Kifo cha mwanafunzi Pemba kisitumike kuadhibu kisiwa kizima kielimu

Nianze makala yangu kwa kuwapa pole wazazi wa mtoto aliyepatwa na faradhi ya kifo ambacho kinaelezwa kusababishwa na adhabu ya kupitiliza kutoka kwa walimu wake kwa kosa linalodaiwa la kuiba solatepu au gundi ya karatasi ambayo hutumika kufungashia au kugandishia vitu mbalimbali vyenye asili ya karatasi. Hakika katika jamii yetu ya Kipemba ambayo inaishi kwenye kisiwa chetu, ni jambo la huzuni na lisilo la kawaida kupata tokea na nitaeleza kwa uchache.

Niseme kwamba adhabu ya viboko ni miongoni mwa adhabu kongwe kupata kuwepo na inayoendelea kuwepo. Hii ni adhabu iliyozoweleka na kukubalika tangu enzi na enzi na linapohusika suala la elimu na malezi, bakora ni moja miongoni mwa nyenzo ambazo hutumika sana kwenye jamii ya Kipemba kwenye suala la kuadabisha. Kwangu si geni, kwani nimekutana nalo nikiwa mdogo sana wa kuanza alifu, bee, tee kwenye madrasa mahali ambapo kwa mujibu wa jamii yetu, ndio mahali pa mwanzo kwa mtoto kuanza dunia ya kusaka elimu.

Ni humu ambamo mbali ya kunikuta mimi, pia nilishuhudia wenzangu wakipigwa bakora huku wakiwa wamefungwa kwenye viguzo au shina la mnazi. Ni humu ambamo tulifunzwa kilimo kupitia kwenda kulima kwenye shamba la mwalimu wetu wa madrasa kila Alkhamis. Ni humu ambamo tulifunzwa kuheshimu wakubwa na kuwapokea mizigo yao tunapokutana nao njiani. Ndimo tulimofunzwa kuhudumia misikiti kwa kujaza maji ya kuweka udhu pamoja na usafi wa ndani na nje. Ndimo tulimofunzwa mapenzi na huruma kwa wazazi wetu. Lakini kubwa, ni humu ambamo tulifunzwa kusaidia sana wazazi wetu kwenye majukumu mbalimbali ya kifamilia.

Na Ahmad Abu Faris

Je, ni nani aliyezaliwa miaka ya ’70 ambaye kapitia madrassa na leo eti hajuwi kulima au hakuwahi kulima kwenye shamba la mwalimu wake?

Mfumo huu ulikuwa mtambuka. Kwani hali hii haikuishia madrassa pekee, bali uliendelea hadi kwenye maskuli. Wakati nikianza darasa la kwanza kisiwani Pemba, nilishuhudia shamba kubwa la shule ambalo lilikuwa likilimwa na kuhudumiwa na wanafunzi. Kupitiya mashamba haya, walimu waliweza kufaidika kwa kupata chakula pamoja na kuwesha upatikanaji wa pesa kupitia mauzo ya mazao mbalimbali yaliyotokana na nguvu za wanafunzi. Hapa mtoto wa leo anaweza kuuliza, kwani tulipelekwa skuli kwenda kusoma au kulima? Hapana, maana ya skuli ni pamoja na kumjengea mwanafunzi uwezo wa kumudu mazingira yaliy mzunguka likiwemo suala la kilimo, ambalo kwa jamii ya Kipemba ndicho chanzo kikuu cha chakula kiendacho tumboni kila uchao.

