HABARI

Fursa Kijani na ukombozi wa vijana Zanzibar

“Tukiwezeshwa tunaweza” ni msemo maarufu hasa kwa wanawake ambao wanajishughulisha na ujasiriamali kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Lakini msemo huu unatafisiriwa vizuri hapa Zanzibar ambapo vijana zaidi 70 wamewezeshwa kupata muelekeo kuwa wazalishaji wazuri kwa ajili ya maendeleo ya taifa na familia zao.

Vijana hao, ambao awali walikuwa wamekata tamaa kwa kukosa jambo la kufanya ili kujikwamua kimaisha, walitafutwa kwa njia mbalimbali ili kupewa elimu ya uzalishaji wa kila aina, kikiwemo kilimo hai, yaani kisichotumia kemikali; ufugaji nyuki, pamoja na utengenezaji mbolea ya kiasili, chini ya mradi unaojuilikana kwa jina la Fursa Kijani.

Mafunzo hayo yanalenga kuwashajiisha vijana kujishughulisha na kilimo hai na kuacha kujishughulisha na kilimo cha kisasa ambacho kinatumia mbolea za kemikali zinazoharibu mazingira na afya za binaadamu.

Bernadette Kirsch ambaye ni mwanzilishi wa Practical Permaculture Institute of Zanzibar, taasisi inayowasomesha vijana hao, anasema wanataka kujikita katika kuleta matokeo mazuri yenye faida kiuchumi, kijamii na kimazingira.

“Hawa vijana wakishapata elimu hii, tunawaomba kuwasaidia wenzao wengine ili waweze kujikwamua kimaisha kupitia Fursa Kijani,” anaongeza Kirsch.

Lengo ni kuwainua vijana

Milele Foundation Zanzibar kwa sasa ndiyo taasisi inayofadhili mradi huu wa Fursa Kijani ambao ulizinduliwa mwaka 2016 kutengeneza fursa kwa vijana wa kike na kiume na ambao hawapo mashuleni. Kupitia kazi za kijani, vijana hao wanapata uwezo na ujuzi wa vitendo na pia kuunganishwa na wanufaikaji wa mradi na ujuzi halisi wa kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Fumba Town Service Center, Sebastian Dietzold, akitoa maelezo ya nafasi ambazo huwapatia vijana mara baada ya kuhitimu masomo yao katika Chuo cha Practical Permacuture Institute of Zanzibar ambapo wanafunzi wake hupata udhamini wa Milele Foundation.

Mratibu wa mradi huo kupitia Milele Foundation Zanzibar, Bi Khadija Sharif, anasema kuwa vijana hao hupata ufadhili wa kila kitu kwa wiki mbili ambao unawasaidia kulala hapo hapo kwenye eneo la mafunzo.

“Lengo la kutoa full scholarship (ufadhili kamili) ni kutaka kuwawezesha vijana hawa kikamilifu ili waweze kutoka na kitu ambacho tumekikusudia kwa ajili yao na nchi yao,” anaeleza Bi Khadija, akiongeza kuwa mradi huo ni wa majaribio kwa sasa na endapo ukifanikiwa una lengo la kuwachukua vijana wengi wa Kizanzibari ili “kujenga taifa lenye vijana imara na maisha bora.”

“Tunataka tutoe timu bora ambayo itapelekea kupata na jamii iliyo imara,” ndilo dhamira kuu kwa mujibu wa Bi Khadija, anayesema pia kuwa mafunzo yanayotolewa hapo yanajumuisha wiki mbili za kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kilimo endelevu na miezi mitatu ya kujifunza kazini katika kituo cha Fumba Town Service Center (FTSC).

Changamoto zinazowakabili waandalizi

Licha ya kazi hiyo kubwa inayofanywa na taasisi hii ya Milele, katika hatua hii ya awali tayari kumejitokeza changamoto kadhaa, ikiwemo ile ya baadhi ya vijana walikimbia kabla ya masomo kwisha.

“Lakini tuligundua wale vijana walikuwa na shghuli nyengine ndio ikawa hawakuwa na kitulizano pale chuoni lakini kwa sasa tumejipanga vizuri” alieleza Khadija.

