HABARI

Unyooshaji nchi uelekezwe mote 

Jitihada za kuikarabati nchi yetu, kama kweli zimekilenga kinachosemwa, kuitakatisha na kuiimarisha nchi, zielekezwe  kwenye maeneo yote kwa kupagusa kila panapoonesha kuleta dosari katika uimara na usafi wa nchi yetu, ndipo tutakapojivunia nchi iliyotakataka kwa uimara wake. Nchi iliyotakataka kiuchumi, kisisasa, kijamii, kiulinzi na kadhalika.

Hatuwezi kusema kwamba Tanzania imetakata kiulinzi na kiusalama wakati tunasikia katika sehemu mojawapo ya nchi baadhi ya wananchi wanafanyiwa unyama kama unaoendelea katika maeneo ya mkoa wa Pwani, hatuwezi kusema Tanzania imetakata wakati imejaa watu wanaolala mitaani, hasa watoto, kwa kukosa mahali pa kujihifadhi. Ni vigumu kusema kwamba Tanzania imetakata wakati inakosa ustaarabu wa kisiasa, demokrasia inaminywa kimabavu kinyume na Katiba ya nchi inavyoagiza, na kadhalika.

Lakini kwa leo, katika hayo niliyoyataja, nitakachokiangalia ni suala la kijamii, suala la wanaoitwa watoto wa mitaani. Itakuwa ni vigumu kusema kwamba nchi imepiga hatua kiuchumi wakati imejaa watoto wanaotangatanga wakiwa hawana matunzo, hawana pa kujihifadhi, hawana chakula cha uhakika na hawapati elimu.

Na kadri hali halisi ilivyo kasi ya watoto walio katika mazingira hayo hatarishi inazidi kuongezeka. Ikichukuliwa kuwa watoto ndio taifa la baadaye, uwepo wa ongezeko la watoto wa aina hiyo ni tishio kubwa katika mustakabali wa nchi. Taifa la baadaye litawezaje kujimudu kwa kuwategemea watu waliotelekezwa na kukulia mitaani?

Hilo ni bomu kubwa linalotegwa bila kuchukuliwa tahadhari za uhakika huku kila mtu, hususan viongozi, akiwa anaona na kushindwa kutoa kipaumbele katika jambo hilo. Ila uwezekano wa bomu hilo kuteguliwa bila madhara yoyote upo mkubwa.

Izingatiwe kwamba watoto hao wanaoitwa wa mitaani hawanyeshi kama mvua, wengi wao ni watoto wanaozaliwa katika njia haramu na baadaye kutelekezwa. Kwa kiasi kikubwa hilo ni tatizo linalosababishwa na unyama wa wazazi, hasa wa kiume, kwa wengi wao kulazimisha sitarehe za muda mfupi bila kujali kuwa matokeo yake yanaweza kuwa ya muda mrefu!

Kimtazamo hiyo haijatofautiana sana na mikataba yenye maslahi binafsi ya kuruhusu rasirimali za nchi kusombwa na kupelekwa ughaibuni, nyingine zikipelekwa kwa siri kupitia katika kinachoitwa makinikia, huku nchi ikibaki tupu na umasikini wake wa kulazimishiwa!

Kama nilivyosema mwanzo watoto ni taifa la baadaye, hiyo ni rasirimali ya nchi iliyo kubwa kuliko makinikia, maana taifa bila watu, hata liwe na makinikia ya kujaza dunia nzima, bado si lolote si chochote. Sababu taifa ni watu wanaopaswa kuzifaidi rasirimali za nchi yao.

Kwa hiyo kama ambavyo Rais Magufuli ameweza kufuatilia tulichodhani ni makinikia na kukuta kumbe ni ujambazi mkubwa ambao nchi yetu imekuwa ikifanyiwa kwa muda wote ukiwa umefichwa kwenye kitu hicho, makinikia, na baadaye kugundulika tofauti, ndivyo anavyopaswa kulitupia jicho jambo hili la “watoto wa mitaani” na kutafuta namna ya kulikomesha.

