama alivyo waziri wake. Inakufanya wakati mwengine ufikiri hivi mpaka lini viongozi wa Zanzibar watahadaiwa na “viji-appartment” vya Kigamboni, huku wakidhamiria kabisa kuitia umaskini nchi?

Unafika mtu nafasi ya kuwa msimamizi mkuu wa Serikali, lakini huridhiki wala huna huruma kwa wanyonge na watoto wanaolalia uji na kuamkia uji patupu. Halikuumi basi tumbo unapowakuta watoto wa kimasikini wakijaa vumbi kwa kukosa hata madawati ya shule, wakati kuna bilioni 7 zinazotaka kuangamizwa kienyejienyeji?

Fikiri hizi bilioni 7 zingewasaidia wananchi kwa namna ipi hasa ukisikia hospitali hazina dawa? Haya mafuriko na kiburi cha kuwaambia wananchi wanajenga bila ya mpangilio, jee zisingeweza kusaidia kuirejesha miundombinu na kutusogezea maendeleo? Hivi kweli zisingeweza kutusaidia sisi tunaozaliana bila mpangilio katika maendeleo kama ambavyo Dk. Shein anavyolalamika? Fikiri wale wajawazito wanaohangaika na vichanga hospitalini kwa afya ya kubahatisha kabisa, jee zingewasogeza wapi fedha hizi? Basi hata Mungu hamumuoni na huu ulaji uliokithiri na kuvuka mipaka, basi hata ya utu? Tuna deni la umeme, jee halilipiki?

 

Sasa vuta picha ya kule Uwanja wa Ndege na haya yanayofanyika. Tazama ile meli iliyonunuliwa ikidaiwa kuwa ni mpya. Tazama pia namna gani kila penye nia ya maendeleo hakuna linaloendelea. Yote kwa sababu ya mazowea ya nchi chini ya watawala hawa ni kujinufaisha binafsi.

Wakati tukipiga kelele kwa hili sakata la mchanga wa dhahabu na hii mikataba yetu, basi na huku Zanzibar chini ya mawaziri hawa ndio sababu ya kukwama kwa kila nyenzo ya maendeleo. Ikiwa Msimamizi Mkuu wa Serikali ambaye anawajibika na kuiwakilisha serikali hadi kwenye chombo cha kutunga sheria, ndiye anaeshadidia kuitia nchi katika hasara ya namna hii ,hivi hao anaowasimamia watakuwaje?

Tumalize kwa kujiuliza: hivi kweli huyu mama anaweza kunyanyuka na kutuusia wananchi maadili, uadilifu na umoja, wakati yeye binafsi ni sehemu kubwa ya mtafaruku uliopo, kwa sababu tu ya mazowea ya ubinafsi na maslahi yake mwenyewe? Hivi huyu mama atasimama lini na kutuomba radhi wananchi kwa naqama aliyotuwachia wakati akiwa Waziri wa Fedha na hizi “Retainer Notes” zilizotufikisha hapa kiasi cha kudaiwa bilioni 7 kirahisi ahisi? Hivi tuseme hawa wangelikuwa upande wa pili,  wangelisalimika na utumbuaji unaoendelea? Hivi haoni haya kabisa kwa hii “legacy” yake visiwani?

Anataka awaaminishe wana CCM kuwa tatizo lao kukosa kura Zanzibar, ati ni kwa sababu ya Wapemba kuletwa Unguja kupiga kura. Ikiwa ni Wapemba wanapungua kwa idadi hiyo kisiwani Pemba, sasa kwa nini basi na hiyo idadi ndogo waliyobaki bado CCM haitakiwi? Au kwa nini kuna ongezeko la kura za upinzani katika kila mkoa wa kisiwa cha Unguja? Hivi anataka kuwaambia wananchi kuwa ni Wapemba walioko Kaskazini kabisa hadi mwisho kule Kusini mwa Unguja? Basi mpaka Makunduchi?

