Maalim Seif anaringia uadilifu wake

Maalim Seif Sharif Hamad

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ana sifa ya kuuthibitisha ukweli anaouamini hata akiueleza kwa namna ya kubashiri kinachoweza kuja mbele ya safari.

Sifa hii inaendana sana na mazoea yake ya kupenda kutembea na maneno yake. Akisema, anamaanisha. Akiahidi jambo, hulisimamia, akalitekeleza. Ni mambo yanayomsababishia kujivunia asili yake ya kujiamini na kuaminika.

Anajiamini kuwa kiongozi shupavu na muadilifu aliyeijenga CUF kufikia kuwa tishio lisilo mbadala mbele ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachovuta pumzi kwa kutumia visaidizi. Lazima kibwebwe na dola ndipo kiishi.

Karibu wiki mbili zilizopita, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutangaza jambo jipya linaloongeza uzito katika mwenendo ule ule wa kuthibitishia ulimwengu kuwa yeye si rahisi kushindwa kwa dhulma.

Na Jabir Idrissa

Amefichua tukio jingine baya linaloumbua watawala kwa vile walivyojitoa haya na kuamua kutumia taasisi za kidola kutekeleza mkakati wa kudhoofisha jitihada zake za kuwaongoza wananchi wa Zanzibar kuikamata serikali kutokana na ushindi wao ulioporwa wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Katika mkutano huo, Maalim Seif alibashiri kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini mwenye dhima ya kusimamia haki kwa usimamizi wenye ufanisi wa kumbukumbu muhimu za maisha ya binadamu, ufilisi na udhamini, naye ataingia mtegoni kama walivyoingia wengine na kukoleza mgogoro wa uongozi wa chama hicho uliopandikizwa.

Alisema wazi tayari uongozi wa RITA ulishaanza kushinikizwa kutekeleza matakwa ya watawala ya kuvuruga CUF, ili kuwavunja moyo viongozi wake katika jitihada wanazozifanya za kupigania haki ya Wazanzibari kupata uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wa ridhaa yao kama walivyoamua katika uchaguzi uliohujumiwa kwa kutangazwa umefutwa wote tarehe 28 Oktoba 2015.

Maalim Seif alisema Bodi ya Wadhamini ya CUF iliyopendekezwa kupitia ofisi yake, baada ya kuandaliwa kwa mujibu wa taratibu zote za kisheria zikiwemo zinazoelekezwa na Katiba ya chama hicho, itapigwa na chini, na penye sehemu yake, kuidhinishwa Bodi iliyopendekezwa na Profesa Ibrahim Lipumba, anayeongoza genge la waliofukuzwa uongozi pamoja naye baada ya kusaliti chama hicho.

Hakupotea na kweli hakukosea kitu. Ndivyo ilivyotokea. Wakala wa Usajili alikabidhi barua rasmi ya kuidhinisha bodi ya kundi hilo la Prof. Lipumba, mwanasiasa aliyejiuzulu uenyekiti kwa hiari yake tarehe 5 Agosti 2015, akitoa sababu ya kutoridhika na anavyochukuliwa na viongozi wake katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani pamoja na ule wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani wa Zanzibar.

Kwa hatua hiyo ambayo Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson aliikiri mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari waliokutana mjini Morogoro kwa semina ya kujenga mahusiano mema ya kikazi wiki moja baada ya kukubali kumridhisha kibubusa Prof. Lipumba kwa kumuidhinishia bodi aliyoelekezwa kuipendekeza, taasisi hiyo ilijiongeza kwenye orodha ya washiriki wa uchafu wa kuvunja sheria na katiba ya nchi kuhusu suala la upanuzi na uimarishaji wa demokrasia na utawala bora.

Viongozi wa CCM Zanzibar kwa kutambua mafanikio ya Maalim Seif kisiasa, baada ya kujikuta kimeadhibiwa kwa kukataliwa na umma, wameamua kujipakatisha mapajani mwa viongozi wenzao wa Tanganyika na kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama na kama inavyozidi kuthibitishwa hata na taasisi za kijamii ili kumhujumu.

