Mashirika ya haki za binaadamu yalaani kufungiwa Mawio 

Mashirika ya haki za binaadamu na watetezi wa uhuru wa habari nchini Tanzania yamelaani vikali na kwa kauli moja hatua ya serikali ya Rais John Magufuli kulifungia gazeti la Mawio kwa madai ya kukiuka agizo la kutowaandika marais wastaafu kwenye kashfa ya mikataba ya ovyo inayoliibia taifa matrilioni ya pesa kupitia sekta ya madini. 

Katika tamko lao la pamoja lililotolewa leo (Juni 18), mashirika hayo yamesema kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania, Watanzania wana uhuru wa kutoa maoni na kupashana habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao. 

“Kitendo cha kuzuia Watanzania au vyombo vya habari visichapishe picha za viongozi wastaafu, hasa katika mijadala ya kitaifa ambayo inahusu mambo yaliyotekea wakiwa madarakani, ni kuwaziba Watanzania midomo katika sakata la vita dhidi ya wizi wa madini Tanzania,” inasema sehemu ya tamko hilo.

Soma tamko kamili hapo chini: 


TAMKO LA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MAWIO NA HALI YA UHURU WA HABARI NCHINI

UTANGULIZI

Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Umoja wa Vilabu vya Habari Tanzania (UTPC) kwa pamoja tunalaani vikali kufungiwa kwa Gazeti la Mawio na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe Juni 15,  2017. Gazeti limepigwa marufuku kuchapishwa na kuwekwa katika mzunguko kwa miaka miwili. 

MAKOSA WANAYOTUHUMIWA KUFANYA


Gazeti la Mawio limefungiwa siku ya tarehe 15 Juni 2017, baada ya kutoa toleo lake lenye namba 196 la tarehe 15-21 Juni, 2017. Waziri ametumia sheria mpya ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016 kulifungia gazeti la Mawio kwa madai ya kukiukwa vifungu vya sheria hiyo na “Agizo la Mhe Rais” kuhusu kutowahusisha Marais wastaafu na sakata la uporaji wa rasilimali madini nchini.

Gazeti hili limeshutumiwa kutenda makosa mawili; kosa la kwanza chini ya kifungu cha 50 na 59  cha Sheria ya Huduma za Habari Namba 2 ya 2016 na kosa la pili kukiuka “Agizo la Rais laTarehe 14/6/2017…” kama ifuatavyo:

(i) Kuchapisha Picha za Marais Wastaafu

Waziri alidai kuwa, gazeti hilo limechapisha picha na majina ya marais waliopita kwa kuwahusisha na kashfa ya rushwa katika mikataba ya madini kati ya Serikali na wawekezaji.

Waziri anasema kuwa hawakufurahishwa na picha za marais wastaafu ambazo ziliwekwa kwenye ukurasa wa mbele.

(ii) Kuchapisha Makala Kuhusu Uporaji wa Madini kinyume na Agizo la Rais

Kosa la pili ni kuchapisha makala ambayo ilichapishwa katika ukurasa wa 12 wa gazeti hilo kinyume na “Agizo la Rais la tarehe 14/6/2017 linalowataka Watanzania kuacha kuwataja au kuwahusisha marais wastaafu na sakata la upoteaji wa rasilimali madini” . Makala hiyo ni andiko lililosheheni historia ya jinsi viongozi mbalimbali walivyoshiriki katika usimamizi wa uwekezaji katika sekta ya raslimali madini. 

UCHAMBUZI KUHUSU TUHUMA HIZI NA HATUA YA KULIFUNGIA GAZETI

Itambulike kuwa hii si mara ya kwanza kwa magazeti na vyombo vya habari kufungiwa na Waziri katika nchi yetu kwa kutumia sheria mbalimbali kanda miezi, hasa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyofutwa mwaka 2016 na kuridhiwa na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016. Magazeti kadhaa yalifungiwa katika siku za nyuma, ikiwemo Mwananchi, Mawio, Mwanahalisi na Mtanzania. Kwa upande wa Gazeti la Mawio hii ni mara ya pili kusimamishwa. Januari 15, 2016 gazeti hili lilipigwa marufuku kabisa kupitia Tangazo la Serikali (GN) Namba 55 la 2016. Hata hivyo, gazeti hilo liliishtaki Serikali kwa mafanikio katika kesi Na. 15 ya 2016 na hatimaye likaweza kuendelea na machapisho yake.

