Majibu yasiyopendeza ya suala la Kibiti 

Kuna utaratibu wa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana kwa mujibu wa sheria na kwa wanaojitolea kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).  Mafunzo hayo yanawafaa sana vijana kwa kuwajengea ukakamavu na mbinu za kulinda nchi yao pale inapotokea zahama hasa kutokea nje ya mipaka ya nchi yetu.

Uzuri wa mafunzo hayo, hasa yale yanayotolewa kwa mujibu wa sheria, ni kuwaweka kwenye mtazamo wa pamoja vijana wanaotokea katika familia zinazotafautiana na kuzidiana kiuchumi. Wale wanaotokea kwenye familia zenye ukwasi mwingi na wanaotokea kwenye familia duni wanawekwa pamoja ili wawe na mtazamo wa pamoja, kuilinda na kuitumikia nchi yao bila hisia za kwamba wapo wanaohusika na jambo hilo wakati wengine wakijiona hawahusiki nalo.

Baada ya hapo vijana wanaendelea na shughuli zao, waliomaliza kidato cha sita wanaenda vyuoni kuendelea na elimu ya juu na waliomaliza vyuo vya chini kuanza kutafuta ajira katika sehemu mbalimbali. Tayari wanakuwa na uhakika wa kitu cha kufanya huku wakiwa kama akiba ya nchi katika ulinzi wa nchi yao.

Tatizo ninaloliona ni kwa wale wa kujitolea, ambao wengi wao wakishatoka JKT wanakuwa hawana shughuli maalumu za kufanya, huku serikali ikiwashauri wakajiajiri! Lakini hivi kwa yale mafunzo ya kijeshi iliyowapatia watajiajiri kwa kazi gani? Si ni lazima wakajaribu kujiajiri kwa kutumia mbinu walizopatiwa na serikali kule JKT?

Mfano mmoja mzuri wa hili nilisemalo ni wa hali tete iliyougubika mkoa wa Pwani. Tunashuhudia hali ya amani ilivyochafuka mkoani humo, na uchafuzi huo wa amani hauonekani kupangwa wala kutendwa na watu wa kawaida. Sababu Watanzania wa kawaida, wasio na mafunzo yoyote ya ukakamavu, wakiwaona askari tu, hata kama hawajashika silaha huanza kutetemeka na kutii kila wanachoelekezwa na askari hao.

Sio jambo la kawaida Watanzania “kuwakomalia”  askari kiasi cha kuwavizia na hata kuwashambulia bila sababu yoyote kama tulivyoshuhudia kule Rufiji. Ni lazima wahalifu hao wawe wamepata mafunzo rasmi, tena ya kijeshi na wala sio ya kimgambo.

Sababu sio rahisi kwa raia wa kawaida akajua namna ya kutumia silaha za kivita kufanya uhalifu wa aina hiyo. Ni lazima uhalifu huo utufumbue macho na akili. Tunatakiwa tuliangalie hilo la serikali kuwaita vijana wa kujitolea na kuwapatia mafunzo ya kijeshi na kisha kuwaachia wakajitafutie ajira. Hilo ni jambo la kuwa makini nalo.

Ama serikali ikishaamua kufanya hivyo, ni lazima itafute namna ya kuwadhibiti. Aidha kwa kuwapatia ajira ili wawe na uhakika wa kipato au kutowapa kabisa mafunzo hayo kama haina uhakika wa kuwadhibiti.

Sababu mtu uliyemfundisha kutumia silaha kubwakubwa ukimwambia akajiajiri, atafanya nini zaidi ya kutumia weledi uliompatia kujiajiri? Uliyemfundisha mbinu za kijeshi ni lazima atatumia mbinu hizo kujiajiri kijeshi. Hilo linaonekana zaidi ni kosa la aliyemfundisha kuliko yeye mwenyewe anayejiajiri!

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kwamba sio kila wazo jema linatoa matokeo mema. Alisema kuna wakati ili kuwapata vijana walio safi wa kujiunga na Jeshi la Polisi ilibidi kila mmoja achunguzwe tokea nyumbani kwake na athibitishwe na mjumbe wa nyumba kumi anakotokea kuwa ni kijana safi kitabia.

Lakini eti matokeo yake wakatafutwa vijana wakorofi waliokuwa wanasumbua jamii mahali wanakotokea ndio wakathibitishwa kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi! Lengo likiwa ni kuwaondoa makwao ili kupunguza ukorofi wao kwenye jamii walimoishi. Mwalimu alisema lengo lilikuwa safi lakini matokeo yakawa machafu!

Kwa hiyo, kinachowezekana kufanywa ni serikali kuwapatia mafunzo hayo ya ukakamavu na kujilinda vijana wachache ambao ina uhakika wa kuwaajiri na kuwadhibiti ili wasiishie kujiajiri wenyewe kwa kutumia mbinu za kijeshi. Kwa mtindo huo, itakuwa na uhakika wa kutunza amani tuliyo nayo huku ikiwa imewapatia ajira vijana hao.

Ni jambo la kusikitisha kuona serikali inaingia gharama kwa kodi za wananchi kutoa mafunzo kwa vijana isioweza kuwaajiri, kisha baadaye serikali hiyo hiyo iingie tena gharama kwa kodi za wananchi kuwadhibiti wale wale iliowapatia mafunzo wanapokuwa wameyageuza kuwa kitu cha kuivuruga amani ya wananchi wanaowalipia gharama za mafunzo hayo!

Kama nilivyosema mwanzo, JKT ni kitu kizuri kwa vijana iwapo kitatumika vizuri. Na ili kitumike vizuri, serikali haina budi kubadilisha utaratibu uliopo.

Badala ya kutoa mafunzo ya kijeshi, ingeanza kutoa tu mafunzo ya ukakamavu, hasa kwa wale ambao haina uhakika wa kuwapatia wote ajira, na kuanza kuwapa mbinu za ujasiriamali tu.

Yapo mafunzo ya aina mbalimbali kama ujenzi, ufundi seremala, ufundi wa cherehani nakadhalika. Vijana wakipatiwa mafunzo ya aina hiyo inakuwa muafaka kabisa, maana wakishamaliza muda wao wa JKT wanaweza kujiajiri katika taaluma hizo bila usumbufu wowote kwa wananchi. Kwa mtaji huo, serikali haiwezi kupata tena usumbufu wa kuingia gharama ya kuwaelekeza cha kufanya. Labda kama inawezekana kuwapatia vitendea kazi ili wakajiajiri, hata kama ni kwa kuvilipia baadaye.

Serikali haiwezi kuingia gharama ya kuudhibiti uhalifu iliouotesha yenyewe kwa kuwapatia vijana kitu ambacho ni kama mbinu za kuuanzisha uhalifu. Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa, uhalifu utakuwa umepungua kwa gharama nafuu na nchi kuwa ya amani kama ilivyokuwa kwa muda wote.

Kwa hiyo tunapoitafakari hali tete ya usalama mkoani Pwani, hatupaswi kuwaza tu tiba ya hali hiyo, bali pia tuangalie namna tunavyoweza kupata chanjo ya kitu hicho, kwa maana ya kutibu na kisha kuweka kinga ili ugonjwa usijigeuze dondandugu, unatibiwa baada ya muda mfupi unajirudia.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo anayeishi Dar es Salaam na anapatikana kwa anwani ya barua-pepe: prudencekarugendo@yahoo.com

0784989512

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.