Baada ya RITA kuwatambua wadhamini wa Lipumba, CUF yajibu

Chama cha Wananchi (CUF) kimewataka wanachama na viongozi wake wa ngazi mbalimbali kupuuzilia mbali hatua ya kusajiliwa kwa bodi ya wadhamini wa upande wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kikiita bodi hiyo kuwa ni “feki”. 

Taarifa iliyotolewa leo na kusambazwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa habari wa CUF, Salim Bimani, inasema Lipumba sio tu si mwenyekiti tena wa chama hicho, bali pia si mwanachama na ni “kibaraka” anayetumiwa kurejesha nyuma jitihada za Wazanzibari kupata haki yao ya ushindi wa uchaguzi wa Oktoba 2015. 

“Kibaraka Lipumba si mwenyekiti wa CUF. Anachofanya ni muendelezo wa kuhakikisha kuwa dhamira yake ya kujaribu kutaka kukivuruga Chama na kuzuia haki na maamuzi ya Wazanzibari ya Oktoba 25, 2015 isipatikane ili kuwafurahisha wanaomtumia,” inasema taarifa hiyo kwa vyombo vya habari. 
Hata hivyo, Bimani amekiri kupokea taarifa za kusajiliwa kwa bodi hiyo na Mamlaka ya Usajili ya Tanzania Bara (RITA) na baadaye kupata taarifa ya Profesa Lipumba kutaka kuwahoji “Katibu Mkuu, Maalim Seif,  Mhe Nassor Mazrui (Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar) na viongozi wengine waliowataja na anayoiita Kamati yake ya Maadili na Nidhamu.” 

Lakini taarifa hiyo inasema viongozi wa CUF wamejipanga vyema kukabiliana na “usaliti” huo. 

“Tunapenda kuwajulisha rasmi wanachama wetu kuwa hakuna kiongozi yeyote atakayekwenda kuhojiwa na kibaraka Lipumba na genge lake. Tunawapongeza wanachama na viongozi wote kwa utulivu na subra mnayoionyesha katika kipindi hiki wakati viongozi wenu wakibeba jukumu adhimu la kulishughulikia suala hili kwa weledi mkubwa huku ikimtambua adui yetu.”

Chama cha CUF kinapitia hivi sasa kwenye moja ya vipindi vigumu kabisa katika historia yake ya robo karne, baada ya Profesa Lipumba kuamua kujirejesha kwenye nafasi yake ya uwenyekiti aliyokuwa amejiuzulu kwa hiari yake Agosti 2015, akipinga ujio wa Edward Lowassa kwenye ugombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kile alichosema ni “kusutwa na nafsi” yake. 

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, anatajwa kumuunga mkono kwa kila hali Profesa Lipumba kwenye azma yake hii na mkono wake umekuwa ukionekana kwenye kila hatua. 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.