HABARI

Suala la Pwani lisiachwe kwa Polisi peke yao

KINACHOENDELEA  kwa sasa katika maeneo ya mkoa wa Pwani, hasa Mkuranga, Kibiti na Rufiji, ni hali ya hatari. Sidhani kama kuna Mtanzania yeyote anayependezwa na kitu hicho au anayeweza kuona hilo ni jambo lisilomgusa au kumhusu.
 
Tanzania ni nchi inayojivunia hali ya amani na utulivu, hilo ni jambo ambalo bilashaka nchi zote zinalitamani na kulionea husuda. Machafuko tunayoyasikia katika baadhi ya nchi sio kwamba nchi hizo zinayatamani, yanajitokeza tu kwa sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo.
 
Lakini sasa haya yanayotokea moani Pwani ni kama yanaitia jeraha nchi yetu, hatupaswi kukaa kimya na kuyaangalia tu kana kwamba yanatokea nje ya mipaka ya nchi yetu. Nchi yetu ni sawa na mwili mmoja ambao ukiumia kidole cha mguu mwili mzima unashtuka, ukiumia jicho mwili mzima unashtuka, ukiumia sikio mwili mzima unashtuka nakadhalika.
 
Tutajidanganya kusema tuko kwenye amani na utulivu wakati ndugu zetu wa maeneo yanayotajwa wanapata madhara, wanajeruhiwa na wengine kuuawa na watu wasiojulikana. Maana tunaposema amani na utulivu inatakiwa tuvifaidi vitu hivyo sisi sote kama Watanzania tukiwa kama mwili mmoja.
 
Isitokee sehemu moja ya nchi ikawa na amani na utulivu huku sehemu nyingine ikiwa kwenye kasheshe kama hiyo ya Pwani halafu tuendelee kujiona tuko salama kwenye amani na utulivu.
 
Kwa kadri ninavyoona, hili sio tena suala la kulegeza msimamo kwa kuliachia tu Jeshi la Polisi kuwa ndilo lishughulike nalo kwa vile jeshi hilo ndilo linalopaswa kulinda usalama wa raia. Matukio haya ya Pwani yanajionesha yalivyovuka mipaka ya usalama wa raia.
 
Tumeshuhudia vijana wetu wa usalama wa raia wasiopungua 8 wakiteketezwa kwa pamoja katika moja ya matukio ya kinyama yanayoendelea mkoani humo. Nadhani hilo ni tukio ambalo, kama sikosei, halijawahi kutokea kabla hapa nchini yakiondolewa yale yaliyotokea wakati wa Vita ya Kagera.
 
Wakati ule, Vita ya Kagera, Tanzania ilikuwa imeingia kwenye vita kufuatia uvamizi wa kichokozi uliofanywa na nchi jirani ya Uganda iliyokuwa chini ya utawala wa kiongozi wa kijeshi aliyekuwa kama mwendawazimu, Idd Amin Dada.
 
Kwahiyo kilichofanyika ni uamuzi wa Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Nyerere wakati huo, kuliamru jeshi lake kukabiliana na uvamizi huo wa Amin. Hiyo ni kwa sababu kazi ya jeshi ni kulinda mipaka ya nchi.
 
Kwahiyo kwa matukio haya ya Pwani ambayo hatujajua mhusika ni nani, tusikae tukijiridhisha kuwa maadamu yanatokea katikati ya nchi mipaka yetu iko salama. Inawezekana maadui wakawa wamepenya kisirisiri na kuleta zaama ndani kwa ndani  wakiamini kwamba watakabiliana na polisi wakati majeshi yanaangaza tu kwenye mipaka ya nchi.
 