Pamoja na kujengwa kupitia niliyoyaeleza, bakora na adhabu nyingine vilikuwa sehemu ya maisha yetu kwenye maskuli. Wapo ambao walichukia kusoma kutokana na kukithiri kwa bakora. Wapo ambao walipigana na walimu kutokana na kukithiri kipigo dhidi yao. Wapo ambao waliwavizia walimu hao na kuwapopowa mawe njiani kutokana na kuwachukia kwa bakora kali walizokuwa wakiwachapa. Binafsi nikiri kwamba, nilimchukia sana mwalimu wangu wa somo la dini kutokana na mkono wake kuwa mwepesi kuchapa wanafunzi. Lakini huwezi amini kwamba mwalimu huyu niliyemchukia, alikuwa baba yangu mdogo au Wapemba huita Ammi. Jee, kweli Ammi yangu, yaani mdogo wa baba yangu, alikuwa na dhamira mbaya dhidi yangu?

Jambo moja lazima nikiri kwamba wanafunzi wakorofi tulikuwepo, wapo na wataendelea kuwepo. Lakini pia walimu wenye mkono mwepesi kwenye kupiga walikuwepo, wapo na wataendelea kuwepo. Hizi ni khulka za kimaumbile ambazo kwa mujibu wa kanuni zetu haziwezi kuondoka. Na iwapo tukijaribu kuziondosha, madhara makubwa ya kimaadili yanaweza kuja kutukumba baadaye. Nalisema hili kwa vile adhabu za viboko ni miongoni mwa adhabu ambazo zipo kidini na ndio sababu kuna muda hata wake zetu vipenzi tunatakiwa kuwachapa bakora kwa kufuata utaratibu maalumu pindi wanapokithirisha utovu wa adabu. Je, itakuwaje kwa watoto ambao kila uchao wanamezwa na majanga mapya ya kidunia? Kosa sio kuadabisha, bali kukithirisha adhabu. Kwamba adhabu apewayo mtoto isilingane na adhabu apewayo mkubwa.

Niweke wazi kwamba kilichotokea kwenye skuli hii ya Laurent International kisiwani Pemba hakifurahaishi wala kukubalika. Ni kama kupakia tani kumi kwenye gari ya tani moja au kupakia mzigo mkubwa kwenye gari mbovu. Hapo lazima maharibiko yatokee na yametokea kama wote tunavyoshuhudia.

Binafsi yangu ni mzazi na mtu mwenye kuitambuwa skuli hii. Sikutarajia kuja kusikia kwamba ndani ya skuli kuna mwanafunzi kafa kutokana na adhabu kubwa aliyopewa na mwalimu wake. Hakika hili ni tukio baya na hakuna mzazi au muungwana mwenye kulikubali.

Hata hivyo, kuna kitu ambacho tunapaswa kukitazama kwa jicho la aina yake. Kwamba ndani ya kisiwa cha Pemba, shule hii ni miongoni mwa mashule machache au pekee ambayo inabeba matumaini ya watu wenye kipato cha wastani wenye kujuwa umuhimu wa elimu. Ni skuli hii pekee ambayo ina basi la kubeba wanafunzi kuanzia Konde, Tumbe, Sizini, Micheweni, Wingwi, Kiungoni, Shengejuu, Chwale, Mchangamdogo, Kiuyu hadi ilipo, Ole Kianga.

Kwa mtu asiyejuwa mitaa na vichochoro vya kisiwa cha Pemba, anaweza asipate picha sahihi ya umbali toka Konde hadi Ole Kianga, ila itoshe kusema kwamba ni umbali mrefu mno ambao hakuna skuli nyingine yoyote katika kisiwa cha Pemba inayokusanya wanafunzi kutoka umbali kama huo. Je, kwanini skuli hii wazazi pamoja na ugumu wa maisha ya Pemba, wakubali kudunduliza na kutowa watoto wao wadogo alfajiri kubwa toka Konde hadi Ole Kianga?

