News Ticker

Ni kuona ama kuonya, kuonesha au kuonyesha? 


Nawaomba radhi wanaukumbi kwa kuwarudisha nyuma kwenye mazungumzo ya juzi, kuhusu haya maneno yaliyoko hapa juu. 

Nianze kwa kuungama. Katika baadhi ya nyakati hutolewa maoni hapa, ambayo nami hutamani niongeze yangu, lakini hujizuia na kujiambia niyapishe yapite. Wakati mwingine huyapisha kwa kuogopea nisije nikaonekana najifanya kuwa ni mjuvi (mjuaji) mno! Lakini mara nyingine hushindwa kujizuia.

Mwenzetu, Bwana (au ni Bibi?) Nii Adjetey, aliomba aelezwe tafauti kati ya “kuonesha” na “kuonyesha.” Wa kwanza aliyemjibu akaashiria kwa ufupi tu kwamba “kuonesha” latokana na “ona”; na “kuonyesha” latokana na “onya.” Na wenzetu wengine wawili wakafuatia kwa kutoa mifano ya matumizi ya maneno hayo, na kuelezea kwamba “ona” lina maana sawa na “tizama” (tazama); na kwamba “onya” lina maana ya kukanya/kuadibu/kukataza. Nakubaliana na hayo.

Nitakalo kuongeza ni kwamba mbali na kuwa “onya” lina maana hiyo iliyoelezwa, pia lina maana ya “onesha” – ambayo naamini ndiyo maana yake ya asili. Katika lugha ya Kiswahili kuna maneno machache ya vitenzi vilivyomalizika kwa silabi -na, ambavyo vikibadilishwa katika hali ya kusababisha, silabi hiyo ya mwisho hugeuka na kuwa -nya. 

Kwa hivyo, basi, ukinionya kitu huwa unanionesha kitu hicho. Waweza pia kumsikia mtu akisema kwamba Fulani alikuja hapa akaruonya vituko! 

Na ukiwa mgonjwa, halafu ukala dawa ikakuponya, dawa hiyo huwa imekusababisha wewe kupona. 

Tukija katika mambo ya uganga, waganga wanapofanya ya kufanya ili kugonya k’oma, huwa wanaisababisha mizimu kugona, yaani kuilaza au kuituliza. Katika Kiswahili cha kale – na hadi leo katika lugha za Mijikenda – neno “kugona” lina maana ya “kulala.” Ndipo kwa wale walio na mke zaidi ya mmoja hutakiwa wagawanye ugoni kwa siku sawa sawa – ukilala siku mbili kwa mke wa kwanza, basi na kwa mke wa pili iwe ni siku mbili pia. Na kutokana na neno “kugona” ndipo tukapata neno “ngono”, ambalo twalijua maana yake.

Miongoni mwa maneno yanayofuata kanuni hiyo ni “kana” (=kataa; kutokubali). Kwa hivyo, unapomkanya mtoto huwa unamkataza asifanye jambo fulani, aghlabu jambo ovu au la hatari. Pia neno “dangana” ((= kutokuwa na hakika ya jambo, au kutoujua ukweli wa jambo, au kutatizika na jambo). Kwa hivyo, unapomdanganya mtu huwa unamsababisha asiujue ukweli wa jambo fulani.

Basi, kwa ufupi, neno “onya” lina maana ya kusababisha mtu kuona, kutahadharisha, kukataza, kuadibu. Na “kuonesha” na “kuonyesha”, au “maonesho” na “maonyesho”, hiyo ni mibadala; hakuna tafauti ya maana. 

Baadaye leo, inshaAllah, nitajaribu kutoa maoni yangu kuhusu neno “tasiliti”, lililoulizwa maana yake.

TANBIHI: Imeandikwa na Mwalimu Abdilatif Abdalla, ambaye amekuwa mwalimu wa lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu mbali mbali duniani. 

About Zanzibar Daima (1509 Articles)
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s