Alieleza changamoto nyengine wanayokabiliana nayo ni kutokana hali za maisha za vijana kwani wanatoka katika familia masikini sana na sasa wanategemea kila kitu kwao wao na lakini wamejitahidi kuzitatua na sasa hali inakwenda vyema.

Kituo hicho FTSC kinaonekana kutoa mchango mkubwa kwa vijana hao kwani mara wanapomaliza mafunzo kutoka katika chuo cha Practical Permaculture Institute of Zanzibar huwachukua wahitimu hao na kuwapatia mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi mitatu.

Kutoka mtaani hadi kwenye utaalamu

Mara baada ya kumaliza mafunzo hayo ya vitendo, kituo hicho huwafanyia usaili wahitimu hao na baadaye huto ajira kwa wale ambao watafaulu. Hadi sasa, tayari imeshaajiri vijana 30 kutoka kwenye mradi wa Fursa Kijani kati ya 70, huku wengine wakipata ajira kutoka sehemu nyingine kama vile  mahoteli.

Mwandishi wa makala hii, Talib Ussi, akizungumza na wahitimu wa mafunzo mbalimbali katika mradi wa Fursa Kijani ambao hufadhiliwa na Milele Foundation.

“Lengo la kuuwachukuwa hawa vijana ni kutaka kufikia malengo ya taasisi yetu ya kujenga nyumba bora,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa FTSC, Sebastian Dietzold, akiwa afisini kwake Fumba, umbali wa karibuni kilo mita 25 kutoka kitovu cha Mji wa Zanzibar.

“Sisi tunajenga nyumba ambayo yatakuwa ni makazi bora, lakini kama hakuna maisha mazuri, hatutakuwa tumefikia hilo lengo,” anaongeza Dietzold, akifafanua kuwa huwa wanawawezesha vijana hao ili maisha yao yawe ya kisasa kwa kutegemea zaidi kilimo hai ambacho hakina athari kwa binaadamu.

“Awali vijana wengi walikuwa hawana uwezo wala fikra zozote zile, lakini sasa kama taasisi tunajivunia vijana wengi ambao wamepata masomo na kuzalisha vitu vya aina tofauti. Nawaomba vijana wote ambao hawana uwezo wajitokeze na watawezeshwa ili na wao waweze kujikwamua, kwani fursa zipo nyingi hasa wakishapata ujuzi,” anasema Dietzold.

Muharami Ali Hamad ni miongoni mwa vijana ambao walipata mafunzo hayo kupitia mradi huo wa Fursa Kijani. Kijana huyu sasa anazishukuru taasisi hizo has,a akieleza thamani yake kubwa kwa Milele Foundation Zanzibar ambayo ndiyo iliyomdhamini kupata ujunzi alinao.

“Leo unaponiona hapa kaka’angu nafanya kitu ambacho katika akili yangu ya kawaida hakikuwemo. Namshukuru Mola wangu halafu sasa nisipoishukuru taasisi hii nitakosa radhi zake,” anasema Muharami, ambaye anafanya kazi kwenye kitengo cha kufuga asali ya kisasa ambayo inatumia utaalamu wa hali ya juu tofauti na ile iliyozoeleka.

Kwa upande wake, Bi Ujudi Ali Khamis, ambaye yeye anafanya kazi katika kituo cha kutengeza mbolea hai, anasema kuwa ni wakati wake sasa kuwapitia wanawake wenzake na kuwashawishi waweze kujiunga na chuo ili baadaye waweze kuwa na taifa ambalo vijana walio wengi wanaweza kujitegemea.

“Kazi yangu sasa hapa ni kutengeza mbolea. Lakini nikitoka tu kazini, huwa nakwenda kutoa elimu kwa wenzangu mitaani,” anasema Bi Ujudi.

TANBIHI: Makala hii pamoja na picha imetumwa na mwandishi wa habari wa kujitegemea visiwani Zanzibar, Talib Ussi.

 

2 thoughts on “Fursa Kijani na ukombozi wa vijana Zanzibar”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.