CUF yaja juu viongozi wake kukamatwa

Chama cha Wananchi (CUF) kimelijia juu jeshi la polisi kwa kile kinachosema ni kukamatwa kwa viongozi wake wa Mkoa wa Pwani, katika wakati ambapo mauaji na mashambulizi ya kuvizia yanaendelea kwenye eneo hilo kwa muda mrefu sasa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, ambaye alikuwa mkoani Pwani kufuatilia hatima ya viongozi kadhaa wa chama chake ambao hadi sasa hawajuilikani walipo, ameeleza kukasirishwa kwake na namna jeshi la polisi na serikali ya mkoa huo wanavyoyachukulia maisha ya viongozi hao kirahisi.

“Tuko hapa Kibaha kwa RPC (mkuu wa polisi) wa Pwani na RC (mkuu wa mkoa) wa Pwani. RC wa Pwani ameomba tuahirishe mazungumzo yetu hadi wakamilishe shughuli nyingi zikiwemo za Mwenge wa Uhuru, imagine (fikiria)!”, ameandika Mtatiro kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Kiongozi huyo wa juu kabisa wa CUF ametoa wito kwa serikali na jeshi la polisi kuwaachia “viongozi wote wa CUF wanaoshikiliwa” kwenye kile alichokiita ‘makambi maalum’ yaliyo mkoani Dar es Salaa na Pwani, vikiwemo pia vituo vya polisi kwenye mikoa hiyo, “wakiwahusisha na mauaji yanayoendelea Kibiti, Rufiji, Mkuranga.

Kwa mujibu wa Mtatiro, katibu wa CUF katika wilaya ya Kibiti ni mmoja wa ambao wamekamatwa na polisi tangu Ijumaa iliyopita, lakini licha ya kutafutwa na ndugu zake na viongozi wenzake kwa muda wote huo, hadi sasa hajapatikana na “vyombo vya dola havisemi anashikiliwa katika kituo gani cha polisi”, amehoji.

Katika taarifa yake hiyo, Mtatiro amesema CUF inalitaka jeshi la polisi, kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na ofisi ya mkuu wa polisi “wabadilishe mbinu ya kupambana na wahalifu wanaoua raia mkoani Pwani.”

“Mbinu ya kuwatuhumu, kuwakamata na kuwatesa viongozi wa CUF haina maana, ni ya kiuonevu, kikatili, kisiasa na haitatatua tatizo la Pwani.” Amesema Mtatiro.

Miongoni mwa viongozi wa CUF wanaoshikiliwa bila taarifa zao kuwekwa hadharani ni madiwani, na wenyeviti wa vijiji na vitongoji.

Hayo yanakuja wakati kukiwa na taarifa za hivi punde kwamba mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Kati, Ikwiriri, Athuman Mtoteka, ametekwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.

Mtoteka ni kiongozi wa CUF na anadaiwa kutekwa jana kati ya saa moja na mbili usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, amethibitisha tukio hilo akisema “watu wasiojulikana walifika nyumbani kwa Mtokeka kwa miguu kisha kumchukua na kwenda naye kusikojulikana.”

Mashahidi wanasema wanaeleza kuwa waliwaona watu watano waliofika nyumbani hapo wakitembea kwa miguu kisha kumkamata na kuondoka naye.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.