CCM inajiandalia kiama chake yenyewe

CHAMA CHA MAPINDUZI kinachotawala nchini Tanzania ni muunganiko wa vyama viwili vya siasa: TANU  kwa upande wa Tanzania Bara na ASP kwa upande wa Zanzibar. Kwa hapa nataka niiangalie CCM ya upande wa Tanzania Bara, nikihusisha na mzazi wake kwa upande huo, TANU.
 
Tunakumbuka kwamba TANU ndiyo iliyosimamia harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kwa kipindi kirefu na kwa mafanikio, kikitumia hoja kali bila ulazima wa kushika silaha. Japo baadaye vilijitokeza vyama vingine katika harakati hizo lakini vikawa na hoja legevu, ndiyo maana wananchi wakakiamini TANU kiasi cha wakoloni wa Kiingereza kuamua kukikabidhi nchi chama hicho.
 
Hoja za TANU ziliendelea kuwaingia wananchi na hata viongozi wa vyama vingine vya siasa walioamua “kubwaga  manyang’a” na kujiunga na TANU bila chama hicho kutumia mabavu wala vitisho na kujikuta ni chama pekee cha siasa nchini Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar kutengeneza Tanzania.
 
Muda wote baada ya Muungano wa Tanzania  TANU iliendelea kukubalika kwa wananchi kwa upande wa Bara wakikichukulia kama chama chao pendwa. Siri ya mapenzi hayo, ambayo sasa iko wazi, ni kwa sababu chama hicho hakikutumia mabavu kuwalazimisha wananchi kujiunga nacho, ni hoja tu zilizowashawishi kukithamini.
 
Katikati mwa miaka ya 1970 ukafanyika mchakato wa kuiunganisha TANU na ASP ya Zanzibar na ndipo ikazaliwa CCM mwaka 1977, chama kilichokuwa imara chini ya uongozi makini wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere. Sote tunaona kuwa CCM ya wakati huo ni tofauti kabisa na CCM ya wakati huu.
 
CCM hiyo haikuwahi kutegemea hata mara moja nguvu za dola. Kile kilikuwa ni chama chenye makada, watu wanaokijua wanachokifanya. Tofauti na sasa ambapo kila anayevaa shati la kijani anajiita kada wa chama!
 
Ikumbukwe wakati huo vilikuwepo vyuo vingi vya siasa vikiongozwa na ambacho naweza kusema kilikuwa Chuo Kikuu cha Siasa cha Kivukoni. Watu walikuwa wanasoma siasa, itikadi na ushawishi wa kisiasa. Wanaiva kwelikweli.
 
Lakini baada ya kuvibadilisha matumizi vyuo hivyo watu, hasa vijana, wakaanza kuingia CCM kwa kila mmoja kutumia mbinu za kuzaliwa kujionesha kuwa anakifia chama! Bila kuelewa namna ya kuzilinda itikadi pamoja na sera za chama, sanasana yakaanza kutumika mabavu katika kuonesha kuwa CCM iko imara.
 
Tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi, ambapo vijana wengi wabunifu waliamua kuingia upande wa pili, upande wa upinzani, ikaonekana kwamba wale wa chama tawala hawana lolote jipya kwa vile wote wanatumia ubunifi wa kujitegemea bila uweledi, ndipo chama tawala kikaamua kuegemea kwenye nguvu za dola ili zikisaidie kukiweka juu ya nguvu za upinzani.
 
Nakumbuka mwaka 1992, kabla Baba wa Taifa hajang’atuka kwenye uenyekiti wa chama hicho, aliwauliza vijana wa CCM kwenye mkutano wao mkuu mjini Mwanza,  kama wako imara kiasi cha kutouhofu upinzani, wote wakasema wako imara. Akasema basi tuache vyama vya upinzani vije, wote wakasema hapana! Hiyo hapana ilikuwa na maana kwamba hawakuwa tayari kupambana na vyama vya upinzani.
 
Kuishi kwa kutegemea nguvu za dola ni jambo lisilo la kheri hata kidogo kwenye jamii. Nguvu za kitu chochote zinatakiwa zijisimamie zenyewe, hata uzuri wa kitu unatakiwa ujioneshe na kujitangaza wenyewe katika kuwavutia wanaoutamani. Zaidi ya hapo hakuna chochote, ni kulazimishana tu.
 
Ieleweke kwamba inapojitokeza nguvu ya ziada kukitangaza kinachodai ni kizuri na kina nguvu inaondoa maana yote ya nguvu na uzuri kinavyodai kuwanavyo kitu husika.
 
Maana tabia ya asili ya mwanadamu ni ya kujionea na kukipenda kitu bila ushawishi wa kulazimishwa. Mwanadamu akilazimishwa kukipenda au kukiogopa kitu tayari anakuwa amejengewa chuki dhidi ya kitu husika. Sababu kuna usemi wa kwamba farasi anaweza kulazimishwa kwenda kisimani lakini hawezi kulazimishwa kunywa maji.
 
Sasa hivi tunaona jinsi ambavyo nguvu za ziada zinavyotumika dhidi ya upinzani pengine katika jitihada za kutaka kuutokomeza. Jambo la kushangaza ni kwamba watawala wa nchi wanaotokana na CCM hawataki kuyakumbuka yaliyofanywa na makaburu kiasi cha kuupandisha chati upinzani nchini Afrika Kusini.
 
Kusema ukweli bila ya makaburu kuubana upinzani kwa woga uliopitiliza kiasi cha kuzivuta hisia za jumuiya ya kimataifa, si ajabu makaburu hao wangekuwa bado wanajidai nchini mle hata kwa sasa. Kumbe woga wao wa kutumia mabavu kupita kiasi dhidi ya wazalendo, wapinzani, kikawa kiama chao!
 
Kwahiyo hata hapa kwetu inaonesha kwamba mikakati ya serikali ya kuvuruga mipango halali ya upinzani kwa lengo la kuyalinda maslahi ya chama tawala, CCM, ni kama kuyahatarisha. CCM ilipaswa kuyalinda masilahi yake yenyewe kwa kutenda yenye kuushawishi umma kama unavyofanya upinzani.
 
Upinzani unajinadi kwa kueneza sera zake bila mabavu wala vitisho vya aina yoyote na unakubalika. Ni kipi kinaishinda CCM kiasi cha kuifanya iegemee tu kwenye mabavu na vitisho vya nguvu za dola ikivigeuza mhimili pekee wa uhai wake?
 
Ikifikia wakati mhimili huo ukashindwa kufanya kazi kwa uchovu, kweli chama hicho kitaendelea kuwepo? Maana tumeona vyama vilivyotegemea mbeleko jinsi vilivyoshindwa kuyamudumu maisha nje ya mbeleko.
 
Nchini Romania kwa mfano, Chama cha Kikomunisiti (RCP) chini ya kiongozi wake,  Dikteta Nicolae Ceausescu, kilitegemea nguvu za dola kujiendesha. Lakini mbeleko hiyo ilipochanika ukawa ndio mwisho wa chama hicho huku dikteta huyo akiwa rais wa mwisho wa kikomunisiti.
 
Mabavu yake yaliyopitiliza yakazaa kiama cha utawala wake na chama chake, ikazaliwa Romania mpya!
 
Kwa mantiki hiyo ni wazi kwamba haya yanayofanyika nchini kwa sasa kwa upande wa siasa sitashangaa kwamba  CCM inakikaribisha kiama chake vile vile.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Prudence Karugendo, anaishi jijini Dar es Salaama na anapatikana kwa simu nambari +255 784 989 512 au kwa anwani ya barua-pepe  prudencekarugendo@yahoo.com.
About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.