Alipokutana na waandishi wa habari mara ya kwanza tarehe 9 Aprili 2017, alisema “si siri tena sasa kwamba kile kinachoitwa ‘mgogoro wa uongozi’ ndani ya CUF si chochote bali hujuma zilizopangwa na zinazoendeshwa na dola (serikali na vyombo vyake) kupitia njama ovu na mbinu chafu zilizolenga kuua upinzani makini nchini ikiwa ni sehemu ya kinachoonekana ni mkakati mpana wa kunyamazisha kila sauti inayothubutu kuwakosoa watawala.”

“Nataka ifahamike lengo la njama ovu na mbinu chafu hizi siyo CUF… ni upinzani na hasa UKAWA; na lengo pana zaidi ni kuua demokrasia inayokua Tanzania kwa kuhujumu na kuziua taasisi zote zinazoonekana ni nguzo za demokrasia (Tanzania).

Maalim Seif anatanua wigo wa kuzitathmini jitihada ovu za dola ya Tanzania chini ya CCM, kwa mgongo wa “mgogoro wa uongozi ndani ya CUF” na bila ya aibu wala haya, watawala hawajishughulishi kuamini kuwa wamekaa uchi na ni muhimu wakajifunika ili wasizidi kuadhirika.

Ni nini kama sio dola ya CCM kujidhalilisha inapothibitika kuwa RITA, baada ya kushikwa shingo, wamejiachia na kuidhinisha bodi ambayo haikupatikana kwa utaratibu wa kisheria na unaoelekezwa na Katiba ya CUF wa kuteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT)?

Kweli kabisa CCM hawapendi kuona CUF inabakia taasisi imara ya kuongeza nguvu ya ushawishi kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kweli nchini baada ya kuondoa mfumo uliooteshwa na watawala.

Sasa RITA, huyu wakala wa usajili, ufilisi na udhamini, anajikuta hana namna isipokuwa kuandaa mawakili wa kuisimamia katika kesi mpya iliyofunguliwa na CUF ikitaka itamkwe kuwa kilichofanywa na wakala huyo kuidhinisha bodi ya Prof. Lipumba ni udanganyifu unaostahili kuadhibiwa kisheria.

Shuruti ieleweke waziwazi hapa kwamba kwa kuidhinishwa Bodi iliyopendekezwa na Prof. Lipumba, kupitia msaidizi wake mkuu Magdalena Sakaya, aliyemteua kaimu Katibu Mkuu, akidharau hata uamuzi wake wa kupigania kuwa mwanachama baada ya kufukuzwa tarehe 26 Septemba 2016, watawala wanataka CUF isitulie na upinzani usishikane kuisumbua CCM.

Kwa maneno mengine, viongozi wa CCM wanafurahi kila wanapoona CUF wanavutana kwani hawatapata nafasi tena ya kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi kuwakurupusha watawala nje ya madaraka.

Ndipo Maalim Seif akatoa tahadhari kwamba kwa hali iliyofikiwa ya mkakati wa dola ya CCM, jamhuri inapelekwa katika kukabiliwa na mgogoro mkubwa usiowahi kushuhudiwa katika historia yake. Panahitajika mshikamano kuepusha hatari hiyo.

Tangu Maalim Seif alipokaza kamba ya kushawishi ulimwengu ikiwemo Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, nchini Uholanzi, kuhusu kuhujumu maamuzi ya wananchi kuchagua viongozi wawatakao Zanzibar, na jamhuri yenye mamlaka na vikosi vya ulinzi na usalama, CCM haijasimama kutapatapa.

Swali la msingi kwa nukta hii ni mwisho wa kutapatapa huko kwa CCM utakuaje? Wanaodhulumiwa wanaamini kuwa wataishinda tu CCM na itaanguka chini.

Hili amelisema wazi mwenyewe. “Nawaambia watawala walio nyuma ya njama na hujuma dhidi ya CUF msitulazimishe kutusukuma ukutani. Tutailinda CUF kwa gharama yoyote. mlio nyuma ya hujuma hizi mtabeba dhamana ya mnayoyaandaa. Wazanzibari na Watanzania wote wanaotuunga mkono na wapenda demokrasia ya kweli watasimama imara kulinda haki yao; ni wakati wa kulinda demokrasia ya kweli Tanzania.”

CCM wanaamini wakimhujumu Maalim Seif, watatawala daima. Hata sasa, wanatawala miili tu ya wananchi, si nyoyo zao maana walishaikataa CCM.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.