Kwa mtaji huu, tutaendelea kuibiwa tu

Nimesikia mmoja wa wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Andrew Chenge, anajitapa kwa kusema hawezi kufungwa kwa sababu alichokifunga (kusaini mikataba ya ovyo) kilikuwa na baraka zote za mteule wake.

Marufuku ya marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kutojadiliwa kwenye kashfa za mikataba huyo ya ovyo, ndio leo imepelekea gazeti la MAWIO kufungiwa kwa muda wa miaka miwili.

Kimsingi, mambo yote mawili ni tafsiri kuwa huenda hatujachoka kuibiwa au tumechoka lakini hatujui ni kitu gani tufanye ili kuondokana na zahama hiyo ambayo imekuwa ikiturudisha nyuma kama taifa.

Chenge anaposema hawezi kufungwa anajua anachokizungumza. Anajua katiba ya nchi imempa rais mamlaka makubwa hata ya kuweza kutuibia kwa kushirikiana na washirika wake na asichukuliwe hatua yoyote. Hivyo njia pekee ya kupona kwake ni kumhusisha aliyemtuma. 

Marufuku ya kutowajadili Kikwete na Mkapa ni batili, kwani licha ya kwamba katiba yetu kupitia ibara ya 18 imetoa haki ya kila mtu kuwa huru kutoa maoni yake, lakini pia hakuna sheria yoyote inayosema kumjadili kiongozi wa nchi mstaafu ni kosa la jinai. Hakuna.

Wabunge wamekatazwa kujadili kwa sababu wakifanya hivyo watashughulikiwa na spika au mamlaka nyingine ndani ya muhimili huo licha ya kuwa hakuna kanuni inayowakataza kufanya hivyo.

MAWIO na magazeti mengine yatashughulikiwa kwa sababu anayeamua yafungwe au yaendelee ni waziri ambaye ni sehemu ya serikali iliyotoa marufuku hiyo.

Lakini mimi sitanyamaza katika kutumia haki yangu ya msingi ya kutoa maoni yangu juu ya chanzo cha wizi wa rasilimali za nchi yangu. Ninaamini kabisa niko Tanzania ambayo ni mali ya Watanzania wote na sio familia ya mtu.

Msimamo wangu katika jambo hili ni kuwa rais mstaafu anapowekewa ulinzi wa kutojadiliwa (achilia mbali kufikishwa mahakamani hata kwa makosa aliyofanya kabla ya kuwa rais) ni jambo linalotuma ujumbe mbaya kwa rais aliyepo madarakani na watakaofuatia. Tutaendelea kuibiwa. Tutaibiwa kweli kweli. Kwa nini? Kwa sababu wakituibia hatutakuwa na haki ya kuwawajibisha. Hata wateule wao watatumia ulinzi huo kujilinda kama anavyofanya Chenge.

Hii habari ya kukataza watu wasijadili uhusika wa viongozi wetu wastaafu ni habari ya ajabu sana katikati ya kile kinachoitwa “vita dhidi ya rasilimali”. Tuondoe kinga hizi then tutakuwa tumewafanya viongozi kutotumia vibaya madaraka yao pindi wanapochaguliwa kuwa viongozi wetu.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Bob Wangwe kwenye ukurasa wake wa Facebook tarehe 15 Juni 2017

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.