HABARI

Lipumba apingwa kila kona, sasa zamu ya Unguja

Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wa wilaya zote saba za kisiwa cha Unguja wamejitokeza hadharani kumpinga aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakimshutumu kwa kushirikiana na maadui kukiuwa chama chao. 

Wakizungumza na waandishi wa habari leo (Julai 9) katika Ofisi za CUF zilizopo Vuga, Mjini Unguja, wenyeviti na makatibu wa wilaya hizo wamesema Profesa Lipumba anashirikiana na mamlaka za dola kuvunja sheria za nchi kwa dhamira ya kukivunja kabisa chama chao.

“Tunalaani kwa nguvu zote na sauti kubwa hujuma zote zinazofanywa na Mamlaka za serikali zinazolenga kukiuka misingi ya sheria za nchi kwa lengo la kusajili bodi ya wadhamini ya Ibrahim Lipumba ili kumuwezesha kufanikisha uharamia wake dhidi ya CUF. Si tu kwamba hatua hizi, hasa zile za RITA na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa zinakwenda kinyume na sheria za nchi, bali pia kunaziondoshea heshima mamlaka hizo na kuwafanya wananchi kutoziamini na hivyo kuwashawishi kutafuta njia wanazozijua kuzuia uharamia dhidi ya chama chao walichokianzisha kwa gharama ya muda, fedha na uhai wa maisha yao,” inasema sehemu ya tamko lililosomwa na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mjini, Bi Mashavu Bakari.

Viongozi hao wamebainisha njama wanayosema inapangwa na serikali na kundi la Lipumba “kufungua matawi katika baadhi ya maeneo ya wilaya za Zanzibar kwa kuwatumia baadhi ya watu”, hatua ambayo wamesema inalenga kuendelea kuivuruga zaidi CUF. 

“Tunavitahadharisha vyombo vya Dola kuwa macho na hujuma hizi. Kinyume chake, sisi viongozi wa CUF wilaya za kisiwa cha Unguja tutatumia njia za kidemokrasia kwa kuzingatia sheria za nchi kukabiliana na kila aina ya uhuni dhidi ya CUF,” linaonya tamko hilo. 

Tangu Profesa Lipumba kuamuwa kujirejesha kwenye nafasi ya uwenyekiti wa CUF Taifa, mwaka mmoja baada ya kujiuzulu kwa hiyari yake, CUF imejikuta kwenye mzozo mkubwa kabisa wa kiuongozi kuwahi kukabiliana nao ndani ya kipindi cha robo karne ya uhai wake. 

Kundi la mchumi huyo linaonekana kupatiwa kila aina ya msaada na taasisi za dola katika kuhakikisha kile wafuasi wa CUF wanachosema ni “kuzuia haki ya Wazanzibari ya Oktoba 2015” isipatikane. 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.