Baada ya kukung’utwa na madiwani wa Dar, sasa Lipumba atemwa na kanda 6 Bara 

Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) wa kanda sita za Tanzania Bara wameungana na madiwani 19 wa jiji kuu la kibiashara na kiuchumi, Dar es Salaam, kumkana mwenyekiti wa zamani wa chama chao, Profesa Ibrahim Lipumba, kwa madai yale yale ya kutumiliwa na kukisaliti chama hicho, ambacho ni sehemu muhimu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). 

Katika tamko la pamoja la makatibu wa kanda hizo lililotolewa jana (Julai 5) na kusambazwa kwa vyombo vya habari, uongozi wa CUF unatangaza kujitenga kando kabisa na kile kinachofanywa sasa na Profesa Lipumba na wafuasi wake, huku ukitoa wito wa kukomeshwa haraka. 

“… Lipumba hana ugomvi na Maalim Seif, bali ana ugomvi na Chama Wananchi – CUF.  Wanachama wa Chama cha Wananchi – CUF wa Tanzania Bara hatumuungi mkono Prof. Lipumba kama anavyotangaza katika vyombo vya habari siyo kweli, bali ni muongo mzandiki mkubwa anataka kuionesha jamii ya Watanzania kuwa kuna chuki baina ya CUF Tanzania Bara na CUF Zanzibar, nasi tunafahamu kwamba kuwatenganisha Wazanzibar na Watanzania Bara ni  kuvunja Muungano, hivyo Prof. Lipumba ni adui mkubwa wa Muungano,” inasomeka sehemu ya tamko hilo iliyotolewa baada ya mkutano wa viongozi hao mjini Dodoma katika ukumbi wa Social Hall hapo jana. 
Msimamo huu unakuja siku ile ile ambapo madiwani 19 wa jiji la Dar es Salaam waliitisha mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Peacock Hotel kwa dhamira hiyo hiyo ya kumkataa Profesa Lipumba na kundi lake. 

Mussa Kafana, Naibu Meya wa Jiji, aliwaambia waandishi wa habari kwa niaba ya wenzake kwamba “mikono ya Lipumba si salama kwa uhai wa CUF”. 

Itakumbukwa kwamba Profesa Lipumba, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa zaidi ya muongo mmoja, alijiuzulu wadhifa wake kwa hiyari yake mwezi Agosti 2015 akidai “nafsi ilikuwa inamsuta” kwa hatua ya chama chake kukubali ugombea urais wa Edward Lowassa kupitia UKAWA, ambayo iliundwa na yeye mwenyewe. 

Mwaka mmoja baadaye, bingwa huyo wa uchumi aliandika barua ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake kinyume na Katiba na taratibu za chama chake, lakini miezi mmoja baada ya barua yake hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, akamtangaza rasmi kumtambua Lipumba kama mwenyekiti wa CUF, hatua iliyokitia chama hicho kwenye mzozo mkubwa hadi leo. 

Tamko la makatibu hao wa kanda sita za Tanzania Bara, mbali na kumtuhumu Lipumba kutumiliwa na Jaji Mutungi kuivuruga CUF, linakwenda mbali zaidi kumtaka mwenyekiti huyo mstaafu kuondoka mara moja kwenye Ofisi Kuu za chama hicho za Buguruni. 

“… tunamtaka Ibrahim Lipumba atuachie Ofisi yetu (Ofisi Kuu) iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, mara moja na akaombe ajira kwa msajili wa vyama vya siasa ili ampangie kazi nyengine. Kama akiendelea kukaidi sisi wanachama tutakuja kuchukua ofisi yetu wenyewe mara moja.”
Kuhusu hatua ya Lipumba kusaidiwa na Wakala wa Usajili wa Tanzania Bara (RITA) kusajili kile wanachokiita bodi feki ya wadhamini, makatibu hao walisema wanasimama na uamuzi wa CUF kutokuitambua bodi hiyo pamoja na uongozi batili ulioiteuwa. 

“… Tunasikitika na kuhuzunishwa kwa kitendo cha Mkurugenzi wa RITA kuisajili Bodi ya Prof. Ibrahim Lipumba na genge lake kinyume kabisa na katiba yetu ya mwaka 1992 toleo la 2014, kifungu cha 98 (uk 90), ambacho kinaelezea Bodi ya Wadhamini ya chama cha CUF huteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo linapatikana kwa mujibu wa Ibara 79 (1) (m) uk. 69.”

Mbali ya kutomtambua Profesa Lipumba na kundi lake, makatibu hao wa kanda sita za Tanzania Bara wamesema wataendelea kuwajibika moja kwa moja kwa Katibu Mkuu Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad, na kuwataka makatibu wote wa wilaya kuandika taarifa zote za chama na kuzielekeza Makao Makuu ya chama, Mtendeni, Zanzibar, wakikumbusha masharti ya katiba ya chama chao, Ibara ya 123: “Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi wa Chama watakuwa na Ofisi zao Makao Makuu ya chama na, au Ofisi Kuu ya chama, lakini kiongozi yoyote aliyetajwa katika kifungu hiki anaweza kufungua Ofisi ya muda au kudumu katika sehemu nyingine ya nchi pindi akipata idhini ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.”

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.