Wanaitwa watoto wa mitaani, kitu ambacho sio sahihi hata kidogo. Mitaa haizai, haijawahi kubeba mimba. Ukweli ni kwamba watoto hao wanazaliwa na kutelekezwa na watu walioishiwa ubinadamu, tena wengi wao wakiwa ni watu maarufu.

Zinahitajika mbinu za kuwatafuta na kuwapata wazazi hao waliovaa ngozi za ubinadamu kumbe ndani wakiwa ni wanyama wakatili kupitiliza. Kuwazaa watoto na kuwakana au kuwatelekeza kiasi cha watoto hao kugeuka wa mitaa!

Kuondolewa kwa jambo hilo, nina maana ya kuwabaini wazazi wa watoto husika, kutalipunguzia taifa mzigo usio wa lazima kama sio kuuondoa kabisa.

Njia ya kufanikisha jambo hilo ni nyepesi, wapo watoto wanaowaelewa wazazi wao lakini wazazi hao wakiwaruka na kutangaza bila haya kuwa hawawatambui japo jamii kwa kiasi kikubwa inaelewa kuwa hao ndio wazazi wao.

Wizara inayohusika na watoto ingeanzisha mchakato wa kuupata ukweli kuhusu jambo hilo. Kwa sasa teknolojia imepanuka katika kulithibitisha jambo hilo. Kila mzazi anayetajwa angelazimishwa kugharamia kipimo kiitwacho DNA katika kujua kama mtoto aliyemtaja ni wa kwake kweli au anasingiziwa.

Kitendo cha mzazi aliyetajwa kukatalia kipimo hicho moja kwa moja kinadhihirisha kuwa madai yaliyotolewa na mtoto ni halali kabisa, hata bila kupima mtu husika anatakiwa alazimishwe kumchukua mtoto wake na kumpatia matunzo yote yanayotakiwa kwa mtoto.

Na katika kuikomesha tabia hiyo haramu, tabia ya kinyama, vilevile kungekuwepo na adhabu kali kwa wote wenye tabia ya aina hiyo.

Hivi karibuni Rais Magufuli alitoa tamko kwamba wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni wasiruhusiwe kuendelea na masomo, hiyo ni sawa na kusema kwamba watelekezwe!

Kwa mtindo huo ni sawa na kusema hata  watoto watakaozaliwa nao watelekezwe. Moja kwa moja wasichana hao waliotelekezwa na mimba zao wanatarajiwa kuwazaa watoto wa mitaani! Kwa lugha nyingine watoto wa mitaani wanaandaliwa wakiwa mimba!

Hatuoni kwamba serikali inajiandalia yenyewe mzigo usio wa lazma kama nilivyooonesha hapo juu? Sababu kitendo cha kumnyima elimu msichana kisa kapata ujauzito tayari ni hukumu mbaya kwa mtoto ambaye bado ni mimba. Kosa la mtoto huyo ni lipi?

Maana asilimia kubwa ya wasichana wanaopata mimba wakiwa mashuleni ni ya kubakwa, kupitia kwenye vishawishi vya aina mbalimbali au kulazimishwa pale wanapojaribu kuviruka vishawishi hivyo. Wanaowabaka na kuwapa mimba wanatumia lugha za kihuni, “kuingia mitini au kusepa”, wanaishia kutojulikana wakiwa wamewaachia mizigo wasichana hao ya kuwaharibia maisha na watoto wanaozaliwa vilevile.

Lisipoangaliwa hilo ieleweke kwamba juhudi zote zinazofanyika za kuikwamua nchi toka kwenye tope la umasikini zitakuwa ni kazi bure, sawa na wasemavyo Wahaya “okutahira amaizi omurugega” yaani kuchotea maji kwenye tenga! Hiyo inashadidia usemi mwingine wa Kihaya alioutumia Rais Magufuli, “obwato buf’amagoba.”

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo. Anapatikana kwa barua pepe: prudencekarugendo@yahoo.com, na simu nambari +255784989512

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.