Jibu ni kwamba Laurent International ni skuli inayotowa elimu bora zaidi ya skuli nyingi kisiwani Pemba. Ni skuli ambayo ukimtazama mwanafunzi wake, unaiona tofauti kubwa baina yake na skuli nyingine ambazo zimekizunguka kisiwa hicho. Kuanzia mavazi, elimu na hata mandhari iliozunguka skuli hii, ipo tofauti kubwa sana. Kwa wale wasiojuwa, Laurent International ndio skuli pekee binafsi ambayo inakusanya wanafunzi wa kutwa toka mikoa miwili ya kisiwa cha Pemba, yaani mkoa wa kusini wenye wilaya mbili za Mkoani na Chake Chake na ule wa kaskazini wenye wilaya za Wete na Micheweni. Je, ni busara kuifungia skuli ya aina hii kwa kosa la mwalimu mmoja au wawili?

Kwangu mimi kilichofanyika ni adhabu ya jumla kwa wazazi, watoto wao wanaosoma hapa, walimu, madereva na wamiliki wa magari ambao wamepata fursa ya ajira kupeleka na kurudisha wanafunzi makwao. Jee, hilo ni sahihi?

Tayari serikali imeshatowa uamuzi wa kuifunga skuli hii, lakini je, kuifunga ndio uamuzi sahihi kwa ajali iliyotokea? Kuifunga mushaifunga kwa vile ni suala la kun-faya-kun, lakini pia mutueleze ni wapi mutawapeleka mamia ya wanafunzi wengine ambao wanasoma kwenye shule hii ambayo mfumo wake wa usomeshaji ni tofauti sana na ule wa skuli nyingi tusomazo kina sisi. Kwamba kina sisi mwanafunzi hufeli skuli kabla hajamaliza iyo skuli yenyewe! Yuko hovyo na haulizwi! Mwalimu hana akitiliacho mkazo zaidi ya kusisitiza wanafunzi kuja na makuti! Ndio, si halipwi vizuri, afanye nini kumbe!?

Katika maisha yetu, lazima tuweke akilini kwamba skuli ni mahala penye kukusanya walimu na wanafunzi wenye khulka na tabia zenye kutofautiana. Kama eneo lenye mkusanyiko wa binadamu wasio na ukamilifu, ndani yake hawatokosekana walimu wakorofi, mafedhuli, viburi na kila aina ya sifa mbaya. Lakini pia hawatokosekana wale karimu na rahim. Ndio maumbile yetu. Lakini pia hawatokosekana wanafunzi wakorofi wenye tabia mbaya sambamba na wale wenye tabia njema. Haya ndio maumbile yetu.

Muda hauruhusu lakini kubwa niseme kwamba kuifunga skuli ya Laurent International kwa ajali iliyotokea si uamuzi wenye kuzingatia maslahi mapana ya kijamii. Hii ni adhabu ya jumla kwa wanafunzi, wazazi, walimu na jamii iliyozunguka skuli hii. Kwangu hii ni sawa na kosa kufanya mmoja, lakini bakora wakapigwa elfu moja. Hii ni skuli ambayo imekusanya vipaji vya sehemu tofauti. Linapotokea tatizo, unapaswa kuleta suluhisho na sio kuumba tatizo jingine. Kuifunga skuli hii kumeongeza tatizo badala ya kuliondowa. Fanyeni tafakuri upya.

Nimalizie kwa mara nyengine tena kwa kutoa pole kwa wazazi wa mtoto aliyeteswa hadi kusababishiwa madhara yaliyopelekea kuchukuwa uhai wake. Kama mzazi, nayahisi matumaini muliojenga juu ya mtoto wenu. Najuwa si jambo rahisi kwa mnyonge wa Pemba kusomesha mtoto wake kwenye shule ya gharama kama hii. Ila kujuwa kwenu umuhimu wa elimu bora ndiko kulikowasukuma kumpeleka mtoto kwenye elimu bora zaidi. Inaumiza moyoni kwamba japokuwa nyinyi mulimuhitaji kumjengea maisha mema mwenenu, jitihada zetu waja hazishindi kudura ya Allah. Haikupangwa aendelee kuwa nasi, ingawa tulitamani sana awe nasi. Kubwa tuseme inna lillah wainna illaih rrajiun.

About Zanzibar Daima 1609 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.