CHADEMA yaungana na CUF kumng’oa Lipumba 

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinasema sasa kinauvaa mgogoro wa kiuongozi kwenye mshirika wake, Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kinadai kuhujumiwa na aliyekuwa mwenye wake, Profesa Ibrahim Lipumba. 
CHADEMA imezindua kampeni maalum yenye lengo la kumuondoa bingwa huyo wa uchumi ambaye alijiuzulu nafasi yake ya uongozi wa CUF mwezi Agosti mwaka 2015 na kisha kujirejesha katika mazingira ya kutatanisha mwaka mmoja baadaye. 

Operesheni hiyo iliyopewa jina la Operasheni Ondoa Msaliti CUF (OBM) imezinduliwa na CHADEMA kwa kushirikiana na viongozi wa CUF, baada ya kikao cha pamoja kilichofanywa na viongozi wa CHADEMA Kanda ya Pwani na wenzao wa CUF kujadili mgogoro ndani ya CUF na mustakabali wa chama hicho na vyama vinavyounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Saed Kubenea, Makamu Mwenyekiti Kanda ya Pwani ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) amesema: “Sisi kama Chadema kwa umakini kabisa tutawasaidia viongozi wa CUF na wanachama wao kumwondoa msaliti Prof. Lipumba Buguruni.”

“Katika hili pia tumeamua kila siku ambayo kesi ya CUF inaendeshwa mahakamani wanachadema tutajitokeza kuisindikiza CUF tunayoitambua; tumekubaliana Mameya wetu wote wa jiji la Dar es Salaam wasitoe ushirikiano kwa mtu yeyote wa vimelea vya Lipumba.”

Kwa upande wake, Dkt. Makongoro Mahanga, Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam amesema: “Chadema ni washirika wa CUF katika Ukawa. Hivyo tunaamini wanavyoyumbishwa CUF hata sisi hatuwezi kubaki sarama.”

“Tumeona tunaathirika. Makao makuu ya Chadema na CUF yapo katika kanda yetu. Tumejiridhisha kwamba mgogoro si kati ya Lipumba na Seif, ni kati ya dola. Tumeamua kupambana na dola kwa kuanza na hawa wasaliti wakiongozwa na Lipumba.”

Aidha, Riziki Ngwali, Mbunge wa Viti Maalum na Kiongozi wa Wabunge wa CUF bungeni, amesema “Tunataka pia Watanzania watambue kuwa mgogoro wa dola dhidi ya CUF ni wa kupandikizwa. Kwa sababu vyombo vyake vinatumika.”

Chanzo: Habari hii imeandikwa kwa msaada wa mtandao wa MwanaHalisi Online. 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.