Mapinduzi kwenye muziki ni muhimu 

KWA  mara ya kwanza Tanzania imeamua kuithamini sanaa ya muziki na kuichukulia kama njia mojawapo inayoweza kuwaingizia kipato halali wale wanaojihusisha nayo ikiwa ni pamoja na kuliingizia kipato taifa kwa njia ya kodi. Hiyo ni pamoja na kulitangaza taifa letu kwingineko duniani kupitia kwenye usanii huo.

 

Miaka ya nyuma muziki ulikuwa ni kwa ajili ya kusitarehesha tu hapa nchini kwetu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha shughuli za kisiasa.

 

Mfano Mbaraka Mwinshehe Mwaruka akiwa na Morogoro Jazi, aliimba wimbo wa “Makao makuu kuhamia Dodoma ni jambo la busara”, wengine wakaimba kuhusu kilimo cha kufa na kupona, mbuga zetu za Tanzania na nyimbo nyingine nyingi za kuwasifu viongozi wa nchi, hasa Baba wa Taifa.

 

Lakini nyimbo zote zilikuwa ni za kusitarehesha na kuhamasisha pasipo waimbaji kukipata kifuta jasho kinacholingana na umuhimu wa kazi walizozifanya.

 

Sote tunakumbuka kwamba mwanamuziki gwiji, Marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, alivyokufa mjini Mombasa, Kenya, kutokana na kukosa pesa ya kununulia damu ya kumuongezea baada ya kuwa amevuja sana kwenye ajali ya gari. Tuseme umasikini ndio uliomuua pamoja na yeye kufanya kazi kubwa ambayo ilitakiwa kumfanya tajiri mkubwa.

 

Lakini kwa kipindi hiki ambacho muziki umegeuka biashara ya kipato kikubwa katika eneo la Afrika Mashariki, tuliona jinsi kijana mmoja mwimbaji wa Uganda, Joseph Mayanja maarufu kama Chameleone, alivyoweza kujinusuru mwenyewe baada ya kupata ajali ya kudondoka toka ghorofani mjini Arusha.

 

Ingekuwa ni enzi hizo kwa sasa Chameleone angekuwa amebaki tu kwenye historia sawa na Mbaraka Mwinshehe. Lakini kwa uwezo alionao unaotokana na kazi yake ya usanii wa muziki aliweza kukodi helkopta ikamuwahishe kwenye hospitali kubwa kwa ajili ya matibabu mazuri. Huyo ni msanii wa muziki ambaye hajaweza kuifikia hata robo ya kazi ya Mbaraka Mwinshehe kwenye sanaa hiyo.

 

Kilichonisukuma kuandika makala hii ni tukio la “kuamka, kuanguka na kusimama tena” kwa Saida Karoli, msanii wa muziki wa asili. Katika tamasha lake la miaka 15 ya usanii wake wa kupanda na kushuka, waziri mwenye dhamana ya sanaa, Harrison Mwakyembe, kaeleza mambo mazuri ambayo bilashaka yamewapatia faraja wasanii wote wa muziki hapa nchini.

 

Mwakyembe kaonesha kwamba taifa limeanza kuwajali na kuwathamini wanamuziki likiwa linaelewa kwamba hata wao ni sehemu ya kuliingizia kipato kizuri. Kwahiyo nalo limeamua kujipanga katika kuhakikisha kazi ya wasanii inatambulika na kuheshimika kwa manufaa yao wenyewe na taifa kwa ujumla.

 

Mwakyembe pia kagusia suala la hatimiliki, ambalo kwa muda mrefu lilikuwa halifanyiwi kazi hapa nchini kwetu. Ilikuwa mtu anatoka jasho kubuni muziki ambao ulifurahiwa na wengi huku wengine wakiuiga muziki uleule na kujipatia kipato mgongoni mwa aliyeubuni bila malalamiko ya mhusika kutiliwa maanani.