Itambulike  kuwa kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga utaratibu wa kisheria wa kumpa Waziri mamlaka makubwa katika sekta ya habari. Sheria iliyopita na ya sasa hazina tofauti yoyote hasa katika mamlaka ya Waziri kulifungia gazeti pekee na kwa makosa atakayoyaona yeye ni kinyume na maslahi ya umma. Sheria hii mpya imeendelea kumfanya Waziri awe Mhariri Mkuu, Mlalamikaji, Mpelelezi, Mwendesha Mashtaka na Hakimu kwa wakati mmoja.  

Kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari imetumika kulifungia Mawio kwa madai kuwa kuchapisha picha za viongozi wastaafu ni kinyume na maslahi ya umma. Kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania, Watanzania wana uhuru wa kutoa maoni na kupashana habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao. Kitendo cha kuzuia Watanzania au vyombo vya habari visichapishe picha za viongozi wastaafu, hasa katika mijadala ya kitaifa ambayo inahusu mambo yaliyotekea wakiwa madarakani, ni kuwaziba Watanzania midomo katika sakata la vita dhidi ya wizi wa madini Tanzania.

Katika kosa la pili, gazeti hilo lilitumia makala ya mbunge mmoja na mtaalamu wa sheria za madini nchini yenye maelezo juu ya mambo muhimu katika kumsaidia Mhe. Rais katika vita ya uporaji wa rasilimali madini.  

Vyombo vya habari, kama watu wengine, wana haki ya kutoa habari kama wanadhani ina maslahi kwa umma ilimradi hazikiuki sheria. 

Tumeshangazwa kuona waziri ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ametumia Agizo la Rais kama sheria, kitendo ambacho ni hatari kwa mustakabali wa taifa kama kila kitakachoagizwa na kiongozi mkuu kitachukuliwa kama ni sheria.  

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mawio, Agizo la Rais kuhusu kuzuia marais wastaafu wasitajwe au kujadiliwa kwenye sakala la madini, lilitoka wakati tayari gazeti hilo toleo la tarehe 15/6/2017 likiwa limeshachapishwa na kusambazwa kwa mawakala nchi nzima tarehe 14/6/2017, wakati ambapo ndipo Agizo la Rais lilitoka tarehe hiyo hiyo 14. 

Taarifa rasmi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali ilinukuu Kifungu cha Sheria cha 50 (a) (b) (c) (d) na (e) kuwa ndicho kilichokiukwa na gazeti la Mawio kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe. Aidha, kifungu kilichotumiwa na waziri kutoa adhabu hakiendani na kifungu kilichotamka kosa lililotendwa na gazeti la Mawio. Kwa mujibu wa kifungu kilichotumika, mamlaka yenye uwezo wa kutoa adhabu ni mahakama baada ya kumsikiliza mtu huitwa, jambo ambalo katika maamuzi ya Waziri Mwakyembe hali kufanyika, ukiachilia mbali kwamba yeye sio mahakama. 

Ikumbukwe kwamba mamlaka pekee yenye uwezo wa kutoa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mahakama kwa mujibu wa Ibara ya 107 (A) (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, waziri kutoa adhabu kama hii amekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Kifungu alichotumia kutoa adhabu hakielezi kosa lililotendwa na gazeti la Mawio na kisheria adhabu haiwezi kutolewa bila kuwepo kosa (no punishment without law, kwa Kilatini Nullum Criminem Sine Lege). Waziri ametoa adhabu kwa gazeti la Mawio bila kufuata misingi ya sheria ilhali yeye mwenyewe ni mwanasheria.