Ukweli ni kuwa anguko la CCM ni kwa sababu ya mazowea ya uongozi wa aina yake. Yaani karatasi ya ukurasa mmoja tu inayoidhinishwa na yeye binafsi imetufikishia deni la bilioni 7, halafu kweli atuonyeshe mchawi ni nani? Haya ndio yaliyopelekea kulazimishwa kuchukuwa mapumziko wakati ule akiwa Hazina. Leo anahubiri uadilifu, maadili na wema. Wapi!? Aangelianza kwa vitendo kwanza kwa kukata mshahara wake kulipa fidia ya hasara aliyotuingiza.

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

3 Comments

  1. Hayo uliyoyaandika hapo no ya uongo mtupu kama unakumbuka vyema wakati wa rais Salmin name bi Amina waziri wa fed ha ndio wakati ulikuwa wa neema. Kama ulisahau sisi tunakumbuka. Leo unamdomo baada ya kushiba na uongozi wa Dr Salmin kuwapa utajiri na kufungua biashara ulimwengu mzima. Biashara zilishamiri kila mtu alipata riziki. Wafanyakazi walikuwa na mabiashara hata mshahara hawakutegemea.Wao ndio waliowafungulia riziki hadi Leo mkawa na midomo mirefu wa kuwatukana.Wengi wenu huko Dubai mlianza kwenda katika utawala huo. Sasa jiulize baada ya hawa alikuja rais gani? baada ya ufisadi wenu 1995 si nyie mlozunguka dunia nzima mpaka nchi ikanyimwa misaada hata chanzo za watoto. Tafadhali fatilia hizo infomation zako vizuri muache kuandika ya uongo.

  2. Kumekuwepo na upotoshaji wa kinaki na chuki za kisiasa zinazo sambazwa na wanasiasa uchwara waliofilisika kifira na kukosa tu kutambua dhana ya neno upinzani na badala yake wao ni kupinga tu,baadhi ya vijana na cuf wanaotumiwa na viongozi wao MUFLISI WA KISIASA dhidi ya Mh Waziri wa Biashara na Viwanda Mh Amina Salum Ali kuwa ni kiongozi hatari tokea alipokuwa Waziri wa Fedha 1995,Ikumbukwe hawa hawa wanaopaza mdomo leo kumkebehi Mh Amina na ndio hawa hawa waliofaidika na mikakati yake madhubuti ambayo waliifanya Zanzibar kua kitovu cha biashara Africa mashariki yote na nchi nyengine za jirani kuja Zanzibar kufata bidhaa kadha wakadha hadi kufikia Zanzibar kuitwa Dubai ndogo,Furasa na milango ya kibiashara ilifunguka na wapinzani hawo wengi wao ndio wanufaika wakubwa na ndio chanzo cha utajiri wao,Baada kushiba na nema ktk uongozi wa Dr Salmin na serekali yake ikiongozwa na Waziri muandamizi Mh Amina Salum Ali ,baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 NA CUF KUJITEKENYA WENYEWE NA KUCHEKA WENYEWE Kwa kijitamgazia ushindi hewa ndipo Maalim Self Sharif Hamad alipozunguka dunia na kuomba Zanzibar ikatiwe msaada,HUYU NDIYE MCHAWI WENU, lkn kutokana na uimara wa viongozi wa wakati huo ikiomgozwa na Waziri aliekua akiihudumu wizara ya Fedha bado Zanzibar iliendelea kuwa imara kibiashara pamoja na kukatwa Kwa misaada iliosababikshwa na wasioitakia nchi mema cha ajabu watu hao leo wanapata wapi ujasiri wa kumchafua kisiasa mtu aliewatengenezea njia ya wao kuinuka kimaisha?hizi tunaziita ni propaganda uchwara na nypesi ambazo hufanywa na wanasiasa uchwara waliofilisika kisiasa na kufikiri Kwa kutumia nyayo baada ya kichwa ktk DUNIA HAKUNA KWELI MBILI ukweli utabakia kuwa ukweli siasa za kidhandiki hazina nafasi ktk wakati huu,NIWASHAURI TU WANASICUF NA VIJANA MNAOTUMIWA NA VIONGIZI WENU MUFLISI KWANZA JENGINI CHAMA CHENU AMBACHO HATMA YAKE INAELEKEA KULIFATA JINA LA CHAMA CUF(KUFA)uzalendo wa Amina Salum Ali kwa nchi yake utabaki kuwa ni uzalendo na huko kumchafu kwenu ni dali tosho za kuona Mwanamama huyu ni kikwazo Kwa cuf ambayo mbele kuna wanaume ambao wanahofu kubwa na Mwanamama thabiti jembe la kupigiwa mfano,MH AMINA SALUM ALI FANYA KAZI ZAKO MANENO YA MUFLISI WA KISIASA YASIRUDISHE NYUMA JUHUDI ZAKO ZA KUITUMIKIA NCHI YAKO KTK NAFASI YAKO YA UWAZIRI WA BIASHARA NA VIWANDA

