HABARI

Kwa nini siwezi kuuamini muhimili huu katika madini 

Wabunge wa chama fulani na ambao kutokana na wingi wao ndio waamuzi wa kila kitu kwenye muhimili huo uliotakiwa kuwa muhimu nchini petu, nao wanataka tuwaamini na tuliamini bunge hili kwenye hili sakata la madini. Lakini wenye akili wanajiuliza waaminiwe kwa lipi?

Ni muhimili huu huu ambao mwaka 1997 ulipitisha kwa dharura sheria mbili: ile ya kodi na ya uwekezaji, ambazo ndizo zilizowahalalishiaa wawekezaji kuwapa madini yetu. Ndizo sheria ambazo zilifuta kodi nyingi kwenye sekta ya madini, huku muhimili huu huu ukiitikia: “Ndiyo!” kuhalalisha wawekezaji kusamehewa  na kufutiwa kodi!
Ni hawa hawa ambao mwaka 2007 walimfukuza bungeni Zitto Kabwe baada ya kutaka ufanyike uchunguzi kwenye mkataba kati serikali na huyu huyu Acacia wakati huo akiitwa Barrick. Hawa hawa walitetea huo mkataba uliowaruhusu Barrick kusafirisha haya makinikia. 

Hawa hawa walikataa waziri aliyesaini mkataba huo asijadiliwe bungeni na kumuadhibu aliyeibua hoja kuhusu Mkataba huo ulioidhinisha wana Kahama wafukuzwe kwenye maeneo yao kuwapisha hawa Acacia!

Tena waliotetea mkataba huu uliovuja mpaka kwenye vyombo vya habari, baadhi yao bado wamo bungeni, wengine ni viongozi bungeni!

Bunge la Tanzania 

Ni hawa hawa, na wengine wamo bungeni tena ni viongozi, ambao mwaka 2010 waliitetea sheria ya madini na kupiga kura za ndiyo kwa sheria hii inayowapunja wazawa kwenye malipo ya fidia, baada ya kuhamishwa kupisha wawekezaji wakiwemo Acacia!

Hii sheria ya ajabu inayosema eti Mtanzania anamiliki sehemu ya juu ya ardhi, huko chini siyo mali yake. Ni muhimili huu huu ndiyo mwaka 2010 uliotunga sheria ya kuwafanya watu wanaoishi pembezoni mwa migodi wawe masikini wa kutupwa pamoja na kuishi sehemu yenye utajiri!

Ni muhimili huu huu ambao mwaka 2009, baada ya uovu kukithiri huko kwenye mgodi wa Barrick,  pale wananchi wa Nyamongo walipotiririshiwa sumu, baadhi wakababuka, wengine wakapoteza maisha, mifugo ikafa, ardhi ikachafuliwa na sumu, ukaunda Kamati mwaka 2009, lakini matokeo yake ni kuwa Kamati hiyo iliwakumbatia wawekezaji na kuwaita waathirika wa sumu kuwa ni wavamizi na wizi. 

Askari wa kutuliza fujo wa Tanzania mgodini akipambana na wananchi 

Kinachonisikitisha ni kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati ile bado wamo bungeni. Wale waliowasaliti wana wa Nyamongo kwa kuwaambia kuwa wamejitakia kwa kuwavamia wawekezaji, leo hii wanajidai kuongea kwa hasira. 

Wakati mwaka 2009 waliwasaliti Watanzania na kuwatetea wawekezaji, leo wanataka tuwaone vinara wanaopambana na wizi huu wa madini!

Mwaka 2004, Watanzania waliokuwa wanaishi kijiji cha Mtakatifu wakihamishwa kinyama, usiku wa manane. Kamati ya muhimili ili huu huu ilikwenda Geita, ikashuhudia Watanzania wakiishi kwenye jengo chakavu la mahakama eneo la Sofia Town. 

Mitambo ya wawekezaji mgodini 

Baadhi ya waliounda Kamati hiyo mpaka leo wamo bungeni, lakini walifumbia macho unyama huu, waliwaita watu wa Mtakuja wavamizi, na leo wanataka tuwaamini kuwa wana uchungu dhidi ya wizi huu!

Hivi hawa wabunge hawajui chochote kinachoendelea Geita? Hawajui kinachoendelea Nyamongo? Hawajui kinachoendelea Mererani? Wanasubiri nani aseme kinachoendelea huko? Je, wao wanachojua ni ‘makinikia’ tu?

Huu muhimili huu umekaa kimya miaka yote. Kamati ya Bomani, Kamati ya Lau, Kamati ziliundwa zaidi ya tatu kabla ya hii, ripoti mbali mbali zimetoka zikithibitisha uporwaji wa mali zetu, na huu muhimili ulikuwa unatazama tu, kisha bado wanataka tuwaamini kuwa wao ni wapambanaji wa kwelikweli dhidi ya unyang’au huu! 

Nakumbuka baada ya Mto Tigithe kumwagiwa sumu, kamati ya viongozi wa dini iliunda timu ya wataalam kuchunguza kama kweli mto huo ulichafuliwa na sumu kutoka Barrick. Ripoti ilitoka na ikathibitisha kuwa mto ulichafuliwa na sumu. Huu mhimili kimya! Haukuwahi hata kuutumia utafiti huo kusaka haki ya waathirika wa sumu za Tigithe!
Ni muhimili huu huu ndiyo uliotunga sheria ya sisi kupata mrahaba wa asilimia nne (4%) tu. Ni hawa hawa waliopitisha sheria hii, sasa wanataka tuwaamini kwa lipi?

Muhimili huu ujitafakari unapojadili mambo mazito ya nchi hii. Ujipime kwa uzalendo wake. Ujipime uwezo wake katoka kuisimamia serikali. Ujipime uwezo wake kuwawakilisha Watanzania!

Huu muhimili huu!! 
Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Dotto Bulendu kwenye ukurasa wake wa Facebook tarehe 2 Juni 2017.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.