 

Kusema ukweli hiyo haikuwa tofauti na ugaidi uliokuwa ukifanyika ndani ya sanaa ya muziki hapa nchini kwetu. Uharamia huo ndio,  kwa kiasi kikubwa,  uliokuwa ukidumaza vipaji vya wasanii ambavyo ni vingi hapa nchini.

 

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1980, mwanamuziki nguli wa Marekani, Marehemu Michael Jackson, aliingiza maneno fulani kwenye wimbo wake mmoja,  ya “mamase mamasama makosa” aliyoyatoa kwenye muziki wa Soul Makossa wa Emmanuel Dibango maarufu kama Manu Dibango wa nchini Cameroon.

 

Manu Dibango kuyasikia akaona utajiri tayari na kukimbilia mahakamani. Alipoulizwa Michael Jackson maneno hayo yana maana gani akajibu aliyapenda tu kwa vile yaliunogesha wimbo wake wa Wanna be startin’ somethin’. Palepale ikabidi Michael Jackson amlipe Manu Dibango dola milioni 500!

 

Fikiria kiasi hicho angekipata Saida Karoli kwa sasa angekuwaje? Ila maneno mengi toka kwenye nyimbo zake yamekuwa yakichukuliwa bila malipo yoyote huku yeye akirubuniwa kwa mambo madogomadogo wakati wanaoyatumia maneno hayo wakijipatia vipato vikubwa!

 

Jambo la kushangaza nimemsikia mtangazaji mmoja wa kituo kimojawapo cha redio akisema kwamba kwenye tamasha la Kusimama, kuanguka na kusimama tena la Saida Karoli, kaimba wimbo mmoja akitumia maneno ya Marehemu Ndanda Kosovo ya “ngambile kumtwala ma Kadogo, Kadogo omwana anchumbila akatoke, Kadogo anjungila akalamba, Kadogo anyalila ekinda, Kadogo bwaigoro kayo egyo siri yange”!

 

Hiyo imedhihirisha kwamba baadhi ya watangazaji wanasema maneno wasiyoyajua. Maana hayo ni maneno ya lugha ya Kihaya, Ndanda Kosovo ni Mkongo, sasa Mkongo na Kihaya wapi na wapi? Kwa taarifa maneno hayo ni ya Saida karoli mwenyewe aliyoyatumia muda mrefu kabla hajaibuliwa na wakuzaji wa vipaji “promoters”.

 

Alichokifanya Ndanda Kosovo ni kuyaiba kwa kusaidiwa na Wahaya aliofahamiana nao na kutangulia kuyarekodi, lakini ukweli ni kwamba huo ni ubunifu wa Saida Karoli mwenyewe. Wala Kosovo hakukielewa alichokuwa akikiimba.

 

Jambo alilolisahau Mwakyembe ni la kuwashauri wanamuziki wengi wa kinachoitwa kizazi kipya, vijana wa Bongofleva, kujifunza muziki kama kweli wanataka kuendelea kuitwa wanamuziki. Sababu muziki sio nyimbo wala mashairi, muziki unatoka kwenye ala.

 

Kwahiyo wanapotaka kuitwa wanamuziki wanapaswa kujifunza kucheza ala za muziki na kuwa nazo kama alivyo Saida Karoli. Yeye anakuwa nazo ngoma za kienyeji, manyanga, marimba nakadhalika. Sio anaitwa mwanamuziki akatumbuize mubashara anakuja na CD. Sababu CD ingeweza kuchezwa hata kama yeye hayupo.

 

Mwanamuziki akiitwa akatumbize mubashara anatakiwa afanye hivyo na sio kuwaachia watu wakasikilize CD huku yeye akifanya viini macho tu. Hicho ndicho kitu ninachokiona kuwa Saida Karoli anawazidi wanamuziki wengi wa kizazi kipya, uwezo wa kucheza muziki mubashara, kitu kinachomfanya aitwe mwanamuziki zaidi ya wanaoitwa wanamuziki bila kuwa na ala za muziki wala uwezo wa kuzitumia.

 

prudencekarugendo@yahoo.com

0784989512

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.