Tuhuma za dhuluma dhidi ya Mzee Gora: Jibu la Ally Saleh kwa Waziri Rashid 

Salam. Mimi naitwa Ally Saleh. Natumai utakuwa na muda wa kuyasoma maelezo haya ili, kwanza, ujielimishe juu ya suala la Mzee Haji Gora na, pili, upate usikie upande wa pili wa shillingi

Bahati mbaya umeeneza shutuma kwa mtizamo hasi bila ya kusikiliza upande mwengine. Lakini mimi nimekusamehe kwa sababu najua akili yako iliongozwa na siasa.

Mimi nimemjua Mzee Haji Gora zaidi ya miaka 25 na nia ya kufanya kazi naye imekuwepo mara kadhaa katika nyingi ya kazi zake. 

Moja katika kazi yake aliyonikabudhi na ambayo bado ninayo na nina nia ya kuichapisha ni ile inayoitwa “Moto wa Tumbatu”, ambayo ni utenzi ulioandikwa 1964 na haujachapishwa hadi leo.

Ally Saleh 

Najua Mzee Haji Gora amechapisha kazi kadhaa lakini nyingi yake hazijauzika na kwa hivyo mapato anayopata ni madogo na kwa hivyo hahisi faida.
Kazi za kumpatia pesa ni vitabu vilivyoingia katika mtaala wa Kidato cha Nne huko Bara. Huko ndiko kwa kuuliza.

Soma vizuri sura ya mwisho ya hicho kitabu changu.

Kwa hakika, kama kuna kazi hazijamfaa pengine zipo ila sio hii. Maana hii ndio kwanza imechapishwa na si haki kuanza kuihukumu kwa sababu uuzaji wa vitabu sio kama sahani ya maandazi, kwamba itauzwa siku hiyo hiyo.

Nilianza kufanya kazi hii zaidi miaka ya minne nyuma. Mzee Haji Gora alikuwa ana muundo wa rasimj ambayo alishaitembeza kwingi na sie tunayemjua tunaijua tabia yake hiyo. 


Nilikaa nayo kwa zaidi ya miezi sita tukikutana nyumbani mara kadhaa nikimrekodi mtiriko mzima wa maisha yake na kuunda muundo kama ilivyo sasa kwenye kitabu changu, ambapo pia nikafanya tafiti kadhaa.

Nimekaa na kitabu kutafuta mchapishaji mpaka mwaka jana ulipoundwa Wakfu wa Emerson kwa ajili ya Zanzibar na mimi kuchaguliwa kuwa mjumbe wa bodi yake. Niliwashawishi wajumbe wenzangu kwamba tuchapishe vitabu viwili – hicho cha maisha yake na pia Moto wa Tumbatu, ila bodi ilikubali kimoja.

Nakala ya kwanza kule kwenye kampuni ya uchapishaji ya Multi Colors ikaharibika yote na bodi ikapoteza shilingi milioni 7. Lakini tu katoa tena shilingi milioni 6.5 kuchapisha Dar es Salaam nakala 3,000. Yote haya ni kwa sababu tukitaka maisha ya Mzee Haji Gora yaandikwe mwenyewe akiwa hai.


Nakala zilizoharibika wamepewa Wizara ya Elimu kusambaza. Na maana ya kuharibika ni kukosa sura ya mwisho. 
Nakala zote za chapisho la pili zinadhibitiwa Wakfu wa Emerson na mimi nina nakala moja tu yangu nyumbani kwangu. 

Bodi imepeleka kwa mauzo katika duka la Masomo Bookshop la Mjini Zanzibar na pia duka jengine moja la jijini Dar es Salaam, ambapo mauzo yanashughulikiwa na mwenyekiti wetu, Said el Gheithy. 