  3. Kumekuwepo na upotoshaji wa kinaki na chuki za kisiasa zinazo sambazwa na wanasiasa uchwara waliofilisika kifira na kukosa tu kutambua dhana ya neno upinzani na badala yake wao ni kupinga tu,baadhi ya vijana na cuf wanaotumiwa na viongozi wao MUFLISI WA KISIASA dhidi ya Mh Waziri wa Biashara na Viwanda Mh Amina Salum Ali kuwa ni kiongozi hatari tokea alipokuwa Waziri wa Fedha 1995,Ikumbukwe hawa hawa wanaopaza mdomo leo kumkebehi Mh Amina na ndio hawa hawa waliofaidika na mikakati yake madhubuti ambayo waliifanya Zanzibar kua kitovu cha biashara Africa mashariki yote na nchi nyengine za jirani kuja Zanzibar kufata bidhaa kadha wakadha hadi kufikia Zanzibar kuitwa Dubai ndogo,Furasa na milango ya kibiashara ilifunguka na wapinzani hawo wengi wao ndio wanufaika wakubwa na ndio chanzo cha utajiri wao,Baada kushiba na nema ktk uongozi wa Dr Salmin na serekali yake ikiongozwa na Waziri muandamizi Mh Amina Salum Ali ,baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 NA CUF KUJITEKENYA WENYEWE NA KUCHEKA WENYEWE Kwa kijitamgazia ushindi hewa ndipo Maalim Self Sharif Hamad alipozunguka dunia na kuomba Zanzibar ikatiwe msaada,HUYU NDIYE MCHAWI WENU, lkn kutokana na uimara wa viongozi wa wakati huo ikiomgozwa na Waziri aliekua akiihudumu wizara ya Fedha bado Zanzibar iliendelea kuwa imara kibiashara pamoja na kukatwa Kwa misaada iliosababikshwa na wasioitakia nchi mema cha ajabu watu hao leo wanapata wapi ujasiri wa kumchafua kisiasa mtu aliewatengenezea njia ya wao kuinuka kimaisha?hizi tunaziita ni propaganda uchwara na nypesi ambazo hufanywa na wanasiasa uchwara waliofilisika kisiasa na kufikiri Kwa kutumia nyayo baada ya kichwa ktk DUNIA HAKUNA KWELI MBILI ukweli utabakia kuwa ukweli siasa za kidhandiki hazina nafasi ktk wakati huu,NIWASHAURI TU WANASICUF NA VIJANA MNAOTUMIWA NA VIONGIZI WENU MUFLISI KWANZA JENGINI CHAMA CHENU AMBACHO HATMA YAKE INAELEKEA KULIFATA JINA LA CHAMA CUF(KUFA)uzalendo wa Amina Salum Ali kwa nchi yake utabaki kuwa ni uzalendo na huko kumchafu kwenu ni dali tosho za kuona Mwanamama huyu ni kikwazo Kwa cuf ambayo mbele kuna wanaume ambao wanahofu kubwa na Mwanamama thabiti jembe la kupigiwa mfano,MH AMINA SALUM ALI FANYA KAZI ZAKO MANENO YA MUFLISI WA KISIASA YASIRUDISHE NYUMA JUHUDI ZAKO ZA KUITUMIKIA NCHI YAKO KTK NAFASI YAKO YA UWAZIRI WA BIASHARA NA VIWANDA

Leave a Reply to stela. gwamaka Cancel reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.