Ikumbukwe mpaka sasa kwamba kuzuia kujadili watu au juu ya masuala ambayo hayakuwekwa katika ripoti mbili za kamati za Mheshimiwa Rais  juu ya kashfa ya madini hakuondoi haki na wajibu kwa Watanzania kama ilivyoanishwa katika Katiba ya nchi kama ifuatavyo:

• Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake Ibara ya 18(a). Makala iliyochapishwa katika ukurasa wa 12 ni maoni ya mwandishi wa makala hiyo kwa mujibu wa kifungu hiki.

• Kila mtu amepewa haki wakiwemo waandishi wa habari kutafuta, kupokea na kutoa taarifa kama inavyoelezwa katika Ibara ya 18 (d) ya  Katiba. Wanahabari ni sehemu muhimu katika maendeleo ya taifa letu na wamekuwa kiungo kizuri cha utekelezaji haki hii.

• Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na shughuli muhimu kwa wananchi Ibara ya 18 (b). Suala la Madini ni tukio muhimu kwa maisha ya Mtanzania na gazeti la Mawio lilikuwa katika kufikisha taarifa mbalimbali zinazohusiana na sakata hili la madini.

• Katiba ibara ya 27 (1) imempa kila Mtanzania wajibu wa kulinda rasilimali asili za nchi. Hivyo, pamoja na kuwa kuna  ripoti mbili za kamati, bado Watanzania wengine wana wajibu wa kumsaidia Mhe. Rais katika kulinda rasilimali za nchi kama gazeti la Mawio lilivyofanya kwa kuruhusu Watanzania watoe taarifa wanazoona ni muhimu kumsaidia Rais katika sakata hili.

Tumebaini pia hakukuwa na  utaratibu mzuri wa kuwasikiliza viongozi wa Mawio, kwani Idara ya Habari iliwasiliana kwa njia isiyo rasmi na Mhariri wa Mawio bila ya kutoa barua yoyote ya kiofisi. Pamoja na kwamba hakukuwa na mawasiliano yoyote ya kiofisi zaidi ya simu, Mawio waliandika barua ya kuelezea sababu za kuchapisha gazeti lao na taarifa husika. Moja ya sababu ni kuwa gazeti lilipishana na Agizo la Rais. Maana yake Agizo liliwafikia wakati tayari gazeti limekwishachapwa na kusambazwa kwa mawakala. 

Nguvu kubwa kama hizo alipewa Waziri pia katika Sheria ya Magazeti ya 1976 na sasa imeletwa  katika Sheria ya Huduma za Habari. Waziri chini ya sheria hii mpya anafanya kazi kama mhariri mkuu, mlalamikaji, mchunguzi, mpeleka mashtaka na jaji. Kwa mfano, Kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari inasema kwamba: “Waziri atakuwa na uwezo wa kuzuia au kuweka vikwazo kwa uchapishaji wa maudhui yoyote ambayo yanahatarisha usalama wa taifa au usalama wa umma.” Hiki ni kipengele pekee ambacho Waziri anaweza kutumia kupiga marufuku gazeti. Kifungu hicho kinampa nguvu kubwa mno mtu moja kuamua makosa yanayofanywa chini ya Sheria ya Huduma za Habari na kuwa muamuzi wa makosa hayo pia. Ni kinyume na misingi ya sheria za utawala bora.

Licha ya ukweli kwamba sheria hii ni mbaya sana na ni hatari kwa uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari kwa ujumla, tunaona hakuna uwezekano wowote kwamba machapisho hayo yameweza kuuweka “usalama wa taifa au usalama wa umma hatarini”. Badala yake, uchapishaji wa picha za viongozi wastaafu wa nchi na makala iliyoundwa vizuri ikionyesha namna ambavyo sheria mbaya katika sekta ya madini zilipitishwa katika nchi yetu kipindi cha uongozi wao inaweza kutumika vyema na serikali, Bunge na wadau wengine ili kupata ufumbuzi sahihi katika usimamizi wa rasilimali zetu.

Kufungiwa kwa Mawio si tu kumekiuka sheria zetu kuhusu uhuru wa kujieleza, lakini pia kimataifa kumevunja Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na Mkataba wa Afrika ambao Tanzania imeridhia. Kwa uzuiaji huu, idadi kubwa ya Watanzania wamenyimwa haki ya kupata taarifa na hivyo inapunguza kiwango cha uwazi kwa viongozi wa serikali kwa sababu waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla ni waangalizi  wa utendaji wa serikali.

