CCM Zanzibar na viti vyao vya barafu 

Balozi Seif Ali Iddi

Jiwe la barafu lililoivia baridi kali liko mithili ya chuma. Hufanana na chuma kwa uzito na hata ugumu wake. Likikuangukia mguuni ni sawa tu na uliyeangukiwa na kipande cha chuma kwa kile kishindo na maumivu yake. Kitu pekee kitakachokufanya ujuwe kuwa kilichokuangukia mguuni sio chuma ni vile kuzizima kwake.

Ugumu, uzito na umadhubuti huu wa jiwe la barafu hutegemea kushuka sana kwa kiwango cha joto pale ulipo. Kila joto likishuka, ndipo barafu nayo huwa madhubuti zaidi. Kinyume chake ni kuwa kila joto likipanda, ndipo nalo jiwe hili la barafu hupoteza haiba, nguvu na umadhubuti wake na, hatimaye kuyayuka ghafla. Na aibu yake sasa! Likiyayuka halipitii hata katika hatua ya mchanga na vumbi, ni maji moja kwa moja. Hayoo!

Madaraka, nguvu, jeuri na kiburi cha watawala  wa Zanzibar tokea kumalizika kwa uchaguzi wa tarehe 25  Oktoba 2015 na hasa hivi sasa, tunaweza kufananisha na jiwe la barafu lililoshiba baridi kali kama yale mawe ya barafu yaliyoko katika milima ya Alps kule Ulaya.

Na Ahmed Omar

Hawa wameshiba jeuri na  kiburi chao hicho kilichotegemea sana msingi mmoja tu wa kuugeuza uongo na kuutegemea uwe kama ndio ukweli kupitia maamuzi ya kinafiki ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kinywa cha Jecha Salim Jecha alipotangaza eti uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 umeharibika.

Hivi sasa watawala wanaendeleza  dhulma zao na maovu yao. Wanaendelea kupanga na kutekeleza vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhulumu na kuwabagua Wazanzibari kama ilivyo kawaida yao. Hawana wasiwasi. Wamejitanafasi katika viti vyao vya barafu wanatikisa miguu huku wakitoa maamuzi na amri za kifedhuli, kibabe na kidhalimu.

Ukiwauliza wana CCM: kwani hamuyajui yaliyotendeka? Kwani hamujui kwamba chama chenu kimevunja katiba ya nchi, sheria, matakwa na matashi ya raia, uhuru wao, haki zao, matumaini yao na hisia zao? Wanakujibu: “Yote tunayajuwa na ni kweli tupu!”

Ukiwauliza tena: kwani hamjui kwamba chama chenu kimevunja mikataba ya demokraisa na haki za binadamu ya kilimwengu na kuipaka kinyesi? Wanakujibu: “Tunayajua yote na ni kweli tupu!”

Ukiwauliza: kwani hamjui kwamba chama chenu kimeiingiza nchi katika mahusiano mabaya ya kidiplomasia na nchi mbalimbali za ulimwengi na jamii ya kimataifa kwa ujumla? Watakujibu: “Tunayajuwa yote na ni ukweli mtupu!”

Sasa waulize: kwa nini sasa hawa CCM wanafanya hivi? Jeuri na kiburi hichi wanatoa wapi? Sikiliza majibu yao hapo: “Nchi hii ni ya kimapinduzi. Tulipomfukuza mkoloni, tulimwaga damu. Hatuwezi kuwapa CUF nchi kwa kura. CUF hata ishinde kwa kura zote na mara zote, milele abadan haipewi hatamu za nchi hii kuongoza. Dunia nayo haiwezi kutuingilia kwa lolote. Haya ni mambo ya ndani ya nchi yetu. Hamuoni mumezunguka dunia nzima hakuna mulilolipata? Hakuna mabadiliko yoyote wala uchaguzi mpya mpaka 2020!”

Hayo ndio majibu pekee ya CCM wala hakuna mengine. Hakuna majibu ya utetezi wala ya kihoja. Ni havo tu. Sasa cha kushangaza kuna Wazanzibari wanayaogopa majibu hayo sana. Wanaamini hayo majibu ndio mwisho wa safari. Hakuna la kufanywa wala kuwa. Ndio waladhwaalina, Amiina!

Labda tujiulize maswali machache: Hivi jeuri hii ya CCM inatokana na kuwa na nguvu kubwa za kijeshi duniani kujilinda na kuingiliwa na nchi nyengine pale wafanyapo maamuzi yasiyokubalika? Hivi watawala wetu hawa madikteta wameiamini jeuri yao kwa kuwa tuna uchumi mkubwa duniani usiotetereka na usiotegemea misaada kutoka popote na hivyo nchi yetu haishurutishwi wala haipokei mashinikizo ya kupinga dhuluma dhidi ya raia?

Hivi jeuri hii ya kwenda kinyume na mikataba ya kimataifa bila hofu, ni kwa sababu nchi yetu ni muhimu sana duniani kiasi ambacho haioni haja sana na kuheshimu mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia ya kiulimwengu?  Au ni kwamba nchi yetu imekamilika kila idara haitetereki na haitetereshwi? Ina jeuri kama Korea Kaskazini, Urusi na China?

Jawabu ni kuwa: hapana, nchi yetu haina jeuri na kiburi cha uchumi, kijeshi wala kidiplomasia. Ni masikini na wanyonge wa kutupwa. Ubabe, udikteta na udhalimu wetu si kama wa Korea Kaskazini, China wala Urusi. Hivyo basi watawala wetu wasione kimya, wakadhani  ulimwengu hautachukuwa nafasi yake.

Dunia haikurupuki katika kuchukuwa hatua zake dhidi ya nchi ya madikteta na madhalimu. Wenzetu ni watu wa misingi. Wanaongozwa na njia zao na taratibu zao kwa umakini mkubwa. Hatimaye, huhakikisha ni lazima nchi ziwaheshimu raia, haki zao na matashi yao.

Wazaanzibari tunapaswa tuamini kuwa dunia haipo kimya na katu haiwezi kukaa kimya dhidi ya madhalimu hawa wa haki za msingi za raia na mahodari wa uonevu. Viti walivyokalia watawala wetu wa Zanzibar ni vya barafu tu. Baridi imeshawadanganya kwa mwaka mmoja wakajiona wako juu ya madaraka madhubuti, yasiolegalega. Sasa joto limepanda na linazidi kupanda kwa kasi kubwa na viti vimeanza kuyayuka.

Vinayayuka na muda si mrefu wataanguka chini.
Babu Ali safari hiyo imewadia!
Unayo!

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Omar kwenye ukurasa wake wa Facebook tarehe 4 Juni 2017

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.