Majaliwa awang’ang’ania wanaopata ujauzito shuleni

Kwa mara nyengine tena, serikali ya Rais John Magufuli imepigia msumari kwenye msimamo wake wa kutokuwakubalia wanafunzi wa sekondari na msingi wanaopata ujauzito kurejea masomoni baada ya kujifunguwa, licha ya ukosoaji mkali kutoka ndani na nje ya nchi.

Akiakhirisha mkutano wa saba wa bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi leo Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia wabunge kwamba msimamo wa serikali unasalia kuwa ule ule uliotolewa na Rais Magufuli hivi karibuni, akidai kwamba huo si msimamo mpya, bali wa muda mrefu.

“Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki, kuchimba madini, n.k.” alisema Majaliwa, akiongeza kwamba takwimu za mwaka 2015 pekee zinaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito.

“Msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati. Msimamo huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili.”

Badala yake, alisema Majaliwa, jukumu la kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anasoma na haingii kwenye vitendo vinavyoweza kumpatisha ujauzito ni la kila Mtanzania. “Hivyo, ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito.”

Kwa kauli hii rasmi ya serikali ndani ya chombo cha kutunga sheria, kuna dalili kuwa sasa fursa ya kubadilisha mtazamo huo ni ndogo sana, licha ya kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inatajwa kuliweka hili la kuwahakikishia wasichana wanaopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kujifunguwa kuwa ni kipaumbele chake.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.