Kwa ujumla, hatukuona sababu kubwa ya kulifungia gazeti hilo kwani tuhuma zote zilikuwa zinazungumzika lakini katika njia ambayo ingehusisha makundi kadhaa katika sekta ya habari badala ya kumwachia Waziri awe mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mwamuzi kwa wakati mmoja.

WITO NA USHAURI WETU 

• Serikali itengue uamuzi wake wa kulifungia gazeti la Mawio kwani umeenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 ambayo kimsingi haimpi mamlaka waziri kutoa adhabu aliyoitoa.

• Juhudi za serikali katika kuhakikisha uchumi unakua na juhudi za kupambana na rushwa lazima ziende sambamba na viongozi kuwa wavumilivu na kukubali kukosolewa kwa mambo ambayo ni muhimu katika kufikia malengo na matarajio hayo.

•  Ili kutimiza nia ya Rais wetu ya dhati katika kukabiliana na watuhumiwa wote wa kashfa za madini, yampasa kuruhusu wananchi kuwajadili kwa uhuru wale wote wanaotuhumiwa kuhusika bila kujali kwamba wametajwa katika taarifa za Kamati au la.

• Tunamshauri Rais atambue kuwa hiki kizuri anachokifanya leo katika kulinda rasilimali asili, kinaweza kuwafanya wananchi kwa nia nzuri kabisa kuhoji viongozi wa zamani walifanya nini kwa kuwa walikuwa na jukumu kubwa katika kushawishi aina ya usimamizi wa rasilimali wakati wa uongozi wao. 

• Ikumbukwe kwamba vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na magazeti, hufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Katiba inasema wazi chini ya Ibara ya 18 kwamba Watanzania wote wana haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari na maoni kwa njia yoyote.

• Kwamba serikali inapaswa kuondoa marufuku yake dhidi ya Mawio kuzingatia kwamba sheria hii inakiuka misingi ya kidemokrasia na inajenga picha hasi ya nchi yetu kwa jumuiya ya kimataifa.

• Ni wakati muafaka sasa kwa Sheria ya Huduma za Habari 2016 kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kwamba vifungu vyake vinaendana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa ukakika wa uhuru wa kujieleza.

• Tunamshauri Mhe Rais avione vyombo hivi vya habari kama wabia wazuri katika kupambana na rushwa nchini na asikubali kuona wasaidizi wake wanachukua hatua za kuwajengea hofu waandishi wa habari katika kuhabarisha mambo yanayohusu ufisadi na uhujumu uchumi.

• Vyombo vyote vya habari na wanahabari waweke tofauti zao pembeni na waamke kupigania uhuru wao wa kufanya kazi zaao kama katiba ya nchi inavyotaka.

• Kwamba waandishi wa habari na wahariri wachukue kwa uzito masuala yenye maslahi ya taifa na pia kusimamia maadili ya taaluma zao.

•  Tunashauri Sheria ya Huduma za Habari ifanyiwe marekebisho ili kuondoa vifungu vinavyompa mtu mmoja mamlaka ya kufungia chombo cha habari na kuweka mfumo shirikishi utakaoshirika wadau wengine wa vyombo vya habari katika kufuatilia makosa yanayofanywa na vyombo vya habari. 

• Kutokana na kuwa hakuna sehemu yoyote ya kupeleka rufaa dhidi ya maamuzi ya Waziri katika Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,  endapo hakutakuwa na mazungumzo na waziri, tutakwenda mahakamani kwa kushirikiana na Mawio kuonyesha haki zilizokiukwa katika kulifungia gazeti hili. 

Imetolewa kwa pamoja kati ya MCT, UTPC na THRDC leo Juni 18, 2017

Pili Mtambalike

Kaimu Katibu Mtendaji  Baraza la Habari Tanzania (MCT)

Onesmo Olengurumwa

Mratibu wa Taifa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)

Deogratius Nsokolo,

Rais – Umoja wa  Vilabu vya Waandishi Habari Tanzania-UTPC

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.