Kwahiyo ushauri wangu kwa Amiri Jeshi Mkuu, Dk. John Pombe Magufuli, ni wa kulichukulia suala hili kwa hasira kali. Angeyaamuru majeshi yake yote kuliingilia eneo hilo la Pwani na kisha kulichambua kama karanga ili kieleweke. Maana mpaka sasa tumeishaamini kuwa uhalifu huu unaoendelea hauwezi kuwa unafanywa na vibaka tuliowazoea ambao wanaweza kukabiliwa kiurahisi na skari polisi wa kawaida.
 
Nalisema hilo nikiwa nimetilia maanani kwamba tatizo linatakiwa kukabiliwa likiwa changa, sababu pale linapokua na kuwa kubwa zaidi litahitaji kukabiliwa na kutatuliwa kwa nguvu na gharama kubwa zaidi vilevile.
 
Tumeona katika baadhi ya nchi duniani ambako vurugu tu za wananchi zinayafanya majeshi kuingia mitaani yakiwa na zana za kivita, virafu, mizinga nakadhalika, sasa iweje sisi tuendelee kuviweka ndani vifaa hivyo vya kujihami wakati hali ikiwa tete katika sehemu ya nchi yetu?
 
Maana tumezoea kuviona vifaa vyetu hivyo kwenye maonesho ya siku za mashujaa na kuvishangilia huku tukiamini kuwa, kwa mtaji huo, tuko salama. Sasa iweje tusumbuliwe na vijitu vichache vinavyotuletea madhara makubwa kiasi hiki wakati nguvu zetu zikiwa stoo?
 
Nimeamua kumkumbusha Amiri Jeshi Mkuu kuhusu nguvu zetu tulizoziweka stoo kufuatia kauli yake ya kwamba yeye sio mtu wa kujaribiwa. Sasa kwa nini awaachie hawa wakorofi wachache wamjaribu?
 
Mtu anayekujaribu mara nyingi hutaka kuona ukali wako unafikia kiasi gani, kwahiyo ukimlegezea anazoea. Ataendelea kukujaribu mpaka yawe mazoea, lakini akithubutu mara moja ukamchapa kiboko kikali anakoma kabisa, hawezi kukujaribu tena. Sababu atakuwa ameamini kwamba ni kweli wewe hujaribiwi!
 
Nayasema hayo nikiwa nakumbuka kwamba mwanzoni mwa miaka ya 1970, baada ya Idd Amin kumpindua Obote kule Uganda, kiongozi huyo wa kijeshi alianza kuifanyia Tanzania uchokozi alipogundua kuwa Nyerere kamkaribisha Obote kama rais.
 
Kabla mapambano hayajapamba moto ukatokea usuluhuishi ambao Nyerere aliukubali, lakini Amin akabaki akiamini kwamba Tanzania hamna kitu, kwamba anaweza kuichezea jinsi atakavyo, hivyo akarudia tena mwishoni mwa miaka ya 1970. Kumbe alikuwa ameweka kidole kwenye mzinga wa nyuki, na huo ndio ukawa mwisho wake.
 
Kwahiyo haya yanayoendelea mkoani Pwani, vurugu za mara kwa mara, ambazo zimewafanya wananchi wa maeneo hayo wakose kufanya shughuli zao kwa kujiamini,  zikiambatana na mauaji ya hapa na pale, ni lazima yakomeshwe mara moja kwa kuzingatia kauli ya rais na Amiri Jeshi Mkuu ya kwamba hajaribiwi.
 
Rais Magufuli, akiwa mlinzi namba moja wa wananchi wake, hapaswi kuwalegezea hata kidogo wakorofi hao. Anapaswa atumie nguvu kubwa hata kama watu wenyewe ni vibaka tu lakini wakionesha kumjaribu kupitia kwenye mazingira hatarishi.
 
Donda hilo tunapaswa tulitibu kwa nguvu zote kabla halijageuka dondandugu. Sababu inasemwa kwamba hata mbuyu huanza kama mchicha. Tusichelee mwana kulia tukaja kulia wenyewe.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Prudence Karugendo, anapatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com na simu +255 784 989 512

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.