Wakfu umekubali kutokata hata senti ya uchapishaji ili afaidike Mzee Haji Gora. Hili si jambo la kawaida katika wakati ambapo mfuko umetumia shilingi milioni 13.5. 
Mimi nimesema nasamehe chochote kwenye umri wote wa Mzee Haji Gora. Kawaida kama mwandishi nina haki ya kupata baina ya asilimia 10 hadi 20 ya mauzo.
Kwa maana hiyo, Mzee Haji Gora anapata shilingi 20,000 kamili kwa kila kitabu kinachouzwa, jambo ambalo halipo duniani kote, ila kwa sababu tumekubali kumchangia.
Kuhusu hatimiliki ya kitabu 

Kawaida, kitabu ni cha mwandishi. Hiki si kitabu chake japo kimeandikwa juu ya maisha yake. 
Kisheria, vitabu alivyoandika yeye mwenyewe ndivyo vyake na ndio kanuni ya kazi yoyote ya sanaa. Haki ya umiliki ana ni ya mchapishaji au mwandishi. 
Ikiandikwa hakimiliki maana yake ni “intellectual property” ambayo ni akili yangu mwandishi wa kitabu. Naona hilo ulikuwa hujui

Lakini Mzee Gora hakuandika kitabu hiki, bali ni muandikiwa tu na bado anapata asilimia 100 ya mauzo yote. Hakika hii ni ‘bonus’ kubwa. 

Juu ya yote, mauzo hayo anapewa kila baada ya nakala chache kwa sababu ya mahitaji na risiti zipo zote kila alichopewa.

Kama ulikuwa hujui pia kitabu chake tumekichapa kwenye mtandao wa amazon.com kupitia kampuni ya Zanzibar Daima Publishing na vipesa tunadunduliza, lakini akitaka hata kesho atapewa.

Kama kweli serikali inataka kusaidia 

Sasa kama serikali inataka imsaidie, basi ni kwa moja kati ya mawili haya: ama izinunuwe nakala zote ili apate kama shilingi milioni 60 kwa mpigo, au ishawishe kitabu hiki kiingie kwenye mtaala, hasa wa Bara, na kwa maana hiyo ataweza kupata hadi shilingi milioni 100 mara moja. Wallahi atakuwa ni milionea.

Watoto wake wameelezwa yote lakini hawataki kufahamu kwa sababu wanatumia fursa ya uzee wake kumzonga ili wafaidike. Hii ni kama ile kesi ya Marehemu Bi Kidude.

Bi Kidude alifanywa ng’ombe wa maziwa na pia hivyo hivyo ni kwa Mzee Haji Gora. Watu hawafanyi kazi ila wanataka kumnyonya mzee.

Mimi niliandika kitabu cha Maisha ya Bi Kidude na sikusikia amepewa kitu maama yake sie muandishi wa hicho kitabu.
Tumsaidie Mzee Gora kwa nia thabiti

Huku mjini, sisi tunatafuta kila njia ya kumhifadhi Mzee Haji Gora kama mimi binafsi na kama kundi. Mfano mwaka juzi watu walichapisha kitabu cha mashairi yake 12 yaliyotafsiriwa Kiingereza na asilimia 100 akapewa yeye mwenyewe bila hata kukatwa gharama za uchapishaji. 
Hiyo ndiyo hadithi ya upande wa pili na msimamo wangu wa asilimia 100 ya mauzo kadri ya uhai wake na asilimia 100 ya Wakfu wa Emerson pia upo pale pale.

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

2 Comments

  1. Mimi binafsi nilishtuka kusikia Ally Saleh anatuhumiwa kwa hayo. Nilicheka. Ally Saleh ninayemjua mimi siamini kama anaweza kuchukua hata cent 5 ya Mzee Haji Gora; lakini ni kawaida ya Zanzibar hufanyi jema ikawa kheri, siku zote inaishia na ubaya. Ukifanya ubaya, kama wanavyofanya wengine, ndio unaishia na kuwa na sifa kem kem. Kwa ufupi, mimi ninayemjua Mzee Haji Gora, na Sheikh Ally Saleh, naona Ally Saleh ‘anamlea’ Mzee wake.Mimi namuona hodari sana Ally Saleh anaweza kujibebesha mambo mengi ya kijamii /baadi yetu tunazo ideas nyingi lakini tunarudi nyuma kutokana na mazingira yenyewe ya Zenj.

  2. Wengi wetu tunamjua mzee Haji Gora, na tunajuana na kufanya baadhi ya kazi nae. Ally Saleh pia tunajua vyema kabisa. Tokea lini SMZ kufikiria kuwatunza wazee wetu wenye vipaji vya namna hii? Vyereje waibuke leo na tuhuma zisizo na mashiko yyt? Kujiaibisha tuuu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.